Jan 01, 2017 11:10 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 18-21 (Darsa ya 686)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 686, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 18 na 19 ambazo zinasema:

فَأَصْبَحَ فِي الْمَدِينَةِ خَائِفًا يَتَرَقَّبُ فَإِذَا الَّذِي اسْتَنصَرَهُ بِالأَمْسِ يَسْتَصْرِخُهُ قَالَ لَهُ مُوسَى إِنَّكَ لَغَوِيٌّ مُّبِينٌ

Akapambazukiwa mjini asubuhi akiwa na hofu na hadhari. Mara yule yule aliye mtaka msaada jana akawa anampigia kelele amsaidie. Musa akamwambia: Hakika wewe ni mpotevu dhahiri.

فَلَمَّا أَنْ أَرَادَ أَن يَبْطِشَ بِالَّذِي هُوَ عَدُوٌّ لَّهُمَا قَالَ يَا مُوسَى أَتُرِيدُ أَن تَقْتُلَنِي كَمَا قَتَلْتَ نَفْسًا بِالأَمْسِ إِن تُرِيدُ إِلاَّ أَن تَكُونَ جَبَّارًا فِي الأَرْضِ وَمَا تُرِيدُ أَن تَكُونَ مِنَ الْمُصْلِحِينَ

Basi Musa alipo taka kumshika kwa nguvu, yule aliye adui yao wote wawili akasema: Ewe Musa! Unataka kuniuwa kama ulivyo muuwa mtu jana? Wewe hutaki ila kuwa jabari katika ardhi, wala hutaki kuwa miongoni mwa wema.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa alipofikia rika la ujana, Nabii Musa (AS) alitoka kwenye kasri la Firauni na kuingia mjini kuchanganyika na watu. Katika kipindi hicho Bani Israil walikuwa wakidhulumiwa na kuonewa mno na Mafirauni pamoja na Waqibti. Alipokuwa mjini alikumbana na mkasa wa ugomvi uliotokea baina ya Mqibti na mtu mmoja wa Bani Israil ambapo Mqibti alikuwa amemzidi nguvu na kumpiga mtu wa Bani Israil. Nabii Musa akaingilia kati kumsaidia yule jamaa wa kaumu yake aliyekuwa akionewa na akampiga ngumi Mqibti, ambayo bila ya kutarajia ikawa ndio sababu ya kifo chake. Aya tulizosoma zinasema: Baada ya tukio hilo, Nabii Musa hakurudi tena kwenye kasri la Firauni bali aliendelea kubakia kule kule mjini kwa kificho, kwa sababu alichelea na kuhofia asije akakamatwa na askari wa Firauni. Lakini siku ya pili yake akamwona tena mtu yuleyule wa Bani Israil akipigana na mtu mwengine, na mara hii akamwita kumuomba amsaidie. Lakini kabla ya kufanya hivyo, Nabii Musa alimwambia yule mtu: Wewe ni mtu mjinga na usiye na busara; kwa sababu kila siku unatafuta kisingizio cha kugombana na kupigana na Mqibti huyu au yule na hivyo kuhatarisha maisha yako na ya wenzako. Haya unayoyafanya sio tu hayana faida yoyote bali yanawasababishia matatizo pia watu wa Bani Israil." Lakini pamoja na hayo, mtu huyo alikuwa ni madhulumu aliyetingwa na shari ya mtu dhalimu. Kwa hivyo Nabii Musa hakumwacha mkono bali alichukua hatua ya kumsaidia. Lakini badala ya kumpiga ngumi Mqibti, mara hii alimzuia barabara ili asiweze kumpiga na kumdhuru mtu yule wa Bani Israil. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika kupambana na adui tusiingie kichwakichwa bila ya mipango na mikakati na pasina kuangalia kama tija itapatikana, ili tusije kujitia matatizoni sisi wenyewe na wengine pia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tusiache kuwakosoa na kuwarekebisha wenzetu wanapokosea na wanapofanya sivyo, lakini sambamba na kufanya hivyo tusiwaache mkono mbele ya adui dhalimu anayewanyongesha. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba tusimame imara na kwa nguvu zetu zote kukabiliana na adui.

Darsa ya 686 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 20 na 21 ambazo zinasema:

وَجَاءَ رَجُلٌ مِّنْ أَقْصَى الْمَدِينَةِ يَسْعَى قَالَ يَا مُوسَى إِنَّ الْمَلَأَ يَأْتَمِرُونَ بِكَ لِيَقْتُلُوكَ فَاخْرُجْ إِنِّي لَكَ مِنَ النَّاصِحِينَ

Na akaja mtu kutoka mwisho wa mji akipiga mbio, akasema: Ewe Musa! Wakubwa wanashauriana kukuuwa. Basi toka! Hakika mimi ni katika wanao kupa nasaha.

فَخَرَجَ مِنْهَا خَائِفًا يَتَرَقَّبُ قَالَ رَبِّ نَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ

Basi akatoka (mjini) akiwa na khofu na hadhari. Akasema: Mola wangu Mlezi! Niokoe na watu madhaalimu.

Habari za yaliyojiri huko mjini zilifika kwenye kasri la Firauni. Za ugomvi na mapigano yaliyotokea baina ya mtu kutoka kaumu ya Baini Israil ambaye alikuwa mtumwa aliyepambana na Waqibti wawili, na tena basi ni katika siku mbili mtawalia; na pamoja na hizo, ni za kuhusu Musa, ambaye katika mara zote hizo mbili alimsaidia na kumuokoa mtumwa huyo wa Bani Israil dhidi ya Waqibti hao. Kusikia habari za aina hiyo lilikuwa jambo lisiloweza kuvumilika kwa wakuu wa kasri la Firauni, kwa hivyo kwa kauli moja wakaamua lazima Musa auawe ili mtu mwengine yoyote yule asije akathubutu kusimama kukabiliana na Waqibti. Lakini kabla askari waliotumwa kwenda kufanya kazi hiyo hawajachukua hatua, mtu mmoja katika jamaa wa karibu wa Firauni alibaini kilichokuwa kikiendelea; na papo hapo bila ya kupoteza muda aliondoka na kuelekea mjini ili kumpa habari Nabii Musa kuhusu yaliyoamuliwa dhidi yake na kumtaka aondoke mjini hapo haraka ili kunusuru maisha yake. Mtu huyo jina lake limetajwa katika maandiko ya historia kuwa ni Hazqil; na baada ya Nabii Musa kupewa Utume alisilimu na kumfuata Nabii huyo na akawa mashuhuri kwa jina la 'muumini katika watu wa Firauni'. Yeye pia kama alivyokuwa mke wa Firauni, Asia, japokuwa alikuwa akiishi kwenye kasri la Firauni lakini hakuukubali utawala wake, akawa anasubiri mapambano ya Nabii Musa dhidi ya taghuti huyo. Kwa hivyo alipoona hatua hiyo aliyochukua Musa (AS) alihisi mtu huyo anao ujasiri na uwezo unaotakiwa wa kuanzisha mapambano dhidi ya Firauni. Na ndipo akaamua aelekee mjini ili kuweza kumwokoa maisha yake kutokana na hatari iliyokuwa ikimkabili.

Alaa kulli hal, Nabii Musa aliipa uzito habari aliyopewa na mtu huyo na akaanza kuondoka mjini humo kwa hadhari kubwa. Alikuwa akitarajia kukumbana na tukio lolote kutoka kila upande; kwa hivyo alimwomba Mwenyezi Mungu ampe auni na msaada wake atoke nje ya Misri salama usalimini na kunusurika na shari ya madhalimu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba inakatazwa kuwasaidia madhalimu, lakini ni jambo jema la kufanya kujipenyeza ndani ya vyombo vya madhalimu ili kuweza kuwasaidia wanyonge na wanaodhulumiwa na kuzuia dhulma na uonevu zaidi dhidi yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kama tutafanya jambo kwa ajili ya Allah, tutakapokabiliwa na hatari, Yeye Mola atatusaidia na kutulinda. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba wakati mwengine upashaji habari kwa wakati na uchukuaji hatua kwa haraka huweza kubadilisha hatima na majaaliwa ya taifa zima la watu. Katika kisa cha Nabii Musa (AS), kama yule mtu wa kasri la Firauni asingemfikishia habari kwa wakati Mtume huyo wa Allah akaweza kuondoka mjini pale, si hasha pengine angekamatwa na askari wa Firauni na kuuawa. Kadhalika aya hizi zinatufunza kuwa inawezekana kuwepo watetezi wa haki miongoni mwa watu wanaoishi kwenye makasri ya fakhari, kama ambavyo inayumkinika kuwepo wafuasi na watetezi wa batili miongoni mwa jamii ya wanyonge na walalahoi. Almuhimu ni kwamba kigezo cha kumpimia mtu ni kufuata kwake haki na batili, na si maskani na mahala anapoishi. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuoneshe haki na atupe taufiki ya kuifuata, na atuoneshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/