Suratul Qas'as 29-32 (689)
Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 29-32 (Darsa ya 689)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 689, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 29 ambayo inasema:
فَلَمَّا قَضَى مُوسَى الأَجَلَ وَسَارَ بِأَهْلِهِ آنَسَ مِن جَانِبِ الطُّورِ نَارًا قَالَ لِأَهْلِهِ امْكُثُوا إِنِّي آنَسْتُ نَارًا لَّعَلِّي آتِيكُم مِّنْهَا بِخَبَرٍ أَوْ جَذْوَةٍ مِنَ النَّارِ لَعَلَّكُمْ تَصْطَلُونَ
Basi Musa alipo timiza muda wake na akasafiri na ahali zake, aliona moto upande wa Mlima T'uri. Akawaambia ahali zake: Ngojeni! Mimi nimeona moto, pengine nitakuleteeni kutoka huko khabari au kijinga cha moto ili mpate kuota moto.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Musa (AS) alifunga ndoa na binti wa Nabii Shuaib (AS). Na akakubali kuwafanyia kazi ya kuwachungia kondoo wao kwa muda wa angalau miaka minane na kama atataka aongeze miaka miwili mingine ya kubakia hapo na kuendelea na kazi hiyo. Baada ya hayo aya tuliyosoma inasema: Musa (AS) aliyatimiza yale aliyoahidi kuyafanya; na baada ya kufanya kazi ya uchungaji kwa muda wa miaka 10 alimchukua mkewe na wanawe kwa ajili ya kufunga safari ya kurudi kwenye ardhi yake ya asili yaani Misri. Lakini safari yenyewe ilikuwa ndefu na yenye hatari nyingi. Wakati walipofika ardhi ya Sham, ulipoingia usiku walipotea njia, hivyo wakawa wanamtafuta mtu anayeijua njia ili wamuulize apate kuwaelekeza. Wakiwa katika hali hiyo, Nabii Musa aliona moto kwa mbali kwenye bonde la Mlima Turi. Akawa anajiambia: Mtu aliyeuwasha moto ule, bila ya shaka atakuwa anazijua njia za mahala hapa, hivyo ataweza kutuongoza. Isitoshe katika usiku huu wa baridi na giza nitapata kijinga cha moto na kuwaletea ahli zangu ili kiweze kuwapa joto. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mwanamme ni mas-uli wa kukidhi mahitaji ya mke wake na watoto wake; na familia yake nayo inatakiwa iwe pamoja naye kumsaidia katika kutatua matatizo ya kimaisha yatakayowakabili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mtu kuwa na mapenzi ya wat’ani na kwao alikozaliwa ni jambo la kimaumbile; na kila mtu, hata baada ya kupita miaka mingi ya kuishi mbali na kwao, hurejea kwenye ardhi yake ya asili alikotoka. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Musa (AS) ambaye alipitisha muda mrefu wa maisha yake kwenye kasri ilimpasa atumie muda wa miaka 10 kufanya kazi ya uchungaji majangwani ili kujivua na mazoea na raha za maisha ya kwenye kasri na kujiandaa kuhimili na kuyavumilia matatizo na misukosuko mikubwa itakayomkabili siku za usoni.
Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 30 ambayo inasema:
فَلَمَّا أَتَاهَا نُودِي مِن شَاطِئِ الْوَادِي الأَيْمَنِ فِي الْبُقْعَةِ الْمُبَارَكَةِ مِنَ الشَّجَرَةِ أَن يَا مُوسَى إِنِّي أَنَا اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ
Basi alipo ufikia aliitwa kutoka ng'ambo ya bonde la kuliani katika eneo lilio barikiwa kutoka kwenye mti: Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Kwa mujibu wa hadithi, wakati Nabii Musa alipoukaribia moto alibaini kuwa moto huo ulikuwa tofauti kabisa na moto mwengine wowote aliowahi kuuona kabla. Moto huo ulikuwa ukitoa cheche zake kutoka kwenye mti wa kijani kibichi na si mkavu uliokauka. Na macheche ya moto wenyewe yalikuwa yakitoa nuru na mwangaza tu bila ya kuwa na joto wala muunguzo wowote.
Nabii Musa alikuwa katika hali ya kufikiri na kuwaza; ni moto wa aina gani huu, mara akasikia sauti ikimlingania na kumwambia: “Ewe Musa, aliyekuleta wewe hapa ni mimi, ambaye ni Muumba na mwenye mamlaka juu yako wewe na ulimwengu mzima.”
Ukweli ni kwamba Mwenyezi Mungu SW aliyatumia maneno na kuzungumza kwa njia hiyo na mja wake Musa (AS). Kusemezwa ambako kulimpambanua Nabii Musa na Mitume wengine na kujulikana kwa lakabu ya ‘Kalimullah’ yaani msemezwa na Allah. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika utamaduni wa kidini mwahala mnamonasibishwa na Mwenyezi Mungu huwa ni sehemu takatifu hata kama utakuwa ni mlima au jangwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Nabii Musa alikwenda Mlima Turi kwa madhumuni ya kuwachukulia ahli zake kijinga cha moto na ili kuweza kuelekezwa njia, lakini alipofika huko Mwenyezi Mungu alimkabidhi jukumu na mas-ulia ya kuwafikishia watu wito wa uongofu. Kwa maneno mengine, wajibu wetu sisi ni kufanya juhudi na harakati lakini kuhusu tija itakayopatikana, hilo haliko mikononi mwetu.
Darsa ya 690 ya Qur’ani inahatimishwa na aya ya 31 na 32 ambazo zinasema:
وَأَنْ أَلْقِ عَصَاكَ فَلَمَّا رَآهَا تَهْتَزُّ كَأَنَّهَا جَانٌّ وَلَّى مُدْبِرًا وَلَمْ يُعَقِّبْ يَا مُوسَى أَقْبِلْ وَلا تَخَفْ إِنَّكَ مِنَ الآمِنِينَ
Na tupa chini fimbo yako. Basi alipo iona ikitikisika kama nyoka, aligeuka kurudi nyuma wala hakutazama. (Akaambiwa): Ewe Musa! Njoo mbele wala usiogope. Hakika wewe ni miongoni mwa walio salimika.
اسْلُكْ يَدَكَ فِي جَيْبِكَ تَخْرُجْ بَيْضَاء مِنْ غَيْرِ سُوءٍ وَاضْمُمْ إِلَيْكَ جَنَاحَكَ مِنَ الرَّهْبِ فَذَانِكَ بُرْهَانَانِ مِن رَّبِّكَ إِلَى فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا فَاسِقِينَ
Ingiza mkono wako kwenye mfuko wako, utatoka mweupe pasipo na ubaya. Na jiambatishe mkono wako ukihisi khofu. Basi hizi ni dalili mbili zitokazo kwa Mola wako Mlezi kumpelekea Firauni na wakuu wa umma wake. Hakika hao walikuwa watu mafaasiki.
Lilikuwa jambo la kutarajia kwamba kwa kusikia sauti ambayo hakuizoea na wala hajawahi kuisikia kabla yake na kuona mandhari ile na moto ule wa ajabu, Musa (AS) alikuwa na haki ya kupatwa na mshangao na mfadhaiko wa kujiuliza hii ni sauti gani, na hii ni mandhari ya aina gani? Hivyo ili kumkamilishia ithbati na kumhakikishia kwamba kile anachokisikia na kukiona kinatoka kwake Yeye, Allah SW alimuonyesha Mtume wake huyo miujiza mikubwa miwili. Mmoja ni wa fimbo yake Musa kugeuka nyoka, na mwengine ni wa kung’ara kiganja cha mkono wake. Kwa kuona miujiza hiyo miwili, Nabii Musa alibainikiwa na hakika ya kile alichokisikia; kisha baada ya hapo akaamrishwa na Allah arejee Misri akiwa na miujiza hiyo. Jukumu la kwanza kabisa alilopewa kutekeleza lilikuwa ni kwenda kwenye kasri la Firauni ambako alipitisha kipindi kirefu cha maisha yake. Lakini mara hii ilikuwa ni kwenda kwa lengo la kumlingania Tauhidi Firauni ya kumwamini Mungu mmoja wa haki na kuacha kuwatendea dhulma na uonevu Bani Israil. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mtu huweza kuwaongoza watu wengine kwenye njia ya uongofu baada ya yeye mwenyewe kuwa na imani ya yakini juu ya njia hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ili kuleta mageuzi na marekebisho ya msingi ya jamii inapasa kuuendea kwanza mzizi na chimbuko la dhulma na ufisadi wa jamii yenyewe. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba hofu na kukimbia hatari ni miongoni mwa sifa za kimaumbile za mwanadamu; na hakuna tofauti katika hilo baina ya Mitume na wanadamu wengine. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah awape Waislamu nguvu na uwezo wa kuwakabili mataghuti wa zama hizi. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/