Jan 01, 2017 11:38 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 43-46 (Darsa ya 692)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 692, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 43 ambayo inasema:

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ مِن بَعْدِ مَا أَهْلَكْنَا الْقُرُونَ الأُولَى بَصَائِرَ لِلنَّاسِ وَهُدًى وَرَحْمَةً لَّعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ

Na hakika bila ya shaka tulimpa Musa Kitabu baada ya kwisha ziangamiza kaumu za mwanzo, ili kiwafumbue macho watu, na kiwe uwongofu, na rehema, ili wapate kukumbuka.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa hatima na mwisho wa Firauni na jeshi lake ulikuwa ni kugharikishwa katika Mto Nile. Amma aya tuliyosoma inasema: baada ya kuwaokoa Bani Israil na mateso na madhila ya kunyongeshwa na Firauni, tulimteremshia Musa Taurati kwa ajili ya kuwaongoza wao na kuinua kiwango chao cha fikra, basira na uono ili waweze kunufaika na mafundisho yake na kuwa miongoni mwa waja wenye kupata rehma na fadhila zetu maalumu. Tab’an kama wao wataikadhibisha Taurati na kusimama kuipinga haki, nao pia wataangamizwa kama ilivyokuwa kwa kaumu zilizopita zilizofikwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu hapa duniani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kudhihiri kwa Mitume na kuteremshwa vitabu vya mbinguni kumetokana na rehma za Allah na ni miongoni mwa neema kubwa za Mola ili mwanadamu aweze kufikia saada kwa njia ya uono mpana, basira na uongofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Allah SW ameweka kaida na utaratibu maalumu na thabiti katika zama zote za historia. Umma au kaumu yoyote ya watu itakayokengeuka njia ya haki mwishowe huangamia.

Zifuatazo sasa ni aya za 44 na 45 ambazo zinasema:

وَمَا كُنتَ بِجَانِبِ الْغَرْبِيِّ إِذْ قَضَيْنَا إِلَى مُوسَى الأَمْرَ وَمَا كُنتَ مِنَ الشَّاهِدِينَ

Wala wewe hukuwa upande wa magharibi tulipo mpa Musa amri, wala hukuwa miongoni mwa walio shuhudia.

وَلَكِنَّا أَنشَأْنَا قُرُونًا فَتَطَاوَلَ عَلَيْهِمُ الْعُمُرُ وَمَا كُنتَ ثَاوِيًا فِي أَهْلِ مَدْيَنَ تَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا وَلَكِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ

Lakini Sisi tuliziumba kaumu, na ukawa mrefu umri juu yao. Wala hukuwa mkaazi wa watu wa Madyana ukiwasomea Aya zetu. Lakini ni Sisi tulio kuwa tukiwatuma Mitume.

Aya hizi tulizosoma zinatilia mkazo nukta hii, kwamba yale yaliyosimuliwa ndani ya Qur’ani kuhusu kaumu na Mitume waliotangulia ni hoja na ushahidi wa kuthibitisha ukweli wa Utume wa Nabii Muhammad SAW; kwa sababu mtukufu huyo hakuwepo katika yoyote kati ya zama hizo, lakini anayaeleza kwa ufafanuzi matukio yaliyojiri katika zama za kaumu hizo na za Mitume hao waliopita. Kwa mfano matukio yanayohusiana na kupewa Utume Nabii Musa katika Mlima Turi, ambayo yalijiri karne kadhaa kabla ya kuzaliwa Bwana Mtume, yameelezwa ndani ya Qur’ani kwa ufafanuzi, na hata baadhi ya wakati kwa undani kabisa. Aidha ndani ya Qur’ani tukufu zimetajwa habari na matukio yaliyojiri katika mji wa Madyan, ambako Musa (AS) alielekea alipokimbia kutoka Misri; na baada ya kujuana na Nabii Shuaib akamuoa binti yake. Aidha imeashiriwa pia habari ya miaka 10 aliyokaa Nabii Musa huko Madyan na kisha safari yake ya kurudi zake Misri. Namna hivyo hivyo, Qur’ani imetaja visa vya kaumu nyingi zilizopita, ambazo historia zao zinarejea kwenye vipindi vya maelfu ya miaka nyuma. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba habari za kihistoria zilizotajwa ndani ya Qur’ani, kiujumla ni habari za ghaibu, ambazo watu wa zama za Bwana Mtume SAW huko Makka hawakuwa na taarifa nazo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa moja ya hoja za kuthibitisha kuwa Qur’ani ni muujiza na Nabii Muhammad SAW ni Mtume wa haki, ni habari za ghaibu zinazosimuliwa na Qur’ani ambazo ni sehemu maalumu ya aya za kitabu hicho cha mbinguni.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 46 ambayo inasema:

وَمَا كُنتَ بِجَانِبِ الطُّورِ إِذْ نَادَيْنَا وَلَكِن رَّحْمَةً مِّن رَّبِّكَ لِتُنذِرَ قَوْمًا مَّا أَتَاهُم مِّن نَّذِيرٍ مِّن قَبْلِكَ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ

Wala hukuwa kando ya mlima tulipo nadi. Lakini ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi ili uwaonye watu wasio pata kufikiwa na mwonyaji kabla yako, huenda wakakumbuka.

Aya hii inaendelea na maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu kuwa miongoni mwa mambo ya ghaibu habari zilizosimuliwa na Qur’ani kuhusu Nabii Musa (AS) na kusisitiza tena juu ya suala hilo kwa kumhutubu Bwana Mtume SAW kwa kumwambia: yale tuliyokuteremshia wewe ni rehma za Mola wako, ili kwa kubainisha yale yaliyojiri katika kaumu ya Bani Israil uwape indhari watu na kuwatahadharisha na hatima ya matendo yao.

Ni wazi kwamba watu wa zama za Bwana Mtume Muhammad SAW huko Makka hawakuwahi kushuhudia Mtume yeyote hata kuweza kwa njia hiyo kuelewa yaliyojiri katika zama za kaumu zilizotangulia; kama ambavyo katika kipindi cha karne mbili hadi tatu kabla ya kuja Bwana Mtume SAW hakuwa amedhihiri Mtume mwengine yeyote wa kuja kubainisha habari hizo. Tab’an baadhi ya Mitume kama Hud, Saleh na Shuaib (AS) walibaathiwa katika eneo la Bara Arabu na ardhi za kandokando yake, lakini muda mrefu ulikuwa umepita tangu kuondoka kwao kiasi kwamba athari na kumbukumbu zao zilikuwa zimeshafutika na kutoweka.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba moja ya malengo ya kubaathiwa Mitume na kuteremshwa vitabu ni kuwapa maonyo na indhari watu ili wasije wakapatwa na mghafala na kuisahau Akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa akili na fitra, yaani maumbile asili ya mwanadamu humuonyesha kiumbe huyo hakika na ukweli wa mambo mengi lakini kuna mambo mengi pia yanayomfanya aghafilike na wito huo wa batini na wa ndani ya nafsi yake. Kwa hivyo Mitume huwa wanawaonya na kuwakumbusha watu kwa matumaini kuwa asaa watakumbuka na kuzinduka na kurejea kwenye njia ya haki. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 692 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/