Feb 07, 2017 16:42 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika mfululizo wa vipindi hivi vinavyokosoa kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu na suna za Bwana Mtume (saw) makundi ya ukufurishaji yanayotekeleza jinai za kutisha dhidi ya Waislamu wengine hii ikiwa ni sehemu ya 22 ya mfululizo huo.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia namna ambavyo dini ya Kiislamu ilivyopiga marufuku aina yoyote ya utesaji na ukataji wa viungo vya binadamu, tukasema kwamba, mtu anayefanya jinai hiyo Mwenyezi Mungu amemuandalia adhabu kali ya Jahanam. Tukasema kuwa, katika hilo Mtume Muhammad alikuwa akiliusia jeshi la Kiislamu kuchunga haki za binaadamu wakati lilipokuwa likienda vitani. Katika fremu hiyo Nabii huyo wa Allah amewataka Waislamu kuwaheshimu wanyama na kujiepusha kuwatesa kwa aina yoyote ile. Kwa hakika dini ya Kiislamu ni dini ya upole na huruma kiasi kwamba, hata inawataka wafuasi wake kuchunga haki za wanyama ambao sio wanadamu. Katika hali kama hiyo ni vipi dini hii inayousia amani na upendo kiasi hicho inaweza kuhalalisha jinai za makundi ya kigaidi na ukufurishaji? Ndugu wasikilizaji kama tulivyosema, mafundisho, sheria na matukufu yote ya dini ya Uislamu yamejengeka juu ya msingi wa kuheshimu utukufu na haki za binaadamu katika kila wakati na sehemu. Mbali na hayo ni kwamba, lingamanio la dini ya Uislamu pia limejengeka juu ya msingi huo wa kuheshimu matukufu na haki za binaadamu. Kadhalika kitu ambacho kilichangia kuenea kwa haraka dini hiyo katika eneo la Bara Arabu na nje ya mipaka ya eneo hilo, ilikuwa ni mafundisho yake mazuri yanayolingania upendo, huruma, udugu na mengine kama hayo yaliyokuwa yakisisitizwa na Mtume Muhammad (saw). Kuhusiana na hilo Mwenyezi Mungu anasema: " Nasi hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote." Surat Anbiyaa aya ya 107. Ni suala lililo wazi kwamba, rehema inayokusudiwa katika aya hiyo ni yenye maana pana sana ambapo viumbe wote duniani na kwa muda wote hata Malaika wa Mwenyezi Mungu nao wanajumuishwa katika rehema hiyo. Kwa mujibu wa wafasiri wa Qur'ani Tukufu wakati aya hiyo ilipomshukia Mtume wa Mwenyezi Mungu Nabii wa Allah alimuuliza Jibril kama ninavyonukuu: "Je, kuna sehemu iliyokupata katika rehema hiyo? Jibril akasema: Ndio, hakika mimi nilikuwa nina wasi wasi juu ya hatma yangu, lakini nimepata matumaini kwako wewe." Mwisho wa kunukuu.

*****************************************

Ndugu wasikilizaji mnapaswa kufahamu kwamba, Mwenyezi Mungu alimtuma Mtume Muhammad (saw) ili awe rehema kwa walimwengu. Kama ilivyo sifa ya rehema ya Mwenyezi Mungu ambapo inawahusu watu wote wakiwemo waumini na makafiri, kadhalika Mtume Muhammad ni rehema kwa walimwengu wote hadi mwisho wa dunia si tu kwa wafuasi na marafiki wake bali kwa kila kiumbe duniani, wema, wabaya, marafiki wake au hata maadui. Wanadamu wote duniani wakiwemo makafiri na waumini wote wanategemea rehema za Nabii huyo wa Allah. Hii ni kwa kuwa Uislamu umekuja kumuokoa mwanadamu. Hata hivyo inapotokea kundi fulani la watu likastafidi vizuri na rehema hiyo na lingine likashindwa kustafidi vilivyo, hilo haliwezi kuathiri shani ya Nabii huyo wa Allah. Hii ni sawa na mfano wa hospitali iliyopewa kibali cha kutoa huduma ya matibabu ya maradhi yote huku ikiwa na madaktari waliobobea na aina tofauti ya madawa sanjari na kuwafungulia milango wagonjwa wote, hivyo inapotokea baadhi ya wagonjwa kutotumia vyema hospitali ile hiyo haitokuwa dosari ya hospitali bali tatizo litarejea kwa mgonjwa mwenyewe. Kwa ibara nyingine ni kwamba, rehema ya Mtume kwa walimwengu inategemea juhudi za mtafutaji wa rehema hiyo. Ni kwa msingi huo ndio maana katika dini ya Kiislamu haifai kumlazimisha mtu kujiunga na dini hii. Hii ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu amefungua njia za kufikia utukufu na ukamilifu kwa wanadamu wote, hivyo hakuna sababu ya kumlazimisha mtu kujiunga na dini hii. Mwenyezi Mungu anasema: "Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua." Surat Baqara aya ya 256. Kwa mujibu wa aya hiyo linganio la dini ya Uislamu kwa ajili ya kumwamini Mungu Mmoja, linatofautiana kikamilifu na lile linalotumiwa na wanachama wa makundi ya kigaidi na ukufurishaji. Hii ni kwa kuwa kama tulivyosema katika vipindi vilivyopita, wakati aya ya 125 ya Surat Nahli inasema: "Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anayemjua zaidi aliyeipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka," makundi ya kigaidi na ukufurishaji yanawaita watu kwa kutumia ukatili, mauaji na jinai tofauti kama vile kuwanyonga, kuwachinja kama kuku na njia nyingine nyingi za kutisha. Kama ambavyo pia makundi hayo yanawaita watu kujiunga nayo kwa kuwalazimisha sanjari na kudai kuwa Waislamu halali ni wale tu wenye imani na itikadi kama yao la sivyo, watu wengine wote ni makafiri wanaostahili kuuawa. Hii ni katika hali ambayo aya iliyotangulia, inawaita walimwengu kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu kwa kutumia mawaidha, nasaha bora na kwa namna ya kuvutia.

********************************

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni makala yanayokosoa makundi ya ukufurishaji kwa mujibu wa aya na hadithi, kutoka Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iram.

Ndugu wasikilizaji mtakubaliana nami kwamba sira yote ya Mtume wa Uislamu Muhammad (saw) imejaa mafundisho mengi kwa ajili ya wafuasi wa dini ya Kiislamu. Moja ya mafunzo hayo adhimu ya mtukufu huyo ni kukataza kuwa na kinyongo dhidi ya mtu mwingine kwa ajili ya kulipiza kisasi. Mtume wa Allah alikuwa akisisitizia msamaha na kujiepusha na ulipizaji kisasi. Kuhusiana na suala hilo Amirul-Muuminina lmamu Ali (as) anasema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa msamehevu sana na mwenye muamala mzuri na watu wengine kuliko watu wengine wote. Alikuwa akikubali udhuru wa mwenye kumuomba msamaha au udhuru huo." Mwisho wa kunukuu. Kama ambavyo hakumfanyia vibaya mtu ambaye alimfanyia mabaya Nabii huyo wa Allah, bali kinyume chake aliwarejeshea mema watu ambao walimfanyia mabaya. Imamu ali (as) anasema: “Na hakulipiza baya kwa baya, lakini alikuwa akisamehe na mwenye subira ya hali ya juu.” Mwisho wa kunukuu. Imepokelewa kwamba katika vita vya Uhud, baada ya Wahshi kumuua na kuudhalilisha mwili wa sahaba mtukufu Hamza, ambaye pia alikuwa ami yake Mtume (saw), Nabii huyo hakulipiza kisasi kwa jinai hiyo baada ya ushindi wa Makkah bali alitoa msamaha wa jumla kwa maadui wote wa Uislamu ambao kwa miaka yote ya utume wake walikuwa wakimsumbua na kumfanyia kila aina ya mabaya. Na hata wakati Abu Qutadah alipotaka kuwaambia maneno makali watu hao akiwemo Abu Sufiyan, Mtume Muhammad (saw)  alimkataza kufanya hivyo. Kinyume chake siku  ya ushindi wa Makkah Mtume alitangaza kwa kusema: “Leo ni siku ya huruma na upole. Nendeni mkiwa huru.” Aidha mbali na hayo, imepokelewa kuwa baada ya vita vya Khaybar kumalizika, kundi fulani miongoni mwa Mayahudi lilijisalimisha mbele ya Mtume baada ya kutia sumu katika chakula chake kwa lengo la kutaka kumuua, lakini kwa upande wake mtukufu huyo aliliachilia huru akiwa mwenye kutabasamu. Kadhalika mwanamke mwingine wa Kiyahudi ambaye naye alitaka kuweka sumu katika chakula cha Mtume Muhammad (saw), naye alisamehewa na Nabii huyo wa Allah. Pia wakati jeshi la Kiislamu lilipokuwa likirejea kutoka vita vya Tabuk kundi fulani la wanafiki lilipanga njama ya kumuua Mtume kwa kumshambulia kutoka eneo lenye mwinuko, pamoja na kwamba Mtume aliwafahamu wanafiki hao na licha ya masahaba kumsihi sana ataje majina yao, lakini Nabii wa Allah hakufanya hivyo kama ambavyo pia hakuwaadhibu kwa kitendo chao hicho.

*******************************

Huruma na upole ni mambo ambayo yalitawala sira yote ya Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu kiasi cha kuifanya Qur’ani kuisifu shani hiyo katika aya ya 3 ya Surat Shuaraa kwa kusema: “Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.” Ambapo kwa mujibu wa aya hiyo, Mtume alifikia kukereka nafsini mwake kwa sababu tu ya kuhofia kwamba huenda watu wasiwe waumini. Kuhusiana na suala hilo Imam Swadiq (as) mjukuu wa Mtume ananukuu moja ya hotuba za Nabii huyo wa Allah pale aliposema: “Mola wangu ameniamuru kuishi vizuri na watu kama ambavyo ameniamuru kutekeleza wajibu.” Mwisho wa kunukuu. Aidha Mtume anasema: “Mambo matatu kama hayako kwa mtu basi matendo yake hayakamiliki. Uchaji-Mungu unaomkinga  na kumuasi Mungu, tabia njema  inayomuhifadhi baina ya watu na upole unaomkinga na shari ya wajinga.” Mwisho wa kunukuu. Katika kumalizia kipindi hiki tunatakiwa kujiuliza swali hili kwamba, je, ni sifa gani kati ya hizo ambayo inashuhudiwa kwa makundi ya ukufurishaji na kigaidi ambayo wanachama wake wanatekeleza jinai, mauaji na ukatili wa kutisha dhidi ya wanawake, watoto na wazee?

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 22 ya makala haya inafikia tamati hapa kwa juma hili. Msikose kutegea sikio sehemu ya 23 wiki ijayo. Mimi ni Sudi Jafar na hadi wakati huo, kwaherini.

 

 

Tags