Jan 03, 2017 10:39 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 76-78 (Darsa ya 699)

 

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 699, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 76 ambayo inasema:

إِنَّ قَارُونَ كَانَ مِن قَوْمِ مُوسَى فَبَغَى عَلَيْهِمْ وَآتَيْنَاهُ مِنَ الْكُنُوزِ مَا إِنَّ مَفَاتِحَهُ لَتَنُوأُ بِالْعُصْبَةِ أُولِي الْقُوَّةِ إِذْ قَالَ لَهُ قَوْمُهُ لا تَفْرَحْ إِنَّ اللَّهَ لا يُحِبُّ الْفَرِحِينَ

Hakika Qaruni alikuwa katika kaumu ya Musa, lakini aliwafanyia dhulma. Na tulimpa khazina ambazo funguo zake zinawaelemea watu wenye nguvu kuzichukua. Walipo mwambia watu wake: Usijigambe! Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanao jigamba.

Katika aya kadhaa kuanzia mwanzoni mwa sura hii, tulizungumzia kisa cha Nabii Musa (AS) na Firauni. Lakini aya hii tuliyosoma na kadhaa zitakazofuatia zitasimulia habari za Qarun, ambaye alikuwa mmoja wa matajiri wakubwa katika zama za Mtume huyo wa Allah. Kama ilivyoelezwa katika vitabu vya historia, Qarun alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa Nabii Musa, na mwanzo wake alimwamini Mtume huyo. Lakini mali na utajiri vilimtia kiburi na ghururi mpaka akafikia hadi ya kuasi na kusimama kukabiliana na Musa (AS).

Firauni, wapenzi wasikilizaji ni dhihirisho la mtu mwenye nguvu na madaraka ya kitaghuti anayewadhulumu na kuwaonea watu na kusimama dhidi ya haki; Qarun ni dhihirisho na nembo ya matajiri wanaojitukuza, wakajikweza na kujigamba mbele za watu na kuasi kutekeleza mafundisho ya haki. Na Samiriy, yeye ni dhihirisho la wasanii ambao wanawapoteza watu kwa kuwatoa kwenye njia ya haki na kuwaelekeza kwenye shirki na upotovu.

Aya inaendelea kwa kueleza kwamba, chimbuko la uasi wa Qarun ni ghururi, kiburi na kujisahau, ambapo kadiri mali na utajiri wake ulivyoongezeka ndivyo alivyozidi kughafilika na Allah pamoja na waja wa Allah na kufikiria zaidi jinsi ya kujilimbikizia mali kwa kujikusanyia dhahabu na fedha pamoja na vito vingine vya thamani. Hali ya kuwa mali na utajiri pamoja na mzunguko wa gurudumu la uchumi vinapasa vitumiwe kwa ajili ya kuwatumikia watu; si kuwanufaisha matajiri wachache tu wanaojilimbikizia mali hizo na kuwalangua wanyonge na wasio na kitu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba si kitu kibaya kuwa na utajiri na kufanya juhudi za kujiongezea mali na utajiri; kinachokemewa na chenye kuchukiza ni kuwa na ghururi kwa sababu ya mali na utajiri na kuwa asi mbele ya Mwenyezi Mungu, Mtume wake pamoja na waja wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kulewa hakusababishwi na kunywa pombe tu; baadhi ya wakati kupata fedha na utajiri huwalewesha na kuwalevya watu mpaka wakaghafilika na kusahau kila kitu. Watu wa aina hiyo huleweshwa na uwezo, mali na utajiri walionao wakakanyaga na kuponda haki za wenzao.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 77 ambayo inasema:

وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّهُ الدَّارَ الآخِرَةَ وَلا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّهُ إِلَيْكَ وَلا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الأَرْضِ إِنَّ اللَّهَ لا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ

Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.

Katika aya iliyotangulia ilielezwa kuwa baadhi ya wafuasi wa Nabii Musa, ambao walikuwa watu waelewa na wenye ufahamu sahihi wa mambo, badala ya kujidunisha na kujidogesha na kumkweza na kumtukuza Qarun, walimkabili na kumuasa kwa kumwambia tahadhari usije ukaingiwa na ghururi kwa sababu ya mali na utajiri wako; kwani ukifikia hali hiyo hutopendeza tena mbele ya Mwenyezi Mungu, kama ambavyo watu pia hawawapendi matajiri wenye ghururi. Aya ya 77 tuliyosoma inaendeleza maudhui ya aya hiyo iliyotangulia kwa kutaja nasaha nyengine nne zilizotolewa na waumini hao wanaofikiria mwisho na hatima ya jambo, ambapo nasaha muhimu zaidi kati ya hizo ni kwamba dunia ni shamba la mavuno ya akhera. Yaani kama hutopanda kitu hapa duniani, hutokwenda kuvuna chochote Siku ya Kiyama. Mali na utajiri wote huu ni mithili ya mbegu ambayo inapasa ipandwe ardhini ili iweze kutoa mazao. Kuzirundika mbegu ghalani, hata kama zitakuwa nyingi kiasi gani hakuwezeshi kuchipua miche. Nasaha ya pili ni kwamba kama tunakwambia wewe Qarun jitayarishie kutokana na mali ya dunia masurufu ya akhera, maana yake si kwamba usahau kabisa maisha ya dunia na utoe mali zako zote katika njia ya Mwenyezi Mungu; hasha wa kalla! Zitumie pia kwa ajili ya kujineemesha wewe mwenyewe pamoja na familia yako. Shughulika na zote mbili, dunia na akhera; na kila moja ifanyie kazi kwa kiwango inachostahiki. Amma nasaha ya tatu ni kwamba usidhani kuwa hayo uliyonayo ni milki yako wewe. Mali na utajiri wote huo ni milki ya Mwenyezi Mungu, ambaye amekufanyia ihsani ya kukupa wewe. Usijione kuwa ni mmiliki, wewe ni mshika amana tu, kwa hivyo na wewe pia wafanyie wema na ihsani wanyonge na wahitaji. Na nasaha ya nne ambayo waumini hao walimpa Qarun ni kwamba ikiwa hutoyajali, ukayapuuza na kutoyafanyia kazi mawaidha haya ujue kwamba mali na utajiri huo utakufisidi wewe mwenyewe pamoja na jamii pia. Badala ya mali na utajiri wako kutengeneza mambo ya jamii, utakuwa chanzo cha kugawika jamii kitabaka na kuongezeka chuki na uadui wa watu dhidi yako. Na hivyo ndivyo wapenzi wasikilizaji, inavyoshuhudiwa leo hii ndani ya jamii za kibepari, ambapo asilimia ndogo kabisa ya watu ndio wanaomiliki mabenki na mitaji yote ya mali katika jamii huku akthari ya watu wakitaabika kufanya kazi kama watumwa ili kuwatajirisha zaidi na zaidi matajiri na mabepari hao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba lengo na makusudio ya mtu katika kazi na shughuli zake za kiuchumi yanatakiwa yalenge kupata radhi za Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, japokuwa mahitaji ya dunia yake mtu pia yanapasa yakidhiwe kupitia njia hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa tunapaswa kufikiria na kuzingatia hatima yetu ya akhera na wakati huohuo kunufaika na neema za dunia. Kwa maneno mengine, tutenge fungu la matakwa na mahitaji yetu ya kimaumbile, kilichobakia tutumie kujitengenezea akhera yetu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba ikiwa mali na utajiri utatumiwa katika mambo ya kheri na ya kuwafanyia wema watu kwa ajili ya akhera itakuwa sababu ya mtu kupata saada na fanaka ya milele.  

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 78 ambayo inasema:

قَالَ إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَى عِلْمٍ عِندِي أَوَلَمْ يَعْلَمْ أَنَّ اللَّهَ قَدْ أَهْلَكَ مِن قَبْلِهِ مِنَ الْقُرُونِ مَنْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُ قُوَّةً وَأَكْثَرُ جَمْعًا وَلا يُسْأَلُ عَن ذُنُوبِهِمُ الْمُجْرِمُونَ

Akasema: Kwa hakika nimepewa haya kwa sababu ya ilimu niliyo nayo. Je! Hakujua kwamba Mwenyezi Mungu amekwisha waangamiza, katika vizazi vya walio kabla yake, watu walio kuwa wenye nguvu zaidi kuliko yeye, na wenye makundi makubwa zaidi kuliko yake? Na (wakati wa kuteremshwa adhabu) wakosefu hawataulizwa khabari ya dhambi zao.

Aya hii inaeleza jawabu alilotoa Qarun kwa mawaidha na nasaha alizopewa na waja waumini wa kaumu ya Nabii Musa; ambapo badala ya kuyakubali aliyoelezwa na kuyafanyia kazi alijibu kwa ghururi na kiburi kuwa: mali na utajiri huu umetokana na elimu, ujuzi na juhudi zangu mwenyewe. Kwa hivyo mwenye mamlaka nao ni mimi sio nyinyi, hata mnambie nini nifanye na nini nisifanye. Mimi mwenyewe ninajua nitumie wapi na niweke akiba wapi. Ikiwa Mwenyezi Mungu amenipa utajiri huu bila ya shaka ameona ujuzi wangu na juhudi zangu hivyo akaniona nina ustahiki. Qur'ani tukufu imeijibu mantiki hii potofu ya matajiri wenye ghururi kwa kusema: kwani yeye Qarun hajasoma historia, na hajui kwamba walikuwapo watu wenye nguvu zaidi na matajiri wakubwa zaidi kuliko yeye lakini kutokana na kuasi na kuipa mgongo haki waliangamizwa wao na mali zao papa hapa duniani? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba hata kama mali na utajiri hutokana na ujuzi na elimu ya mtu havipasi kumghafilisha yeye na kumtia ghururi; bali inampasa ajue kwamba vyote hivyo vimetokana na ihsani ya Mola kwake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuingiwa na ghururi kwa sababu ya elimu, madaraka na utajiri huweza kumfanya mtu aangamizwe papa hapa duniani. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa ya 699 ya Qur'ani. Tunamwomba Allah atulinde na fitna ya mali, atujaalie kuwa miongoni mwa wale wanaotumia mali waliyojaaliwa katika njia ya kupatia radhi zake Mola. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/