Suratul Qas'as 47-50 (693)
Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 47-50 (Darsa ya 693)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 693, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 47 na 48 ambazo zinasema:
وَلَوْلا أَن تُصِيبَهُم مُّصِيبَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ فَيَقُولُوا رَبَّنَا لَوْلا أَرْسَلْتَ إِلَيْنَا رَسُولا فَنَتَّبِعَ آيَاتِكَ وَنَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ
Na usije ukawasibu msiba kwa iliyo yatanguliza mikono yao, wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Mbona hukututumia Mtume nasi, tukafuata Ishara zako, na tukawa miongoni mwa Waumini?
فَلَمَّا جَاءَهُمُ الْحَقُّ مِنْ عِندِنَا قَالُوا لَوْلا أُوتِيَ مِثْلَ مَا أُوتِيَ مُوسَى أَوَلَمْ يَكْفُرُوا بِمَا أُوتِيَ مُوسَى مِن قَبْلُ قَالُوا سِحْرَانِ تَظَاهَرَا وَقَالُوا إِنَّا بِكُلٍّ كَافِرُونَ
Ilipo wajia Haki kutoka kwetu walisema: Mbona hakupewa kama aliyo pewa Musa? Je! Kwani wao hawakuyakataa aliyo pewa Musa zamani? Walisema: (Qur’ani na Taurati) ni wachawi wawili wanaosaidiana. Na wakasema: Hakika sisi tunawakataa wote.
Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinaashiria moja ya kaida na utaratibu usiobadilika wa Allah katika zama zote za historia na kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu amewapa wanadamu akili; na kwa kutumia akili zao, wanadamu wana uwezo wa kupambanua baina ya zuri na baya katika mambo mengi sana; na kuwa au kutokuwa sahihi mambo mengi ya itikadi, mila na desturi. Lakini pamoja na hayo utaratibu aliouweka Allah ni kwamba huwa hawaadhibu watu kutokana na matendo yao kabla hajatuma Mtume wake kwa kaumu ya watu hao; kwa sababu hilo litawafanya watu wafanya maovu wawe na udhuru na kisingizio cha kutoa kwamba laiti kama tungeletewa Mtume wa kutuongoza kuufuata uongofu, tungeongoka na kuwa miongoni mwa wenye kufuzu. Kisha aya zinaendelea kwa kueleza kwamba: Lakini hata baada ya kupelekewa Mitume pia baadhi ya watu wametafuta kisingizio kingine kwa kusema: Kwa nini Muhammad haonyeshi miujiza kama ile aliyoionyesha Musa? Mbona fimbo yake yeye haigeuki nyoka; au mbona bahari haipasuki ili maadui zake wagharikishwe na kuangamizwa ndani yake? Qur'ani tukufu imevijibu visingizio hivyo kwa kusema: Kwani watu wote waliokuwepo katika zama za Nabii Musa na wakaiona miujiza hiyo walimwamini Mtume huyo hata mseme na kudhani kwamba ikiwa Nabii Muhammad SAW naye pia atafanya kama aliyofanya Musa hakutokuwa na kisingizio tena kwa mtu cha kutoamini? Ukweli ni kwamba watu wanaotafuta visingizio katika kila zama wamekuwa wakiita miujiza ya Mwenyezi Mungu uchawi na mazingaombwe na hawakuwa tayari kuiamini. Wapinzani wa Nabii Musa (AS) walimwita Mtume huyo mchawi na pia wanaompinga Nabii Muhammad SAW wanafanya vivyo hivyo. Katika zama za Nabii Musa, wapinzani wake walisema kugeuka fimbo yake nyoka ni uchawi, kama ambavyo wapinzani wa Nabii Muhammad SAW wanasema aya za Qur'ani pia ni uchawi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mwenyezi Mungu anawatuma Mitume ili kuondoa dhima kwa watu na ili pasibaki kisingizio chochote tena cha kutoa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mengi ya matatizo na masaibu yanayotupata yanatokana na matendo yetu sisi wenyewe. Athari za matendo yetu mema na mabaya hudhihirika papa hapa duniani. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba madai ya uchawi na mazingaombwe ndizo tuhuma zilizokuwa zikitolewa sana na makafiri dhidi ya Mitume wa Allah. Wakanushaji wa haki wakidai kwamba Taurati na Qur'ani ni vitabu viwili vya uchawi vinavyotiana nguvu kila kimoja kwa kingine.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 49 na 50 ambazo zinasema:
قُلْ فَأْتُوا بِكِتَابٍ مِّنْ عِندِ اللَّهِ هُوَ أَهْدَى مِنْهُمَا أَتَّبِعْهُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ
Sema: Basi leteni Kitabu kinacho toka kwa Mwenyezi Mungu chenye mwongozo (wa uongofu) zaidi kuliko hivi viwili nikifuate, kama nyinyi mnasema kweli.
فَإِن لَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكَ فَاعْلَمْ أَنَّمَا يَتَّبِعُونَ أَهْوَاءهُمْ وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّنِ اتَّبَعَ هَوَاهُ بِغَيْرِ هُدًى مِّنَ اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ لا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ
Na ikiwa hawakuitikii, basi jua kuwa wanafuata hawaa zao tu. Na nani aliye potea zaidi kumshinda anaye fuata hawaa yake bila ya uwongofu utokao kwa Mwenyezi Mungu? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhalimu.
Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kuhusu makafiri waliokuwa wakiwatuhumu Mitume wa Allah kuwa ni wachawi na kumhutubu Bwana Mtume SAW kwa kumwambia: Waambie hao wapinzani kwamba: nyinyi mnaoikanusha Taurati na Qur'ani kuwa si vitabu vya Mwenyezi Mungu leteni kitabu kingine chenye uongofu uliokamilika zaidi ya vitabu hivi; na mkifanya hivyo kuweni na uhakika kwamba mimi nitakifuata kitabu hicho. Kwa maneno mengine, Bwana Mtume anasema: lengo ni kuufikia uongofu wa Allah; kwa hivyo kama na nyinyi pia mumetumwa na kubaathiwa na Yeye Mola na mumekuja na kitabu, mimi nitakikubali na kukifuata. Bila ya shaka ni wazi kwamba si wao wana kitabu kama hicho ambacho wamekuja nacho kutoka kwa Mwenyezi Mungu na si eti kuna kitabu kingine kitapatikana kilichokamilika zaidi ya Qur'ani. Wanachotaka wao ni kufuata hawaa na matamanio ya nafsi zao; na kwa kuwa vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo Mitume vinapinga ufuataji huo wa matamanio yao ya nafsi wanavitilia shaka na kuvikadhibisha. Ukweli ni kwamba kuabudu matamanio ya nafsi humzuia mtu kuikubali haki na kumuelekeza mtu kwenye lindi la maangamizi ya upotofu; mpaka kufikia hadi watu wanaoabudu matamanio ya nafsi zao kujipa haki ya kuwaambia Mitume wa Allah kuwa watu waliopotea, na wao kujiona watu waliotaalamika na kuongoka. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ili kuthibitisha ukweli wa haki, baadhi ya wakati inatakiwa kutumia mbinu ya utoaji changamoto ya kutaka kupambana kwa hoja, mijadala na midahalo; kama ambavyo moja ya hoja za kuthibitisha ukweli wa Utume wa Nabii Muhammad SAW na Qur'ani tukufu ni huo utoaji changamoto ya kukabiliana na wapinzani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mwanadamu anatakiwa awe mfuataji haki. Hata kama mpinzani wake atakuwa ndiye aliyesema neno la haki awe tayari kulikubali. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba uongofu wa kweli ni ule unaotokana na elimu na hekima isiyo na ukomo ya Allah SW; si ule unaotokana na elimu pungufu ya mwanadamu na yenye kuchanganyika na utashi wa hawaa na matamanio ya nafsi. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 693 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuoneshe haki na atuwafikishe kuifuata, na atuoneshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/