Jan 03, 2017 10:42 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 79-82 (Darsa ya 700)

 

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 700, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 79 na 80 ambazo zinasema:

فَخَرَجَ عَلَى قَوْمِهِ فِي زِينَتِهِ قَالَ الَّذِينَ يُرِيدُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا يَا لَيْتَ لَنَا مِثْلَ مَا أُوتِيَ قَارُونُ إِنَّهُ لَذُو حَظٍّ عَظِيمٍ

Basi akawatokea watu wake katika pambo lake. Wakasema wale walio kuwa wanataka maisha ya duniani: Laiti tungeli kuwa tunayo kama aliyo pewa Qaruni! Hakika yeye ni mwenye bahati kubwa.

وَقَالَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ وَيْلَكُمْ ثَوَابُ اللَّهِ خَيْرٌ لِّمَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا وَلا يُلَقَّاهَا إِلاَّ الصَّابِرُونَ

Na wakasema wale walio pewa ilimu: Ole wenu! Thawabu za Mwenyezi Mungu ni bora kwa mwenye kuamini na akatenda mema. Wala hawatapewa hayo isipo kuwa wenye subira.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Qarun alikuwa mmoja wa wafuasi wa Nabii Musa (AS). Lakini mali na utajiri mkubwa aliojaaliwa vilimtia ghururi akatakabari na kuasi na kutoka nje ya mstari wa imani. Aya tulizosoma zinaashiria moja ya tabia mbaya na chafu ya Qarun na ambayo mfano wake inashuhudiwa sana katika jamii za leo. Ni tabia ya kujigamba kwa kuonesha utajiri wake kwa namna mbalimbali na kuwadunisha na kuwadhalilisha watu wengine. Kujionesha huko baadhi ya wakati huwa ni kwa sura ya kujenga nyumba za fahari kiasi cha kumshangaza na kumstaajabisha kila anayeziona. Wakati mwengine huwa ni kwa kununua na kupanda magari ya anasa na ya bei ghali na kutamba nayo kwa mbwembwe na maringo huku na kule mijini na majiani; na wakati mwengine huwa ni kwa kuandaa karamu na dhifa za israfu na gharama chungu nzima zenye kila aina ya mapambo na madoido. Hayo ni mambo yanayofanywa na matajiri wabinafsi na walioleweshwa na mali na utajiri wao. Majigambo na majinato hayo baadhi ya wakati huwafanya watu washushe pumzi kwa majonzi na hali ya kukata tamaa na kujihisi ni mafakiri na wasio na bahati na hata kudhani kwamba matajiri kama hao ni watu waliofikia kilele cha bahati njema, saada na fanaka. Tab'an watu weledi na waelewa wanafahamu barabara kwamba si mali na utajiri peke yake vinavyomletea mtu furaha na ufanisi; na si kila tajiri ni mtu mwenye bahati na fanaka. Kuna matajiri wangapi na wangapi wanaosumbuliwa na matatizo ya kiroho na kiakili au ya kifamilia, na badala ya utajiri wao kuwaletea raha na furaha huwa sababu ya kufikwa na mazonge na masaibu chungu nzima. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa na mali na utajiri si jambo baya. Ila kujigamba, kujionesha na kufanya madaha na mambo ya fahari yanayowadunisha na kuwadhalilisha watu wengine ndilo jambo lenye kukemewa na lenye kuchukiza. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ikiwa watawala katika jamii watakuwa na hulka za kibwanyenye na Kiqaruni watauathiri utamaduni, thamani na tunu za jamii na kuwafanya watu wao wakumbatie na kuabudu maisha ya starehe na anasa. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kupenda dunia ndio matamanio ya watu wasio na busara na wenye uono finyu; lakini sivyo walivyo watu waelewa na wenye busara. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa mali na utajiri wa dunia nzima si lolote si chochote mbele ya Pepo ya Allah ambayo ni tuza na jaza watakayopewa waja safi na wema. Kwa hiyo inafaa watu wajuzi na watambuzi wawahadharishe watu na hatari ya kupenda dunia na kuabudu mali.

Darsa ya 700 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 81 na 82 ambazo zinasema:

فَخَسَفْنَا بِهِ وَبِدَارِهِ الأَرْضَ فَمَا كَانَ لَهُ مِن فِئَةٍ يَنصُرُونَهُ مِن دُونِ اللَّهِ وَمَا كَانَ مِنَ المُنتَصِرِينَ

Basi tukamdidimiza yeye na nyumba yake katika ardhi; wala hapakuwa na kundi lolote la kumnusuru na (adhabu ya) Mwenyezi Mungu, wala (mwenyewe) hakuweza kujitetea.

وَأَصْبَحَ الَّذِينَ تَمَنَّوْا مَكَانَهُ بِالأَمْسِ يَقُولُونَ وَيْكَأَنَّ اللَّهَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاء مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَوْلا أَن مَّنَّ اللَّهُ عَلَيْنَا لَخَسَفَ بِنَا وَيْكَأَنَّهُ لا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

Na wale walio tamani kuwa pahala pake jana, wakawa wanasema: Kumbe Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na humdhikisha amtakaye. Asingetufanyia hisani Mwenyezi Mungu angeli tudidimiza. Kumbe makafiri hawafanikiwi! 

Kuwadunisha watu kwa kujionesha kwa mali na kukaidi kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa hoja ya kutokuwa na haja ya akhera kulimfikisha Qarun kwenye hatima mbaya mno, ya Allah SW kumshushia zilzala na tetemeko kubwa lililolizamisha ardhini kasri lake, konde yake na hazina yake yote pasina kusalia athari yoyote ya yeye mwenyewe na kila alichokuwa nacho. Bila ya shaka Qur'ani tukufu imetaja habari za kuangamizwa kwa zilzala na matetemeko ya ardhi kaumu na umma mbalimbali zilizopita. Lakini katika tukio hili ni Qarun peke yake pamoja na kasri lake ndio waliozamishwa ardhini; lakini watu wengine wote hawakudhurika hata kidogo. Na huu wenyewe ulikuwa muujiza mwengine. Kama ambavyo Firauni aliyekuwa akijiona kuwa ndiye mwenye mamlaka mutlaki ya Misri na Mto Nile aligharikishwa ndani ya maji ya mto huo, na nguvu zake pamoja na utawala wake vikaangamizwa.  Wale watu wa kawaida walipoona muujiza huo walizinduka kwenye usingizi wa mghafala na kukiri kuwa walikosea kutamani kuwa na mali na utajiri wa Qarun, kwa sababu riziki ya kila mtu iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu; ni Yeye, na kwa elimu na hekima yake, anaigawa riziki baina ya waja wake, na kila mmoja ni mas-uli kulingana na kile alichopewa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mwisho wa uasi, kujikweza na kujisahau ni idhilali na maangamizi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hata kama mali na utajiri utakuwa mwingi na mkubwa kiasi chochote kile hauwezi kumnusuru mtu na ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba tusiwe na papara ya kuhukumu jambo; wale waliotamani wawe kama Qarun kwa kuona utajiri wake, walipoona hatima na mwisho mbaya uliomfika walisema, imekuwa heri hatukujaaliwa kuwa kama alivyokuwa yeye. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa tukinai na kutosheka na kile alichotupa Allah badala ya kutamani mali na utajiri waliopewa watu wengine. Na tujue kwamba hakuna heri na maslaha na sisi kupata yote tunayoyatamani katika dunia hii. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo ya Qur'ani imefikia tamati.  Tunamwomba Allah atupe utajiri wa nafsi, wa kutosheka na kuridhika na kile alichotukadiria Yeye. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/