Jan 16, 2017 11:35 UTC

Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 50-55 (Darsa ya 713)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 713, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 50 na 51 ambazo zinasema:

وَقَالُوا لَوْلا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَاتٌ مِّن رَّبِّهِ قُلْ إِنَّمَا الآيَاتُ عِندَ اللَّهِ وَإِنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ

Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Hakika ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji mwenye kubainisha tu.

أَوَلَمْ يَكْفِهِمْ أَنَّا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ يُتْلَى عَلَيْهِمْ إِنَّ فِي ذَلِكَ لَرَحْمَةً وَذِكْرَى لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

Je! Kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu hiki wanacho somewa? Hakika katika hayo kuna rehema na mawaidha kwa watu wanao amini.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia ishara mbali mbali za kuonyesha ukweli wa Qur'ani na ujumbe wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Aya tulizosoma zinasema: "Licha ya ishara zote hizo makafiri waliendelea kutafuta visingizio mbalimbali kama kusema, kwa nini Muhammad hatuletei miujiza kama waliyokuja nayo Musa na Isa?! Kwa nini hafanyi tunayoyataka sisi?! Kwa nini hatowi chemchemi zinazotiririka maji katika uwanda na jangwa la ardhi kavu?! Kwa nini hatuletei ujumbe wa maandishi unaotoka kwa Mungu wake?!

Ukweli ni kwamba wao hawakuwa na nia ya kutaka kusilimu na kumwamini Bwana Mtume SAW kama ambavyo kaumu nyingine nyingi zilizopita pia licha ya kuona miujiza kwa Manabii Musa, Isa na Mitume wengineo hawakuwaamini Mitume hao bali nao pia walitafuta na kuzusha visingizio vya kila namna.

Mwenyezi Mungu ameiteremsha Qur'ani ukiwa ni muujiza wa milele wa Nabii Muhammad SAW, na licha ya walioikanusha kujaribu kufanya kila njia, hawakuweza kuleta hata sura moja inayofanana na sura za kitabu hicho kitukufu. Isitoshe ni kwamba muujiza hauko mikononi mwa Mitume, bali ni jambo ambalo Allah SW mwenyewe hulifanya lithibiti pale atakapo Yeye, na bila ya shaka si kwa ombi la makafiri. Jukumu la msingi la Mitume ni kuwapa muongozo na kuwaelekeza watu kwenye uongofu kwa njia ya bishara na maonyo ambako kunawiyana na akili, mantiki na fitra na maumbile ya mwanadamu; na si kuwa kama wachawi na wafanya mazingaombwe kwa kufanya mambo ya ajabuajabu na ya kushangaza ili watu wavutiwe na kuwafuata wao. Wapinzani wa haki walikuwa wakitaka waoneshwe miujiza ya kimaada ambayo ni ya kuja na kuondoka ilhali Qur'ani ni muujiza wa kimaanawi na wa kubaki milele wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Kitabu chenye muhtawa na mambo makubwa kabisa ndani yake ambacho kimeletwa na mtu ambaye hakusoma wala kujifunza katika chuo au madrasa yoyote bali kwa rehma na ukarimu wa Allah amekuwa mwalimu wa wanadamu wa zama zote za historia.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba muujiza wa Mtume wa mwisho ni wa maneno yaliyoandikwa ambao ni wa milele na wa ulimwengu mzima. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Qur'ani ni kitabu kilichokamilika na chenye kujumuisha kila kitu ambacho kimetoa majibu kwa mahitaji yote ya kimaanawi ya mwanadamu na kinaweza kueleweka na kufahamika na vizazi vyote katika zama zote. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Qur'ani ni kitu kinamchotoa mtu kwenye mghafala na kujisahau na kumfanya ateremkiwe na rehma na fadhila zisizo na ukomo za Allah SW.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 52 na 53 ambazo zinasema:

قُلْ كَفَى بِاللَّهِ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ شَهِيدًا يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَالَّذِينَ آمَنُوا بِالْبَاطِلِ وَكَفَرُوا بِاللَّهِ أُوْلَئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ

Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina yangu na nyinyi. Anayajua yaliomo mbinguni na ardhini. Na wale wanao amini batili na wakamkufuru Mwenyezi Mungu, hao ndio walio khasirika.

وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَلَوْلا أَجَلٌ مُّسَمًّى لَجَاءَهُمُ الْعَذَابُ وَلَيَأْتِيَنَّهُم بَغْتَةً وَهُمْ لا يَشْعُرُونَ

Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau si wakati maalumu ulio wekwa, basi adhabu ingeli wajia, na hakika ingeli watokea ghafla, na hali wao hawana khabari.

Aya hizi, upande mmoja zinamliwaza Bwana Mtume SAW kwamba ikiwa makafiri wanaukanusha ujumbe wako, hilo lisidhoofishe azma na irada yako katika kazi yako kwani Allah SW ni shahidi wa idili na juhudi unazofanya na Yeye ndiye mlinzi na msaidizi wako. Na upande mwingine, Bwana Mtume anawatangazia makafiri kwamba kama kweli mimi si Mtume na haya ni madai tu ninayonasibisha na Mwenyezi Mungu, Yeye Mola ni Mjuzi wa kila kitu na ni shahidi wa niyafanyayo, kwa hivyo atanifedhehesha tu. Kisha aya zinaendelea kueleza kuwa: Lakini makafiri wakaidi wanasema: kama uyasemayo ni kweli basi tushushie hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu; hali ya kuwa wao hawajui kwamba Allah anawapa waja wake muhula na fursa ya kuchagua kwa uhuru na hiyari yao njia ya maisha wanayotaka kufuata.

Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuamua makafiri kufuata njia ya kufru na batili na kutokuwa tayari kumwamini Mwenyezi Mungu kusiwavunje moyo waumini, kwani Allah ni Shahidi na mwenye kuona kila kitu na mwishowe ni wao makafiri ndio watakaohasirika na kuharibikiwa. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Mwenyezi Mungu Mwenyewe anathibitisha na anashuhudia kuhusu ukweli wa Utume wa Nabii Muhammad SAW. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu inateremshwa kwa hekima na kwa mipango maalumu, si kwa pupa na kukurupuka. Inafuata irada ya Allah, si matakwa ya watu wakaidi, wenye inadi na wasio na uelewa.

Darsa yetu ya leo ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 54 na 55 ambazo zinasema:

يَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ

Wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka, na hali Jahannamu kwa hakika imewazunguka makafiri!

يَوْمَ يَغْشَاهُمُ الْعَذَابُ مِن فَوْقِهِمْ وَمِن تَحْتِ أَرْجُلِهِمْ وَيَقُولُ ذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

Siku itapo wafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na atasema: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyatenda!

Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kuhusu takwa la kejeli na istihzai la makafiri la kutaka wateremshiwe adhabu haraka na kueleza kwa kuhoji: Kwa nini mnaharakisha adhabu bila ya sababu? Hivi sasa hapo mlipo pia mnaishi katika jahanamu lakini wenyewe hamjui. Ni jahanamu ya dhulma na utovu wa uadilifu; jahanamu ya vita na umwagaji damu; jahanamu ya machafuko na ukosefu wa amani na usalama na jahanamu ya wahaka, fadhaa, msongo wa mawazo n.k. Wao walikuwa wakidhani kwamba adhabu ni kukumbwa na tufani, mafuriko na zilzala tu! Lakini Qur'ani inawaambia, mambo mnayoyafanya hayana tija na matokeo mengine ghairi ya hayo matatizo na masaibu yanayompata mtu mmoja mmoja na jamii yenu kwa ujumla; adhabu yenu ya hapa duniani ni matokeo ya amali zenu ovu. Na bila ya shaka akhera pia mtaingia kwenye Moto wa Jahanamu ambao macheche yake yatakuzungukeni kila upande na hamtakuwa na pa kukimbilia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuchelewesha Allah adhabu ya maangamizi kwa makafiri hapa duniani ni fursa kwao ya kutubia na kurejea kwa Mola. Lakini wao hawaitumii fursa hiyo wanayopewa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kila amali ina batini ambayo hakika yake itadhihirika huko akhera. Jahanamu nayo ni dhihirisho la amali za mtu hapa duniani. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 713 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atakabali dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../