Suratul Qas'as 56-58 (695)
Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 56-58 (Darsa ya 695)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 695, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 56 ambayo inasema:
إِنَّكَ لا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَكِنَّ اللَّهَ يَهْدِي مَن يَشَاء وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ
Kwa hakika wewe humwongoi umpendaye, lakini Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye. Na Yeye ndiye anayewajua zaidi waongokao.
Katika darsa zilizopita tulisema kuwa washirikina wengi wa Makka hawakuwa tayari kusilimu na kuacha imani yao ya kuabudu masanamu. Lakini kinyume chake, baadhi ya Wakristo, yaani Ahlul Kitab waliposikia aya za Qur’ani walisilimu na kumwamini Bwana Mtume SAW na kutangaza kwamba huyu ndiye mtu ambaye Isa Masih alitoa bishara ya kuja kwake.
Aya tuliyosoma inaendeleza maudhui hiyo kwa kubainisha kanuni moja ya msingi; nayo ni kwamba jukumu la kila Mtume ni kufanya tablighi na kufikisha aya za Mwenyezi Mungu na kuwalingania watu tauhidi; lakini hakuna Mtume mwenye dhima juu ya kukubali au kutokubali watu kuuamini wito wake. Yeye ana wajibu wa kuwaonyesha watu njia ya Mwenyezi Mungu, lakini kwamba nani miongoni mwao ataifuata njia hiyo na nani ataikengeuka hilo haliko kwenye mamlaka yake. Mtume huwa anapenda na anatamani watu wote waiamini haki na kumwabudu Mola mmoja tu wa haki. Lakini hana haki ya kuwataka walifanye hilo kwa lazima. Kwani hata kama atawataka wafanye hivyo kwa lazima hatoweza kuzilazimisha nyoyo zao pia ziamini na kuifuata njia ya haki. Ni Allah SW pekee, ndiye ambaye nyoyo za waja wake wote ziko kwenye mamlaka yake; na kwa hivyo kila atakayemwona ana kiu ya haki na analaiki kuwa muumini humpa taufiki ya kusilimu na kuifuata njia yake ya haki. Kwa hivyo si hasha jamaa wa Mtume mwenyewe akakataa kumwamini na akaamua kung’ang’ania imani ya shirki; na si hasha Ahlul Kitab, wakaamua kuachana na taasubi juu ya dini yao, wakasilimu na kumwamini Bwana Mtume SAW. Aya ya 43 ya Suratu Yunus ambayo tuliisoma katika darsa zetu za huko nyuma inasema: Je, wewe utawaongoa vipofu ingawa hawaoni?
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba wajibu wa Mitume ni kuufikisha wito wa Allah kwa watu; si kuwalazimisha. Kuukubali au kutoukubali watu hakuko kwenye mamlaka yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa irada na kutaka kwa Allah kumesimama juu ya msingi wa elimu na hekima. Kulingana na hekima yake Mola humpa taufiki ya kuufuata uongofu kila yule anayemwona ni mstahiki wa hilo.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 57 ambayo inasema:
وَقَالُوا إِن نَّتَّبِعِ الْهُدَى مَعَكَ نُتَخَطَّفْ مِنْ أَرْضِنَا أَوَلَمْ نُمَكِّن لَّهُمْ حَرَمًا آمِنًا يُجْبَى إِلَيْهِ ثَمَرَاتُ كُلِّ شَيْءٍ رِزْقًا مِن لَّدُنَّا وَلَكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لا يَعْلَمُونَ
Na wakasema: Tukiufuata uwongofu huu pamoja nawe tutanyakuliwa kutoka nchi yetu. Je! Kwani Sisi hatukuwaweka imara katika pahala patakatifu, penye amani, ambapo huletewa matunda ya kila aina kuwa ni riziki itokayo kwetu? Lakini wengi wao hawajui.
Aya hii inazungumzia watu waliokuwa wakiishi katika mji wa Makka, ambao walikuwa wakijua ukweli wa Qur’ani na Utume wa Nabii Muhammad SAW; lakini hawakuwa tayari kusilimu na kuikubali haki kwa sababu ya kulinda maslahi yao ya binafsi na ya koo na familia zao. Kisingizio walichokuwa wakitoa watu hao ni kwamba wakubwa wa Makka, ambao wana nguvu, utajiri na kila suhula watatutoa majumbani mwetu na katika mji wetu huu; na hivyo tutabaki hohe hahe katika hali ya kutangatanga. Qur’ani tukufu ikawajibu watu hao kwa kuwauliza:”Ni nani mwenye nguvu zaidi? Mwenyezi Mungu au viongozi wa Makureishi? Mwenyezi Mungu ambaye amekuteremshieni nyinyi anuai za neema na akaufanya mji wenu huu wa Makka uwe katika amani, atakuwa hana uwezo wa kukulindeni na kukuhifadhini nyinyi na shari ya washirikina?”
Japokuwa katika siku za mwanzoni, Waislamu walikuwa wakiteswa na kuudhiwa na washirikina, lakini kwa irada ya Allah walianza kupata nguvu siku baada ya siku mpaka hatimaye wakaweza kuikomboa Makka ikawa chini ya mamlaka yao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba watu wengi wanaokataa kuiamini na kuifuata haki hufanya hivyo kwa sababu ya kutaka kupata starehe na raha za kimaada na manufaa ya binafsi; na si eti kwa sababu ya kutoifahamu haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa amani ina kipaumbele cha kwanza kuliko jambo lolote lile. Ni kwa kuwepo amani na utulivu wa kijamii ndio unapatikana ustawi wa kiuchumi na kuleta neema za kuwezesha watu kujikimu maisha yao kwa kazi na ajira.
Darsa ya 695 ya Qur’ani inahatimishwa na aya ya 58 ambayo inasema:
وَكَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَرْيَةٍ بَطِرَتْ مَعِيشَتَهَا فَتِلْكَ مَسَاكِنُهُمْ لَمْ تُسْكَن مِّن بَعْدِهِمْ إِلاَّ قَلِيلا وَكُنَّا نَحْنُ الْوَارِثِينَ
Na miji mingapi iliyo jifakharisha tumeiangamiza! Na hayo maskani yao hayakukaliwa tena baada yao, ila kwa uchache tu. Na Sisi ndio tumekuwa warithi.
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kwa kuwahutubu na kuwaambia washirikina wa Makka kwamba: nyinyi mumekataa kusilimu na kuiamini haki kwa sababu ya kulinda mali zenu na kuchelea kupoteza raha na starehe zenu; hivi mumesahau kuwa baadhi ya kaumu zilizopita ambazo ziliasi kutokana na kuleweshwa na raha na utajiri mkubwa wa mali walizokuwa nazo ziliangamizwa? Tujaalie na nyinyi pia mpate raha na uneemevu huo; kuna uhakika gani kwamba na nyinyi pia hamtofikwa na adhabu na hatima kama yao?
Ardhi za kaumu ya Aad na Thamud zilikuwepo kwenye njia ilipokuwa ikipita misafara ya biashara ya waarabu wanaotoka Makka kuelekea Sham; na wao walikuwa wakiyaona kwa macho yao maskani na nyumba za watu wa kaumu hizo zilizobakia magofu lakini hawakuwa wakipata ibra na mafunzo kutokana na yaliyozisibu kaumu hizo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba baadhi ya wakati raha na mali hazimfikishi mtu kwenye saada. Si hasha vitu hivyo vikawa sababu ya mtu kuingiwa na ghururi, akawa asi na mwishowe kuangamia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mabaki ya staarabu na tamaduni zilizopita yana mafunzo kwa watu. Kwa hivyo ni jambo muhimu na lenye udharura kuzitunza na kuzihifadhi athari za kale za kaumu zilizopita ili zije kuvipa ibra, mafunzo na mazingatio vizazi vijavyo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba dunia hii ni ya kupita na yenye kumalizika. Tusihadaiwe na dhahiri ya leo tu ya wenye maisha ya raha na starehe, tujue kwamba wao pia wataondoka na kuziacha nyuma mali zao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 695 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah ajaalie amani na usalama irejee katika nchi na ardhi zote za Waislamu na atulinde na kila shari za maadui wa dini yake tukufu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/