Jan 01, 2017 11:27 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 33-37 (Darsa ya 690)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 690, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 33 na 34 ambazo zinasema:

قَالَ رَبِّ إِنِّي قَتَلْتُ مِنْهُمْ نَفْسًا فَأَخَافُ أَن يَقْتُلُونِ

Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nilimuua mtu katika wao, kwa hivyo nahofia wataniua.

وَأَخِي هَارُونُ هُوَ أَفْصَحُ مِنِّي لِسَانًا فَأَرْسِلْهُ مَعِيَ رِدْءًا يُصَدِّقُنِي إِنِّي أَخَافُ أَن يُكَذِّبُونِ

Na ndugu yangu Harun ni fasihi zaidi ulimi wake kuliko mimi. Basi mtume ende nami kunisaidia, ili anisadikishe. Hakika mimi nina khofu watanikadhibisha.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa katika Mlima Turi, Mwenyezi Mungu SW alimwamuru Nabii Musa (AS) aende kwa Firauni na kumlingania wito wa tauhidi yeye na watu wake wa karibu. Baada ya hayo, aya tulizosoma zinasema: Katika safari hiyo ya kwenda kutekeleza jukumu hilo Nabii Musa alishtakia kwa Mola wake matatizo mawili yanayomkabili mbele yake. La kwanza ni tukio la kumsaidia jamaa yake wa Bani Israil katika ugomvi na Mqibti lililosababisha kuuawa Mqibti huyo na hatimaye askari wa kasri la Firauni kuanzisha msako wa kutaka kumkamata yeye ili auliwe kwa sababu ya tukio hilo. Amma kuhusiana na tatizo la pili, Nabii Musa alisema: Ulimi wangu si mwepesi na sina ufasaha wa kutosha; hivyo huenda sitoweza kuitekeleza kazi hii nzito peke yangu. Kwa hiyo naomba ndugu yangu Harun awe pamoja nami ili kunisaidia kukabiliana na ukadhibishaji wa kina Firauni; na kwa ufasaha wa kuzungumza alionao anisadie katika kutetea haki na ukweli wa wito wangu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wakati tunapokubali kubeba mas-ulia ya jambo tunapaswa kubainisha kwa ukweli na uwazi kabisa udhaifu wetu na matatizo tutakayokabiliana nayo na kupendekeza njia mwafaka za kurekebisha kasoro hizo na kutatua matatizo hayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuzungumza kwa fasaha ni miongoni mwa mambo yenye taathira katika kuwavutia watu na ni moja ya nyenzo zinazohitajika ili kuweza kupata mafanikio katika tablighi. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba tusiache kutumia uwezo na suhula za watu wengine katika kutekeleza majukumu na mas-ulia mazito. Tumtumie kila mtu na kitu katika mahala panapostahiki; na si lazima kwamba kazi zote tuzifanye sisi wenyewe peke yetu.

Ifuatayo sasa ni aya ya 35 ambayo inasema:

قَالَ سَنَشُدُّ عَضُدَكَ بِأَخِيكَ وَنَجْعَلُ لَكُمَا سُلْطَانًا فَلا يَصِلُونَ إِلَيْكُمَا بِآيَاتِنَا أَنتُمَا وَمَنِ اتَّبَعَكُمَا الْغَالِبُونَ

(Mwenyezi Mungu) akasema: Tutautia nguvu mkono wako kwa nduguyo, na tutakupeni madaraka, hata wasikufikilieni. Kwa sababu ya Ishara zetu nyinyi na watakao kufuateni mtashinda.

Allah SW alimkubalia ombi lake Mtume wake Musa (AS). Akamkubalia ndugu yake Harun awe pamoja naye katika njia hiyo yenye hatari nyingi ili awe msaidizi wake, na kwa njia hiyo matatizo yote mawili ya Nabii Musa yaweze kutatuka. Kwanza asitokee mtu yeyote atakayethubutu kumdhuru au kutaka kumuua yeye Musa (AS). Na pili kwa kuwepo Harun pamoja naye mbele ya hadhara ya Firauni na watu wake waweze kwa pamoja kuwabainishia ukweli wa ujumbe wao kwa mantiki wadhiha na hoja za wazi na kuwashinda kutokana na miujiza ya Allah watakayoionesha. Japokuwa Harun alikuwa mkubwa kiumri kuliko Nabii Musa, na pia hodari zaidi na mwenye fasaha zaidi katika uzungumzaji, lakini Nabii Musa alikuwa amekomaa kwa sifa za ukamilifu wa kiutu zilizomfanya ateuliwe na Allah kuwa Mtume wake mwenye kuteremshiwa Kitabu na Sharia. Na japokuwa kaka yake Harun, naye pia alikuwa Mtume lakini ilibidi awe msaidizi wake wa kuwa pamoja naye na kumsaidia; kwanza katika kuonyesha miujiza ya kumshangaza na kumvunja nguvu Firauni; na pili kumshinda kwa hoja taghuti huyo kwa kutumia kipaji chake cha ufasaha wa kuzungumza. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika kupambana na batili, si lazima idadi ya pande mbili za haki na batili iwe sawa. Wakati mwengine watu wawili tu wenye hoja zilizo wazi na madhubuti wanaweza kuushinda umati mkubwa wa upande wa batili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa tunapaswa kuwahami na kuwalinda watu wa njia ya Mwenyezi Mungu na wafuasi wa haki ili wasiweze kufikiwa na kudhibitiwa na mkono wa madhalimu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba hata Mitume wa Allah wanahitaji kupewa matumaini na hakikisho juu ya hatima na mustakabali wa harakati yao. Mwenyezi Mungu (SW) aliwapa ahadi ya ushindi Musa, Harun (AS) na wafuasi wao na kuwafanya wawe na matumaini katika njia yao.

Aya ya 36 na 37 za Sura yetu ya al-Qas’as ndizo zinatuhatimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

فَلَمَّا جَاءَهُم مُّوسَى بِآيَاتِنَا بَيِّنَاتٍ قَالُوا مَا هَذَا إِلاَّ سِحْرٌ مُّفْتَرًى وَمَا سَمِعْنَا بِهَذَا فِي آبَائِنَا الأَوَّلِينَ

Basi alipo wafikia Musa na Ishara zetu zilizo wazi, walisema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio zuliwa. Na hatukuyasikia haya kwa baba zetu wa zamani.

وَقَالَ مُوسَى رَبِّي أَعْلَمُ بِمَن جَاءَ بِالْهُدَى مِنْ عِندِهِ وَمَن تَكُونُ لَهُ عَاقِبَةُ الدَّارِ إِنَّهُ لا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ

Na Musa akasema: Mola wangu Mlezi ni Mwenye kujua kabisa nani anaye kuja na uwongofu unao toka kwake, na nani atakaye kuwa na mwisho mwema wa makaazi. Hakika wenye kudhulumu hawatafanikiwa.

Nabii Musa na ndugu yake Harun (AS) walifanya kila njia mpaka wakaweza kufika kwenye kasri la Firauni na mbele ya hadhara ya taghuti huyo na wasaidizi wake. Baada ya kuwafikishia wito wa tauhidi wa kumwamini na kumwabudu Mungu mmoja wa haki waliwaonyesha miujiza waliyopewa na Mola wao ya fimbo iliyogeuka nyoka mkubwa na mkono ulioingizwa kwenye nguo na kutoka ukiwa mweupe na wenye kung’ara. Hata hivyo jibu na radiamali ya kina firauni ambao waliyasikia maneno ya mantiki ya Nabii Musa na Nabii Harun (AS) na pia waliiona miujiza ya Mitume hao wa Allah, halikuwa jengine isipokuwa kukadhibisha na kuvurumiza tuhuma. Wao walidai kwamba kuabudu Mungu mmoja tu ni jambo ambalo halikuwahi kuwepo kwa wazee wao waliowatangulia; kwa sababu hiyo halikubaliki. Aidha wakasema miujiza nayo ni uchawi na mazingaombwe aliyojibunia Musa mwenyewe na kuyanasibisha na Mungu na kudai kuwa ni mambo yaliyo nje ya uwezo wa mwanadamu. Nabii Musa aliujibu ukadhibishaji huo wa kina Firauni kwa kusema: Kama maneno haya na mambo haya niliyoyafanya nimejibunia mimi mwenyewe na kumzulia Mwenyezi Mungu kwa kuyanasibisha na Yeye, Allah mwenyewe ni mjuzi zaidi na muelewa zaidi wa hilo kuliko nyinyi. Kwa hivyo itapasa anifedheheshe na kutoniacha nijitangaze kuwa ni Mtume niliyetumwa na Yeye, ambaye badala ya kuwaongoza watu kwenye uongofu niwapoteze kwa kuwaelekeza kwenye upotofu. Lakini chanzo cha ukadhibishaji wenu si kutojitosheleza hoja zangu ninazokupeni bali chanzo chake ni dhulma mnayotaka kuendelea kuifanya, ambayo kwa mawazo yenu itawezesha kudumu kwa utawala wenu. Kwa hivyo hamuyakubali maneno yangu; na hilo litakuwa sababu ya nyinyi kutofuzu duniani na akhera. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika kukubali mafundisho ya dini kipimo ni akili, mantiki, hoja na burhani; si maneno na mwenendo wa wazee waliotangulia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tuhuma na ukadhibishaji ndio mbinu muhimu zaidi ambayo imekuwa ikitumiwa na wapinzani wa Mitume na warekebishaji wa jamii katika zama zote za historia. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba kufuata uongofu uliolinganiwa na Mitume ndio unaomfanya mja apate saada na uokovu na kuwa na mwisho mwema. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 690 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah ajaalie bora ya amali zetu iwe ni ile ya mwisho wa uhai wetu; na siku bora kwetu iwe ni ile ya kukutana na Yeye. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/