Suratul Qas'as 38-42 (691)
Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 38-42 (Darsa ya 691)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 691, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 38 ambayo inasema:
وَقَالَ فِرْعَوْنُ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَهٍ غَيْرِي فَأَوْقِدْ لِي يَا هَامَانُ عَلَى الطِّينِ فَاجْعَل لِّي صَرْحًا لَّعَلِّي أَطَّلِعُ إِلَى إِلَهِ مُوسَى وَإِنِّي لَأَظُنُّهُ مِنَ الْكَاذِبِينَ
Na Firauni akasema: Enyi waheshimiwa! Sijui kama mnaye mungu asiye kuwa mimi. Ewe Haman! Niwashie moto unichomee udongo, unijengee mnara nipate kumchungulia Mungu wa Musa. Na hakika mimi namwona yeye ni katika waongo.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Firauni na wasaidizi wake waliukadhibisha na kuukataa wito wa haki wa Nabii Musa (AS) na kudai kwamba miujiza aliyowaonyesha pia ni uchawi na mazingaombwe tu. Aidha wakamwambia kuwa wazee wao waliowatangulia hawakuwa wakimjua wala kumwabudu huyo Mungu wake yeye Musa.
Aya tuliyosoma inaendeleza maudhui hiyo kwa kueleza kwamba moja ya hatua alizochukua Firauni ili kukabiliana na Nabii Musa na kwa lengo la kuzuia wito wake wa haki usiwe na taathira kwa watu ni kwamba aliamuru ujengwe mnara mrefu, ili yeye na wakubwa wa kaumu yake waukwee na kwenda juu wakaone kama huyo Mungu anayedai Musa kuwa yupo anaonekana kweli huko mbinguni au la? Kwa hakika Firauni alitoa amri hiyo kwa madhumuni ya kuwahadaa watu wa kawaida. Kwa kufanya hivyo, alitaka kuwaambia kwamba: mimi mwenyewe ni mungu, na simjui mungu mwengine wa kumwabudu nyinyi ghairi yangu mimi. Pamoja na hayo, ili msije mkadhani kwamba nina uadui binafsi na Musa na ninayakataa bure maneno yake ninaujenga mnara huu ili wakubwa wenu pia waufahamu ukweli wa ninayoyasema na wakajionee kwa macho yao wenyewe kuwa hakuna mungu yeyote huko mbinguni; na Musa ni mzushi na mwongo tu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kiburi, ghururi na hulka ya uistikbari humzuia mtu kuikubali haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuhadaa watu wa kawaida kwa kudai kujionyesha kuwa mtetezi wa kutaka kujua ukweli na hakika ya jambo ni miongoni mwa mbinu na hila ya Waistikbari ya kupotosha fikra za watu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba waistikbari wanajihisi wao ndiyo kitovu na mhimili mkuu wa kila kitu. Wanajiona kuwa wao ndio wamiliki na watawala wa dunia, na watu wengine hawana haki na wala hawastahiki chochote. Leo hii pia kuna madola yenye sifa za kifirauni ambayo yanajiona kuwa ndiyo yenye mamlaka ya mambo yote katika ulimwengu huu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 39 na 40 ambazo zinasema:
وَاسْتَكْبَرَ هُوَ وَجُنُودُهُ فِي الأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ إِلَيْنَا لا يُرْجَعُونَ
Na alipanda kiburi yeye na majeshi yake katika nchi bila ya haki, na wakadhania kuwa hawatarudishwa kwetu.
فَأَخَذْنَاهُ وَجُنُودَهُ فَنَبَذْنَاهُمْ فِي الْيَمِّ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الظَّالِمِينَ
Basi tukamshika yeye na majeshi yake, na tukawatupa baharini. Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa wenye kudhulumu.
Aya hizi wapenzi wasikilizaji, zinaashiria mwisho na hatima ya Firauni na watu wake katika dunia huu na kueleza kwamba: kwa upande mmoja, kusimama kwao kuipinga haki na kukanusha asili ya uumbwaji pamoja na maadi, yaani kufufuliwa; na kwa upande mwengine dhulma na uonveu waliokuwa wakiwafanyia watu viliwafanya wafikwe na adhabu papa hapa duniani kwa kugharikishwa kwenye maji ya Mto Nile. Naam, hivyo ndivyo inavyokuwa! Ule mto ambao ulikuwa ndio chanzo cha mapato ya uhai wao, na chemchemi ya nguvu na utajiri wao uligeuka kuwa ndio kaburi lao lililowazamisha na kuwameza mafirauni wote.
Aya hizi zinataja sifa mbili za utawala wa kifirauni zilizosababisha kuporomoka na kuangamia kwake: Moja, ilikuwa ni hulka ya kutakabari na kujikweza kwa kujiona bora na wa juu zaidi kuliko watu wengine; na nyengine ilikuwa ni dhulma yao kwa wanyonge na walio chini yao kwa kuwanyima haki zao za kimaumbile na za msingi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tusisimame kukabiliana na haki na ukweli, kwani mwishowe tutaangamia tu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kutoamini maadi, hisabu na malipo ya akhera humfanya mtu awe na hulka ya uistikbari. Na hiki ndicho chanzo cha mikengeuko, dhulma na jinai zifanywazo na madhalimu na waistikbari. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu si kwa ajili ya akhera tu, bali hata hapa duniani, Allah SW huwaonjesha adhabu ya kudhalilisha madhalimu na waistikbari. Vilevile tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa madhalimu wamekuwa na hatima moja katika zama zote za historia.
Darsa ya 691 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 41 na 42 ambazo zinasema:
وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ لا يُنصَرُونَ
Na tuliwafanya ni waongozi waitao kwenye Moto. Na Siku ya Kiyama hawatanusuriwa
وَأَتْبَعْنَاهُمْ فِي هَذِهِ الدُّنْيَا لَعْنَةً وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ هُم مِّنَ الْمَقْبُوحِينَ
Na tukawafuatishia laana katika dunia hii, na Siku ya Kiyama watakuwa miongoni mwa wanao chusha.
Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia ambazo ziliashiria mwisho wa kina Firauni hapa duniani na kueleza kwamba Siku ya Kiyama, ambapo waovu na wenye madhambi watapelekwa motoni, kina Firauni watakuwa wamewatangulia watu hao; na kama ambavyo hapa duniani walikuwa viongozi wa wafanya madhambi, huko akhera pia watakuwa vivyo hivyo.
Hapa duniani walikuwa daima wakilaaniwa na kuapizwa na madhulumu na waliokuwa chini ya mamlaka yao katika zama zao; na katika zama zote za historia pia wanaapizwa na kulaaniwa na waumini. Mwenendo huo mchafu na muovu utadhihirika Siku ya Kiyama na kuwafanya waonekane na nyuso chafu, mbaya na za kukirihisha. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wale ambao leo hapa duniani wanajiona kwa sababu ya suhula na nguvu za madaraka waliyonayo, Siku ya Kiyama hawatokuwa na wenza wala wasaidizi, wala nguvu za kuwaokoa wao wenyewe seuze kuwaokoa na kuwanusuru wengine. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuwalaani na kuwaapiza madhalimu na kutoa sha'ar dhidi yao ni jambo ambalo Allah SW amelijuzisha. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba wale ambao katika maisha ya duniani walikuwa wakifuata vigezo vya watu waliokufuru na waliopotoka, Siku ya Kiyama pia watafufuliwa pamoja na makafiri na wapotofu hao na kuwafuata katika safari yao ya motoni. Vilevile tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa amali chafu na mbaya za mtu hapa duniani zitamfanya aonekane na sura chafu na mbaya huko akhera. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atuongoze njia iliyonyooka. Njia ya wale aliowaneemesha juu yao. Si ya wale walioghadhibikiwa, wala ya wale waliopotea. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/