Jan 01, 2017 11:12 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 22-25 (Darsa ya 687)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 687, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 22 na 23 ambazo zinasema:

وَلَمَّا تَوَجَّهَ تِلْقَاء مَدْيَنَ قَالَ عَسَى رَبِّي أَن يَهْدِيَنِي سَوَاء السَّبِيلِ

Na alipo elekea upande wa Madyana alisema: Asaa Mola wangu Mlezi akaniongoza njia iliyo sawa.

وَلَمَّا وَرَدَ مَاء مَدْيَنَ وَجَدَ عَلَيْهِ أُمَّةً مِّنَ النَّاسِ يَسْقُونَ وَوَجَدَ مِن دُونِهِمُ امْرَأتَيْنِ تَذُودَانِ قَالَ مَا خَطْبُكُمَا قَالَتَا لا نَسْقِي حَتَّى يُصْدِرَ الرِّعَاء وَأَبُونَا شَيْخٌ كَبِيرٌ

Na alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta kando yao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachungaji. Na baba yetu ni mzee sana.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa mmoja wa watu wa ndani ya Kasri la Firauni alimpa habari Nabii Musa kuwa wakuu wa kasri hilo wameshauriana na kuamua wamuue yeye Musa (AS), hivyo akamtaka aondoke mjini humo haraka iwezekanavyo. Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo na kueleza kwamba: Nabii Musa aliamua kuihama Misri iliyokuwa chini ya mamlaka ya Firauni na kuelekea ardhi ya Madyan kusini mwa Sham, ambayo ilikuwa nje ya mamlaka ya taghuti hiyo.

Hata hivyo safari hiyo ilikuwa na hatari zake pia; hatari ya kupotea njia na vilevile hatari ya kukamatwa na askari wa kasri la Firauni; hivyo akamwomba Mwenyezi Mungu amuongoze na kumuelekeza kwenye njia ya sawa. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba kabla ya Nabii Musa kuingia mjini Madyan, kwenye viunga vya mji huo alikutana na mkururo mkubwa wa kondoo waliokusanywa kando ya kisima cha maji huku wachungaji wao wakiwa wameshughulika kuteka maji kisimani na kuwanywesha wanyama wao hao. Lilikuwa jambo la kawaida na la kutarajiwa kwa Nabii Musa, ambaye alikuwa amechoka kutokana na mwendo mrefu wa safari kuelekea kisimani hapo ili alau apate maji ya kunywa na kunawa uso wake uliojaa vumbi. Lakini alipofika kisimani hapo aliona kando yake kitu cha ajabu kilichoipa mguso nafsi yake. Kulikuwepo na wanawake wawili, ambao kama walivyokuwa wachungaji wengine, nao pia walikuwa wameleta wanyama wao ili kuwapa maji, lakini walikuwa wamesimama kando kabisa wakiwachunga kondoo wao wasije wakachanganyika na kondoo wa wachungaji wengine. Nabii Musa, ambaye alistaajabishwa na mandhari hiyo, aliwauliza wanawake hao sababu ya kuwepo kisimani pale, lakini pia wakiwa wamejitenga na wanaume. Wanawake wale walimwambia: Baba yetu sisi ameshakuwa mzee, na kwa hivyo sisi tunalazimika kuwapeleka machungani kondoo wetu. Lakini kwa kuwa hatutaki kuchanganyika na wanaume, tunasubiri kwanza wao wawape kondoo wao maji na kwenda zao kisha ndipo na sisi tutasogea kisimani ili tukawape maji kondoo wetu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kujiweka tayari kuhajiri kutoka kwenye mji na nchi ni moja ya mambo yanayofanywa na warekebishaji wakubwa wa jamii ili kuweza kuwa na utayari wa kuvumilia tabu, misukosuko na matatizo yatakayowakumba katika mustakabali. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dua huwa inapata maana yake halisi baada ya mtu mwenyewe kujitutumua na kufanya jitihada; na si kuomba dua tupu bila ya kujitahidi wala kufanya bidii yoyote. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuchunga mpaka wa maingiliano baina ya mwanamme na mwanamke na kuepusha michanganyiko ya kiholela ya wanawake na wanaume katika sehemu za kazi ni jambo la maadili na ni tunu ya kidini. Ni kama walivyofanya mabinti wa Nabii Shuaib, ambao waliamua kutowapa maji kondoo wao mpaka walipoondoka wanaume, ili kuepuka kuchanganyika na kusongamana nao. Vilevile aya hizi zinatufunza kuwa endapo italazimu, mabinti wa Mitume hufanya kazi ya uchungaji, lakini hawawi tayari katu kudhalilika na kuwa ombaomba.

Tunaihatimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 24 na 25 ambazo zinasema:

فَسَقَى لَهُمَا ثُمَّ تَوَلَّى إِلَى الظِّلِّ فَقَالَ رَبِّ إِنِّي لِمَا أَنزَلْتَ إِلَيَّ مِنْ خَيْرٍ فَقِيرٌ

Basi (Musa) akawanyweshea; kisha akarudi kivulini, na akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mhitaji wa kheri utakayo niteremshia.

فَجَاءَتْهُ إِحْدَاهُمَا تَمْشِي عَلَى اسْتِحْيَاء قَالَتْ إِنَّ أَبِي يَدْعُوكَ لِيَجْزِيَكَ أَجْرَ مَا سَقَيْتَ لَنَا فَلَمَّا جَاءَهُ وَقَصَّ عَلَيْهِ الْقَصَصَ قَالَ لا تَخَفْ نَجَوْتَ مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ

Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea. Basi alipo mjia na akamsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwisha okoka na watu madhaalimu.

Nabii Musa, ambaye kutokana na hofu ya kudhuriwa na Mafirauni aliondoka Misri na kuelekea Madyan, alifika akiwa amechoka huku akiwa hajui wapi pa kwenda. Lakini pamoja na hayo aliyasahau machovu na matatizo aliyokuwa nayo akaamua kuwasaidia wanawake wale wawili kuteka maji kisimani na kuwapa kondoo wao. Baada ya kufanya kazi hiyo, na pasina kutaka ujira wowote kwao, alikwenda zake chini ya mti na kujipumzisha ili kupunguza machovu aliyokuwa nayo. Lakini njaa ilikuwa imembana ikambidi atafute chakula. Nabii Musa alikuwa mgeni katika mji huo na hakuwa akimjua mtu yeyote ambaye angeweza kumpokea yeye kama mgeni wake au yeye mwenyewe kuweza kupata kitu cha kula. Kwa hivyo alimwomba Mwenyezi Mungu amsahilishie na kumkidhia mahitaji yake ya chakula na makazi kwa namna atakayoona Yeye Mola ina maslaha. Kwa upande mwengine, mabinti wa Shuaib, siku ile waliwasili nyumbani kwao mapema zaidi ya kawaida yao. Hivyo baba yao akawauliza, 'kwani leo hamkuwapa kondoo maji hata mumerudi mapema kiasi hiki?' Mabinti wale wakamsimulia baba yao habari ya msaada waliopewa na Nabii Musa. Nabii Shuaib akawaambia: Nendeni kwa huyo mtu mumkaribishe nyumbani ili tuweze kumshukuru kwa alivyosumbuka kwa ajili yenu na kumlipa inavyostahiki kwa msaada aliokupeni. Mmoja wa mabinti wale, akiwa katika hali ya haya na staha kamili alimfuata Nabii Musa kule alikokuwa na kumwambia: "Baba yangu amekualika uje nyumbani kwetu ili akupe malipo ya kazi uliyotufanyia". Nabii Musa alihisi kutokana na maneno na mwenendo wa binti yule, kwamba lazima nyumbani kwao watakuwa ni watu safi na wenye heshima; na baba yao pia atakuwa mtu muungwana, kiasi kwamba hayuko tayari kuona kazi aliyoifanya yeye Musa ipite vivihivi bila ya kutolewa malipo. Kwa sababu hiyo aliukubali mwaliko wake; na kwa hakika vile alivyokuwa akidhani ilithibiti kuwa ndio ukweli halisi wa mambo. Kwa hivyo akafika nyumbani kwa Shuaib, mmoja wa Mitume wa Allah na kumsimulia kisa cha maisha yake kuanzia mwanzo hadi kuja kwake katika mji wa Madyan. Nabii Shuaib alimwambia Musa (AS), 'Mwenyezi Mungu amekuokoa na madhalimu; na wewe utakuwa mgeni wetu hapa kwa muda wowote ule upendao.' Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba hata tunapokuwa tumetingwa na matatizo tusisahau pia matatizo ya wenzetu; na tujitahidi kadiri ya uwezo wetu kuwasaidia na wao kutatua matatizo yanayowakabili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tumwombe Mwenyezi Mungu atutatulie Yeye matatizo yanayotukabili, na kutuwekea njia na sababu za kuyatatulia kwa namna yenye kheri na sisi. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba katika mafundisho ya Mitume hakuna kizuizi kwa mwanamke kushiriki katika masuala ya kijamii; lakini kwa sharti tu kwamba yeye mwenyewe ajistahi na awe na murua, na vilevile kuchungwa mipaka ya mchanganyiko baina ya mwanamke na mwanamme. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa tuthamini tunavyohudumiwa na watu na tuonyeshe shukrani kwao kwa njia mwafaka. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 687 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah ajaalie ahli zetu pamoja na vizazi vyetu viwe vitulizo vya macho yetu, atuzidishie pia mapenzi baina yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/