Jan 03, 2017 10:33 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 64-69 (Darsa ya 697)

 

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 697, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 64 ambayo inasema:

وَقِيلَ ادْعُوا شُرَكَاءَكُمْ فَدَعَوْهُمْ فَلَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُمْ وَرَأَوُا الْعَذَابَ لَوْ أَنَّهُمْ كَانُوا يَهْتَدُونَ

Na itasemwa: Waiteni hao miungu wa kishirikina wenu! Basi watawaita, lakini hawatawaitikia, na wataiona adhabu; (watatamani) laiti wangeli kuwa wameongoka!

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Siku ya Kiyama viongozi wa shirki na ukafiri watachukizwa na wafuasi wao na hawatokuwa tayari kukubali mas-ulia ya kuwapoteza wafuasi wao hao. Aya hii tuliyosoma inasema: Ili washirikina waweze kujionea wenyewe udhaifu wa maabudu na waola wao bandia, Siku ya Kiyama wataambiwa waombeni basi waje wakusaidieni na kukuokoeni wale mliokuwa mkiwafikiria kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Lakini ni wazi kwamba hawatosikia kutoka kwao jawabu lolote wala kupatiwa msaada wowote. Ni wakati huo ndipo watatamani kuwa laiti wangeukubali wito wa uongofu wa Allah wasingebaki peke yao na bila ya kuwa na kimbilio la kuwanusuru na adhabu ya moto. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kila tutakachokikumbatia na kukifuata hapa duniani ghairi ya Allah kitatufanya tukose auni na msaada wake Mola Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Siku ya Kiyama ni siku ya majuto na masikitiko kwa waliokhitari njia ya madhambi na upotofu. Lakini majuto hayo hayatowafalia kitu.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 65, 66 na 67 ambazo zinasema:

وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ فَيَقُولُ مَاذَا أَجَبْتُمُ الْمُرْسَلِينَ

Na siku atapo waita na akasema: Mliwajibu nini Mitume?

فَعَمِيَتْ عَلَيْهِمُ الأَنبَاء يَوْمَئِذٍ فَهُمْ لا يَتَسَاءَلُونَ

Basi zitawapotea khabari siku hiyo, nao hawataulizana.

فَأَمَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَعَسَى أَن يَكُونَ مِنَ الْمُفْلِحِينَ

Ama mwenye kutubu na akaamini na akatenda mema, asaa akawa miongoni mwa wenye kufanikiwa.

Aya hizi zinaendelea na maudhui ya kuhudhurishwa washirikina mbele ya mahakama ya uadilifu ya Allah Siku ya Kiyama na kueleza kwamba, siku hiyo wataulizwa, mliwajibu nini Mitume baada ya wito waliokufikishieni? Mitume walikulinganieni kumwabudu Mungu pekee wa haki na kufanya mema na ya kheri; nyinyi mliwajibu nini? Bila ya shaka washirikina hawatokuwa na jawabu la kutoa kwa suali hilo. Kwani kama watasema sisi tuliukubali wito wa Mitume na kuwaamini, huo ni uongo mkubwa; na uongo hausaidii kitu Siku ya Kiyama. Na kama watasema tuliwakadhibisha, tukawaita wachawi na wendawazimu na tukasimama kukabiliana nao na kuwapiga vita, watakuwa wamekiri kosa lao kwa ndimi zao wenyewe na kujikatia wenyewe hukumu ya adhabu yao. Kwa kweli lolote watakalosema litakuwa ni kwa madhara yao. Lakini hawatokuwa na njia yoyote ya kulikwepa suali hilo wala kisingizio cha kutolea jibu lake. Tatizo jengine litakalowakabili watu hao ni kwamba hawatoweza kuzungumza na wenzao na kutaka ushauri wao au kuulizana wao kwa wao ili kupata njia ya kulijibu suali hilo. Kisha aya zinaendelea kwa kusema: Leo wao wako katika hali ya kutingwa na kutangatanga na wamekwama hawana la kufanya, hali ya kuwa duniani hatukuwafungia njia ya kuweza wakati wowote ule kutubia na kuwaamini Mitume wa Mwenyezi Mungu na kufanya mambo mema. Kwani kama wangefanya hivyo wangekuwa watu waliofuzu na kuokoka; na wala leo adhabu isingewafika. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika mahakama ya Siku ya Kiyama washirikina hawatokuwa na jawabu la kutoa kwa sababu ya kumshirikisha kwao Mwenyezi Mungu na kuwakadhibisha Mitume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Siku ya Kiyama njia zote za kupokea habari zitafungwa; na watu hawatoweza kushauriana wala kuulizana na wenzao wenye fikra moja ili kupata jibu la kutoa mbele ya mahakama ya uadilifu ya Allah SW. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba katika Uislamu mlango wa toba haujafungwa hata kwa washirikina na waliokubuhu madhambi. Utaratibu wa Uislamu ni kwamba umeufungua na kuuweka wazi muda wote mlango wa toba kwa makafiri na wafanya madhambi ili hata kama watakuwa katika hali yoyote ya uovu na upotovu waweze kutubia na kurejea kwenye njia ya haki. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kufuzu na kuokoka kwa mtu kunapatikana kwa kuyaacha maovu na kutenda mema.

Darsa ya 697 ya Qur’ani inahatimishwa na aya ya 68 na 69 ambazo zinasema:

وَرَبُّكَ يَخْلُقُ مَا يَشَاء وَيَخْتَارُ مَا كَانَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ سُبْحَانَ اللَّهِ وَتَعَالَى عَمَّا يُشْرِكُونَ

Na Mola wako Mlezi huumba na huteuwa atakavyo. (Viumbe) hawana khiari. Mwenyezi Mungu ametukuka na ametakasika na hao wanao washirikisha Naye.

وَرَبُّكَ يَعْلَمُ مَا تُكِنُّ صُدُورُهُمْ وَمَا يُعْلِنُونَ

Na Mola wako Mlezi anayajua yaliyo ficha vifua vyao, na wanayo yatangaza.

Katika sehemu hii ya mwisho ya aya hizi, Qur’ani tukufu inatoa jawabu kwa washirikina waliokuwa wakimfanyia Allah washirika wenye nafasi katika uumbaji na uwekaji sharia kwa kusema: Mwenyezi Mungu ni Yeye mwenyewe ndiye anayeamua aumbe nini na akiumbe vipi, nani amchague kuwa Mtume wake na sharia gani awawekee watu. Hakuna mtu yeyote wa kumlazimisha kufanya jambo au kuzuia irada ya Mola na lile analolitaka liwe.

Kwa irada ya Allah SW wanadamu wameumbwa wakiwa na mamlaka ya hiyari ya kuchagua; lakini mamlaka hayo hayako juu ya mamlaka ya lile analoliamua Allah; kwa sababu wao wameumbwa na Yeye Mola na wako chini ya irada yake. Katika masuala ya uumbaji ni wazi kuwa hakuna mwanadamu yeyote ambaye amekuwa au ana nafasi yoyote katika uumbwaji wake yeye mwenyewe au wa viumbe wengine. Kwa upande wa uwekaji sharia pia, ikiwa Mwenyezi Mungu amewataka wanadamu watende au wajiepushe kufanya jambo fulani, wao waja hawana hiyari na mamlaka ya kujipangia na kujiwekea sharia kinyume na alivyopanga Allah SW. Ni kama inavyoeleza aya ya 36 ya Suratul Ahzab kuwa, wakati Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapotoa hukumu ya jambo, waumini wanaume na wanawake huwa hawana hiyari na mamlaka ya kujiamulia kufanya kinyume na hukumu hiyo.

Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba uumbaji wa ulimwengu na uendeshaji mambo yake, na vilevile uwekaji sharia na uteuaji wa Mitume, yote hayo yako kwenye mamlaka ya Allah SW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mtu anayepinga sharia za Mwenyezi Mungu na badala yake akakubali sharia zinazotungwa na mwanadamu huwa kwa hakika amemfanya mwanadamu huyo mshirika wa Mwenyezi Mungu katika upangaji kanuni na sharia.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 697 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepueshe na kila ya aina shirki; kubwa na ndogo, ya dhahiri na iliyojificha. Wassalamu Alaykumu Warahmatullahi Wabarakaatuh…/