Apr 08, 2017 14:08 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 29 ya makala yanayokosoa kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na suna za Bwana Mtume (saw) mienendo ya makundi ya ukufurishaji yanayotenda jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu wengine.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia taathira za vitendo na jinai za makundi ya ukufurishaji na kigaidi. Tukasema kuwa, moja ya taathira za makundi hayo ya kigaidi ni kuharibu na kuchafua sura ya Uislamu unaolingania amani, uadilifu, tauhidi na kuishi pamoja wanadamu wote wafuasi wa dini tofauti. Ukweli ni kwamba, ukatili na jinai za magenge hayo vinaenda sambamba na utekelezaji wa malengo ya madola ya Magharibi ambayo kwa kipindi cha miongo kadhaa iliyopita, yamekuwa yakijaribu kuchafua sura ya Uislamu na kuuonyesha kuwa ni dini ya ukatili na kuchupa mipaka. Kwenda sambamba malengo ya magaidi na madola hayo, ilikuwa ni fursa kubwa kwa Wamagharibi ambao kwa kutumia jinai za magenge ya kigaidi na ukufurishaji, yalieneza katika fikra za walio wengi propaganda chafu kwamba vitendo hivyo ndio uhalisia wa dini ya Uislamu.

Magaidi wa Daesh

Wakati viongozi na vyombo vya habari vya Wamagharibi wanapolitaja kundi la Daesh (ISIS) hutumia jina la 'Dola la Kiislamu' ili kwa njia hiyo kuweza kueneza sumu katika fikra za walimwengu wahisi kwamba magaidi wa kundi hilo ni wawakilishi wa dini ya Uislamu kisiasa na kiutawala, suala ambalo halina ukweli wowote ndani yake. Kwa hakika hii ni sehemu ya siasa za chuki dhidi ya Uislamu ambazo daima zimekuwa zikitekelezwa na Wamagharibi. Hapa kunajitokeza swali hili kwamba, je makundi ya kigaidi na ukufurishaji, yanawezaje kuwavutia vijana kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kufunga safari na kwenda kujiunga nayo licha ya jinai zote ambazo zimekuwa zikifanywa kila uchao na wanachama wake?

Magaidi

Katika kubainisha na kufafanua chambuzi za kiweledi wa mambo, ni kwamba kile kinachowasukuma vijana kujiunga na magenge hayo, ni hatua ya vinara wa makundi hayo ya kigaidi kutumia kimakosa aya na hadithi kwa ajili ya kuhalalisha vitendo vyao hivyo vya kikatili na vya fikra mgando na kujaribu kuvinasibisha na dini tukufu ya Uislamu. Katika fremu hiyo huweza kuingia katika mioyo ya wanachama wa magenge hayo hususan Daesh, dhana kwamba wanatumikia dini ya Uislamu. Hii ni katika hali ambayo, nadharia hiyo inapingana kikamilifu na Uislamu halisi na ni kuelewa vibaya mafundisho ya dini hiyo.

***************************************

Wanachama wengi wa makundi ya kigaidi na ukufurishaji yakiongozwa na genge la Daesh, yamekuwa na historia ya kutenda jinai na utumiaji mabavu katika nchi mbalimbali za dunia, kama ambavyo pia yamekuwa yakitambuliwa kwa kuhusika na mauaji dhidi ya binaadamu. Kwa fedha na anasa za kingono, huwafanya vijana wengi kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kufunga safari na kuelekea Iraq na Syria kwa ajili ya kujiunga na magenge hayo hatari. Lakini kwa ngazi ya juu, viongozi wa makundi hayo, ni watu ambao wanafanya mawasiliano ya karibu na idara za ujasusi na usalama za madola makubwa na baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati, na kimsingi wanatumikia siasa na maslahi ya madola hayo. Utendajikazi na hatua zao zote zinafanyika kupitia fremu ya kulinda maslahi ya kisiasa na kiusalama ya madola hayo ya Magharibi na baadhi ya waitifaki wao katika eneo.

Askari wa Syria akifyatua mzinga kuwalenga magaidi wa Kiwahabi

Kwa mfano tu, baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa genge la Daesh (ISIS) walikuwa Mabaathi watiifu kwa utawala ulioondolewa madarakani wa Saddam Hussein nchini Iraq, utawala ambao kamwe haukuwahi kutetea maslahi yoyote ya kidini. Na ni kwa ajili hiyo ndio maana hata wanachama wake wakawa wanafanya mauaji bila huruma, kufanya ndoa za Jihad, kuwabaka wanawake na watoto wa kike, kuwafanya watumwa wa ngono wanawake, kupora mali za raia na mambo mengi kama hayo ambayo kimsingi hayana uhusiano wowote na dini ya Uislamu. Ukweli ni kwamba, dukuduku la makundi hayo sio kusimamisha sharia za Kiislamu, bali ni malengo mengine yaliyo nyuma ya pazia, hata kama mara kadhaa wanachama wake wamekuwa wakitumia nara na madai ya kidini.

Magaidi wa Daesh walioangamizwa na jeshi la Iraq

Hii ni kusema kuwa, nara zao za kidini zinatolewa tu kwa lengo la kuwahadaa vijana wenye uelewa mdogo na hatimaye waweze kuwavutia kujiunga na magenge hayo ya kigaidi, au kuvutia uungaji mkono wa wananchi. Ni makundi ambayo uhalisia wake, mbali na kujengeka juu ya msingi wa ugaidi, kufanya ukatili na unyama kwa kutumia madai ya kusimamisha dini, yanatekeleza ajenda maalumu za kisiasa na kijeshi za baadhi ya tawala. Hivyo hitimisho tunalofikia ni kwamba makundi hayo hayana lengo jengine ghairi ya kuchafua taswira na sura safi ya Uislamu mbele ya macho ya walimwengu.

****************************

Kinyume na mitazamo ghalati na ya upotoshaji ya makundi ya kigaidi na ukufurishaji iliyo mbali na mafundisho ya Uislamu asili, dini ya Kiislamu ni dini nyepesi sana. Mtukufu Mtume Muhammad (saw) ambaye ni Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, aliwafundisha Waislamu kwamba, dini ni nyepesi. Hii ikiwa na maana kwamba, Mwenyezi Mungu aliwawekea wanadamu sharia nyepesi na wala hakuzifanya sharia hizo kuwa ngumu na zenye kuwataabisha mno waja wake. Ni kwa sababu hiyo, mafundisho ya dini hii ya mbinguni sio magumu wala mazito.

Rais Bashar al Assad wa Syria anayeungwa mkono na wananchi

Kuhusiana na suala hilo Mwenyezi Mungu anasema: "Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama inavyo stahiki jihadi yake. Yeye amekuteueni. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini….." Surat Hajj aya ya 78. Hata hivyo wakati Mwenyezi Mungu anasema kuwa, hajafanya uzito wowote katika dini, kundi la Uwahabi na wanachama wa makundi ya ukufurishaji yanaionyesha dini hii kuwa ngumu na iliyojaa mambo yaliyoharamishwa tu. Matamshi na nasaha zao zimejikita tu katika kupiga marufuku na kuharamisha kila kitu, isipokuwa tu endapo kutathibiti kinyume chake katika Qur'an na suna za bwana Mtume (saw.) Hii ni katika hali ambayo Uislamu umekihesabu kila kitu kuwa ni halali isipokuwa tu kama kutathibiti hukumu iliyo kinyume chake kupitia kitabu cha Allah na suna za Bwana Mtume Muhammad. Aidha tatizo jengine walilonalo Mawahabi na makundi mengine ya ukufurishaji ni kuacha kwao kuchunga misimamo ya wastani kuhusiana na sharia za dini. Hii ni katika hali ambayo Uislamu umesisitiza sana juu ya kuwa na misimamo ya wastani inayoenda sambamba na akili timamu ya mwanadamu.

Jinai za wakufurishaji wa Kiwahabi

Kwa sababu hiyo haifai kuipa uzito na umuhimu sehemu fulani ya dini kupita kiwango ambacho kimeainishwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala kuhafifisha umuhimu wa sehemu nyengine ya mafundisho ya dini hiyo. Aidha haifai kusitisha utekelezaji wa sehemu fulani ya hukumu za dini kwa ajili ya sehemu zingine. Hii ni kusema kuwa, mtazamo wa makundi ya ukufurishaji umeipa uzito kupindukia asili ya jihadi na kupotosha hakika yake na badala yake kuhafifisha na kuzipa nafasi ndogo hukumu na mafundisho mengine ya Uislamu.

********************************

Ndugu wasikilizaji inafaa tufahamu kwamba, kwa sababu mbili, katika imani na itikadi ya makundi ya ukufurishaji, suala la jihadi na kupambana limepotoshwa asili yake katika dini. Kwa kisingizio cha jihadi, magaidi hao wanakiuka misingi yote ya akhlaqi, muruwa, ubinaadamu na thamani zote za kiutamaduni na kidini. Wanachama wa magenge hayo wanawatesa na kuwaua watu bila huruma, wanayachoma moto na kuyaharibu makazi ya watu sambamba na kupora na kuharibu mali zao. Kadhalika makundi ya ukufurishaji kwa kwenda kinyume na mafundisho ya Qur'an Tukufu kuhusiana na vita dhidi ya makafiri na washirikina wenye uadui, yanatafsiri nasi hizo kwa kuwalenga Waislamu na hivyo kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya Waislamu hao. Ukweli ni kwamba, tafsiri ya makundi ya Kiwahabi kuhusiana na jihadi ni kupambana na kuwaua Waislamu wenye kutamka shahada mbili.

Mpiganaji wa harakati ya kujitolea ya wananchi nchini Iraq

Hii ni katika hali ambayo, Mwenyezi Mungu Mtukufu mbali na Waislamu amekataza hata kuwapiga vita makafiri ambao hawajawafanyia mabaya Waislamu hao. Katika hali hiyo Uislamu unawataka Waislamu kuwafanyia wema makafiri hao sambamba na kupinga Mwislamu yeyote kuanzisha vita dhidi yao. Katika hali ambayo dini hii inakataza vikali kuwapiga vita makafiri ambao hawajawafanyia mabaya Waislamu sambamba na kuhimiza kuwafanyia wema, ni vipi Uislamu huo huo utawanyoshea upanga Waislamu kama inavyoshuhudiwa leo kwa makundi ya kigaidi na ukufurishaji? Kama tulivyosema kwamba, makundi ya kigaidi na ukufurishaji yanaitambua jihadi kuwa ni wajibu wa kisheria wa kupambana na Waislamu wenye imani tofauti na Uwahabi.

Jeshi la Iraq likiwa limedhibiti daraja la Mosul

Hii ni katika hali ambayo Qur'an na Mtume wa Uislamu, wameibainisha jihadi hiyo kwamba inatakiwa ipiganwe wakati na dhidi ya watu gani, masharti ambayo hata hivyo hayazingatiwi kwa aina yoyote na wanachama wa makundi ya ukufurishaji. Kwa kutumia baadhi ya riwaya bandia na baadhi ya viashiria vinavyohusiana na mwisho wa dunia, kama vile bendera nyeusi, wanachama wa kundi la ukufurishaji la Daesh wanashikilia mikononi mwao bendera hizo na kujaribu kujiarifisha kuwa wao ni miongoni mwa walio na nafasi athirifu katika matukio ya mwisho wa dunia ambao watasimamisha dola la Uislamu kutoka mashariki hadi magharibi ya dunia. Hii ni katika hali ambayo aghalabu ya riwaya hizo ni bandia na hazina ukweli wowote. Na hata kama baadhi ya hadithi hizo ni sahihi, vinara wa genge hilo wanazitafsiri kwa kujihusisha nazo wao ili kwa ajili hiyo waweze kudhamini maslahi yao machafu.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 29 ya makala haya inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

Tags