Feb 06, 2017 10:24 UTC
  • Maadhimisho ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu (7)

Hali ya kisiasa ya nchi zinazoizunguka Iran daima imekuwa ikiathiri usalama wa taifa hili. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina mpaka ulio na urefu wa kilomita 2000 katika Ghuba ya Ujemi na bahari ya Oman, jambo ambalo lina umuhimu mkubwa wa kijiografia, kiusalama na kisiasa kwa taifa hili la Kiislamu.

Ghuba ya Uajemi ina umuhimu mkubwa wa kiusalama na kijiografia duniani na ndio maana ikawa inazingatiwa sana na nchi za kigeni zinazotaka kuvuruga usalama wa mataifa ya eneo hili na kuyafanya yasijidhaminie usalama wao yenyewe. Miongo kadhaa iliyopita nchi za eneo hili zilibuni mifumo kadhaa ya kiusalama ikiwemo ya Sa'dabad, Baghdad, Umoja wa nchi za Kiarabu na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi katika kipindi cha kambi mbili kuu za Magharibi za Mashariki. Kwa bahati mbaya mikataba na mifumo hiyo ya ulinzi na usalama ilidhibitiwa na nchi za Magharibi na hasa Marekani ambayo ilitumia kila mbinu ili kuhakikisha kuwa inadhibiti na kusimamia usalama wa nchi wanachama wa mikataba hiyo ya kiulinzi na kijeshi.

Sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran zinawashirikisha wakubwa kwa wadogo

 

Katika hali ya hivi sasa pia mikataba ya kijeshi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi imesimama kwenye msingi wa ununuzi wa silaha kutoka nchi za Magharibi kwa ajili ya kukabiliana na adui bandia anayebuniwa na nchi hizo. Siasa hizo zinazofuatwa na nchi za Ghuba ya Uajemi zikiongozwa na Saudi Arabia zimeyafanya mashirika ya utengenezaji silaha ya Marekani na Uingereza kuzingatia kwa namna maalumu soko la silaha la nchi za Kiarabu za eneo hili. Kusuhu suala hilo siku chache zilizopita gazeti la Uingereza la The Guardian liliandika kuwa katika kipidi cha muongo mmoja uliopita Uingereza ilikuwa muuzaji mkubwa zaidi wa pili wa silaha ulimwenguni ambapo ilifanikiwa kuuza nje silaha zenye thamani ya pauni bilioni 100. Marekani nayo tokea mwaka 2009 imeziuzia nchi za Kiarabu za Ghiuba ya Uajemi silaha mbalimbali zenye thamani ya dola bilioni 198. Kwa kuwa na vituo vya kijeshi zaidi ya 14 Mashariki ya Kati, Marekani ina nafasi muhimu katika masuala ya kiusalama na ulinzi ya eneo hili muhimu duniani. Katika ripoti yake ya hivi karibuni kabisa, Kituo cha Utafiti wa Amani ya Kimataifa kilicho na makao makuu yake mjini Stockholm Uswisi kinasema kwamba Kiwango cha uuzaji silaha kwa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kiliongezeka kwa asilimia 70 miaka mitano iliyopita ambapo nyingi ya silaha hizo zilikuwa za Uingereza. Katika hali ambayo Ghuba ya Uajemi imeshuhudia vita haribifu zaidi katika miongo mitatu iliyopita vikiwemo vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran na vya Kuwait, walionufaika zaidi na vita hivyo ni nchi za Magharibi. Hivi sasa wimbi la kuibuka makundi hatari ya kigaidi limeenea na kuvuruga usalama wa nchi zote za nusu ya magharibi mwa Asia. Kuhusu jambo hilo, kuwepo kwa ushawishi wa nchi za kigeni na hasa Marekai na Uingereza katika matukio ya nchi za Ghuba ya Ujemi kumezuia kabisa kupatikana ushirikiano wa kiusalama wa nchi hizo katika kujidhaminia usalama wao. Mazingira ya hivi sasa ya eneo yanaonyesha ukweli huu kwamba iwapo ushirikiano hautakuwepo kati ya nchi hizo na kuendelea kuwepo vitisho vya usalama kutoka nje, ni wazi kuwa usalama wa nchi hizo utakuwa hatarini. Tokea wakati wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran miaka 38 iliyopita madola ya kiistikbari na kikoloni ya Magharibi hayajatoa mwanya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuzibainishia nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi malengo yake ya ushirikiano wa kiusalama. Licha ya kufahamu vyema kwamba Mapinduzi ya Kiislamu hayakuwa na malengo yoyote ya vita dhidi ya majirani zake, lakini madola hayo yalichochea na kuanzisha vita vya kulazimishwa dhidi ya mapinduzi hayo. Kuhusu suala hilo Hussein Zakaa, mjuzi wa mambo raia wa Lebanon anasema: ''Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapatikana katika eneo ambalo lina umuhimu mkubwa wa kistratijia na kimataifa. Eneo hili ni miongoni mwa maeneo mahimu zaidi duniani ambapo katika miaka iliyopita lilishuhudia matukio tofauti muhimu, hitilafu, kutoaminiana na baadhi ya wakati vita ambavyo vilichochewa na nchi za kigeni. Iran imeshuhudia wazi suala hilo kuhusu masuala yanayoihusu. Marekani na nchi nyingine za Magharibi ndizo zilizokuwa waungaji mkono wakubwa wa Saddam katika vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran."

 

Hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikisisitiza juu ya kulindwa na kuheshimiwa mipaka ya kijiografia ya kila nchi, na imekuwa ikipinga vikali kugawanywa nchi zinazojitawala na kusisitiza kutatuliwa kidiplomasia hitilafu zinazojitokeza kati ya nchi hizo. Jamhuri ya Kiislamu inaamini kwa dhati kwamba mapambano dhidi ya changamoto za pamoja na hasa zile zinazohusiana na ugaidi yanaweza kufanikishwa na kutekelezwa kwa mafanikio kupitia ushirikiano wa nchi za eneo. Kwa masikitiko makubwa baadhi ya nchi kwa kuunda muungano bandia eti wa kupambana na ugaidi, badala ya kupambana na magaidi sugu wanaofanya ukatili wa kitisha katika nchi tofauti za Kiislamu na hasa Syria na Iraq zimekuwa zikiwaunga mkono kwa siri na hadharani magaidi hao wa kikatili. Marekani ni moja ya nchi za hizo ambapo John Kerry waziri wake wa zamani wa mambo ya nje alisikika akikiri waziwazi katika moja ya mikanda ya sauti kuhusu uungaji mkono wa nchi yake kwa kundi hatari la kigaidi la Daesh.

Ni wazi kuwa siasa hizo hazina natija nyingine isipokuwa kuendelea kuchochea mauaji dhidi ya watu wasio na hatia na hii ni kwa sababu ugaidi hauna huruma na mtu yoyote yule na huwakumba wote waliomo na wasiokuwemo. Matukio yaliyotokea katika miaka na siku za hivi karibuni katika nchi za Ufaransa, Ujerumani, Uturuki na nchi nyinginezo ni thibitisho tosha kwamba ugaidi na vita vya kichokozi ambavyo leo vimeyasababishia matatizo mengi mataifa tofauti ni matokeo ya moja kwa moja ya maamuzi na misimamo isiyokuwa ya kimantiki inayochukuliwa na baadhi ya nchi katika kulitizama kimaslahi suala zima la ugaidi. Uungaji mkono ulioonyeshwa na wawakilishi wa nchi 190 za dunia katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 19 Disemba 2013 kwa azimio lililopendekezwa na rais wa Jmhuri ya Kiislamu ya Iran, la kupinga kila aina ya ugaidi na kupatikana dunia isiyokuwa na vita wala matumizi ya nguvu ni jambo linalothibitisha wazi kwamba Iran inapinga vikali vita na fikra za kupindukia mipaka ulimwenguni.

Hakuna shaka yoyote kwamba katika hali tata ya hivi sasa kieneo na kimataifa, kila aina ya mughafala na upuuzaji wa ushirikiano wa kiusalama baina ya nchi za eneo itaandamana na matokeo hatari kwa nchi husika. Hali ya hivi sasa ya Mashariki ya Kati na hasa mgogoro wa Syria na machafuko yanayoendelea nchini Iraq, Afghanistan na Yemen ni matokeo ya moja kwa moja kuhusu suala hilihili la kutazama ugaidi kwa mitazamo miwili tofauti ya kimaslahi. Matukio ya zamani na ya hivi sasa ya eneo na kimataifa yanaonyesha kwamba hakuna wakati wowote ambao Marekani imejiweka mbali na uchochezi wa vita. Kuwepo kwa vituo vya kudumu vya kijeshi na kijasusi vya nchi hiyo huko Bahrain, Qatar, Kuwait, Saudi Arabia na Imarati na nchi nyingine za dunia ni jambo linaloonyesha wazi utambulisho wa kivita wa nchi hiyo ya Magharibi. Ujumbe wa uwepo huo wa kijeshi wa Marekani ni kuwa nchi hiyo ni tishio kwa usalama wa eneo na dunia nzima kwa ujumla. Ni sawa kabisa na kama alivyosema Dakta Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kwamba wale wanaopiga makelele ya kuwa eti Iran ni tishio, kwa hakika ima wao wenyewe ndio tishio halisi kwa amani na usalama wa dunia au wanachochea ghasia na kukuza tishio hilo. Rais Rouhani alisisitiza kwamba si tu kwamba Iran sio tishio bali kivitendo ni muhubiri mkubwa wa amani, uadilifu na usalama wa pande zote duniani. Katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita Marekani imekuwa ikifuatilia siasa za eti kuleta mabadiliko duniani ambazo zilianza kutekelezwa katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais Barack Obama ambaye tayari amemaliza kipindi chake cha pili na sasa Donald Trump ameshika usukani wa nchi hiyo hali ya kuwa muelekeo wake wa kisiasa haufahamiki vyema. Pamoja na hayo lakini jambo lililo wazi ni kuwa Marekani na Uingereza katika siasa zao za miongo minne iliyopita zimekuwa zikifuatilia siasa za ubeberu na ukandamizaji wa mataifa mengine huru yanayopinga siasa zao za kidhulma duniani. Kuhusiana a suala hilo, Hannana Subhan Abdallah, mjuzi wa mambo wa nchini Iraq anasema: "Uadui wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hautokani na mambo kama vile ya kuenezwa nje Mapinduzi ya Kiisalmu, haki za binadamu wala suala la nyuklia. Viongozi wa Marekani wana tatizo na utambulisho wa Kiislamu wa Mapinduzi, mapambano dhidi ya dhulma na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokubali mapatano ya kidhalimu. Marekani inayatazama Mapinduzi ya Kiislamu kuwa mwanzilishi wa mwamko wa Kiislamu duniani na kituo cha mapambano dhidi ya siasa zake za ubeberu na kwa msingi huo katika kipindi cha miaka 38 iliyopita imekuwa ikifanya kila juhudi kwa ajili ya kuufuta kabisa mfumo wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hakuna shaka yoyote kwamba ubeberu wa Marekani dhidi ya Iran utaendelea katika muongo wa nne wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuendelea kuongezwa majeshi ya Marekani na Uingereza katika eneo pia kunafanyika kwa lego hilo." Kwa hakika lengo lao la kuongeza askari jeshi wao katika eneo ni kujaribu kuvuruga na kuiletea matatizo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kulinda uthabiti na usalama wa Mashariki ya Kati. Hii ni kwa sababu Iran inataka kuwepo ushirikiano wa nchi zote za eneo katika kuimarisha usalama na amani ya eneo hili bila kuwepo uingiliaji wa madola ya kigeni.

Maandamano ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran

 

Na hadi hapa wasikilizaji wapenzi ndio tunafikia mwisho wa sehemu ya saba ya vipindi hivi vinavyozungumzia maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Basi hadi wakati mwingine tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

Tags