Suratul Qas'as 26-28 (688)
Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 26-28 (Darsa ya 688)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 688, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 26 ambayo inasema:
قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الأَمِينُ
Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Musa (AS) aliwasaidia mabinti wa Nabii Shuaib (AS) kuwanyweshea maji kondoo wao; na kwa sababu hiyo Nabii Shuaib akamwalika na kumkaribisha nyumbani kwake ili kumlipa malipo ya kazi aliyowafanyia. Aya tuliyosoma inaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Yule binti aliyetumwa na baba yake akamfuate Nabii Musa ili kumwalika nyumbani kwao na akamwongoza hadi huko, alimshauri baba yake amwajiri Musa kwa kazi ya uchungaji ili wao watoto wa kike wasilazimike tena kila siku kufanya kazi ya kupeleka na kurudisha kondoo malishoni. Katika shauri na pendekezo alilolitoa binti huyo aliashiria sifa mbili za Nabii Musa: Ya kwanza ni nguvu za kiwiliwili na ya pili ni uaminifu. Nguvu za kimwili za Nabii Musa zilibainika wakati alipokuwa akivuta juu madoo mazito ya maji kutoka kisimani na kuwanywesha kondoo wote wa Nabii Shuaib. Na uaminifu wake na usafi wake wa kimaadili ulidhihirika wakati alipokuwa njiani kuelekea nyumbani kwa Shuaib; ambapo badala ya kumwacha binti yake atangulie mbele ili amwongoze njia; yeye Musa (AS) aliamua kutangulia mbele; na kila pale ilipolazimu alimuuliza kutokea nyuma binti wa Nabii Shuaib amwongoze njia, ili jicho lake lisije likaangukia kwa binti huyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba watoto, wawe wa kike au wa kiume, wana haki ya kupendekeza kwa wazee na wakubwa wao wa familia kile ambacho kwa maoni yao, na kwa hoja na mantiki, wanahisi kuwa ni sahihi; na katika hili hakuna tofauti baina ya msichana na mvulana. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa katika kuchagua na kuajiri watu kwa ajili ya kazi fulani, tunatakiwa tuwachague wale wanaofaa zaidi kuifanya kazi hiyo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba sifa mbili za uwezo na uaminifu; au kwa maneno mengine, kuwa na utaalamu na kuaminika kiimani na kimaadili ndivyo vigezo vinavyopasa kutumiwa katika kuwapa watu vyeo na mas-ulia ya kazi na uongozi.
Darsa yetu ya 688 inahatimishwa na aya ya 27 na 28 ambazo zinasema:
قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ عَلَى أَن تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ وَمَا أُرِيدُ أَنْ أَشُقَّ عَلَيْكَ سَتَجِدُنِي إِن شَاء اللَّهُ مِنَ الصَّالِحِينَ
Akasema: Mimi nataka kukuoza mmoja wa mabinti zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane. Ukitimiza kumi ni khiari yako; lakini mimi sitaki kukutaabisha. Inshallah utanikuta miongoni mwa watu wema.
قَالَ ذَلِكَ بَيْنِي وَبَيْنَكَ أَيَّمَا الأَجَلَيْنِ قَضَيْتُ فَلا عُدْوَانَ عَلَيَّ وَاللَّهُ عَلَى مَا نَقُولُ وَكِيلٌ
Musa akasema: Hayo yamekwisha kuwa baina yangu mimi na wewe. Muda wowote kati ya miwili nikiumaliza sitiwi ubayani. Na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi juu ya haya tunayo yasema.
Nabii Shuaib (AS) aliukubali ushauri aliopewa na binti yake kuhusu kumwajiri Nabii Musa kwa kazi ya kumchungia kondoo wake. Lakini asingeweza kukubali kijana mwanamme ambaye hajaoa aishi nyumbani kwake ambako kuna mabinti zake wawili. Kwa hivyo alimpendekezea Nabii Musa amuoe mmoja wa mabinti hao ili aweze kuishi nyumbani mwao. Lakini kwa kuwa alitaka kazi ya uchungaji na upelekaji kondoo malishoni pia isilale, aliwekeana naye masharti kwamba baada ya kumuoa binti yake, abaki pamoja nao kwa muda angalau wa miaka minane na kuendelea kufanya kazi hiyo ya uchungaji. Alikuwa hataki iwe kwamba, baada ya Nabii Musa kuoa amchukue mke wake na kumtenganisha na familia yake; kwani kwa kufanya hivyo, sio tu hatokuwa amewapa msaada wowote bali atakuwa amemuondolea yeye Shuaib mmoja wa mabinti zake wawili ambao ni wasaidizi wake katika kazi ya uchungaji. Kwa hivyo alitoa sharti hilo la kumuozesha Nabii Musa binti yake mkabala wa kumfanyia kazi ya kumfugia kondoo wake, hali itakayokidhi maslahi na manufaa kwa pande zote mbili. Kwa upande mmoja tatizo la makazi, mke na kazi ya kuendeshea maisha kwa Nabii Musa likawa limetatuka, na kwa upande mwengine badala ya mabinti wa Nabii Shuaib kwenda kuchunga kondoo majangwani kusiko na usalama wangeweza sasa kubaki nyumbani kwao katika hali ya usalama huku wakidhaminiwa pia mahitaji ya maisha ya familia yao. Nukta moja ya kuzingatia hapa ni kwamba kufanya kazi ya uchungaji Nabii Musa kwa muda wa miaka minane, iwe ni kwa hesabu ya mahari ya binti wa Nabii Shuaib au kwa sura ya sharti la kufunga naye ndoa lilikuwa ni pendekezo na takwa la binti mwenyewe; na manufaa yake yalikuwa yanarejea kwa binti huyo, si kwa baba yake. Kwa sababu wakati binti anapolazimika kwenda majangwani kila siku kutokana na uzee wa baba yake ili kupeleka kondoo malishoni, bila ya shaka angetamani apate mume shababi, shupavu na msafi kimaadili ambaye atabeba jukumu la kuifanya kazi hiyo ili angalau yeye aweze kuutua mzigo huo mzito uliokuwa umemuelemea. Lakini pia wakati Nabii Shuaib alipompa Nabii Musa pendekezo hilo alimsisitizia kwamba ‘sisi hatutaki kukutaabisha na kukutia mashakani; hivyo nawe pia kama una fikra na mawazo yoyote tueleze tutasikiliza.’ Nabii Musa alilikubali pendekezo la kupewa mke kwa sharti la kuwafanyia kazi ya uchungaji na akasema: Nitabakia hapa kwa muda wa miaka minane na kutekeleza sharti ulilonipa. Na ikiwa nitataka kubakia kwa miaka miwili zaidi nitaendelea kufanya kazi ya uchungaji ili kuweza kukidhi mahitaji ya maisha yangu mwenyewe na yenu pia.
Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba haikatazwi kwa baba au watu wa kaumu ya msichana kupendekeza binti yao huyo aolewe na kijana mchamungu, mwaminifu na msafi kimaadili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kufunga ndoa kunalitangulia suala la ajira ili mazingira ya mchanganyiko baina ya wanawake na wanaume yawe salama. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika kuainisha mahari ya binti anayetaka kuolewa tuzingatie pia uwezo wa kifedha wa mposaji na kutomdhikisha kwa sababu ya uwezo mdogo alionao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 688 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azitie baraka ndoa zetu, aviongoe vizazi vyetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/