Apr 08, 2017 14:25 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 30 ya makala yanayokosoa kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na Suna za Bwana Mtume (sawa) mienendo ya makundi ya ukufurishaji yanayotenda jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu wengine.

Katika vipindi vilivyopita tulifafanua fikra potofu za makundi ya Kiwahabi na mienendo yao ghalati ya kuwakufurisha Waislamu wengine na kisha kufanya mauaji dhidi yao. Tulisema kuwa, mienendo ya makundi hayo hususan kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) inakinzana kikamilifu na mafundisho yanayolingania uadilifu, amani na ubinadamu ya dini tukufu ya Kiislamu. Katika fremu hiyo tulitumia Qur’an, Suna za Mtume Muhammad (saw) na kauli za Ahlu Baiti wa Mtume wa Allah (as) katika kukosoa makundi hayo. Makundi ya ukufurishaji yanayofuata mafundisho ya Usalafi wa Kiwahabi ambao bendera yake hii leo inashikiliwa na Saudi Arabia, yanawaona Waislamu wengine ambao hawafuati imani yao kuwa ni makafiri na waliotoka katika dini.

Magaidi wakufurishaji wa Kiwahabi

Ndugu wasikilizaji ni vyema kuelewa kwamba, kuwakufurisha Waislamu wengine siku zote kumekuwa na taathira mbaya na chungu katika historia ya Kiislamu kote duniani. Hii ni kusema kuwa, miongoni mwa matukio yanayofuatia baada ya ukufurishaji huo ni mauaji na jinai za kutisha dhidi ya watuhumiwa. Kama inavyoshuhudiwa hii leo ulimwenguni ambapo makundi ya ukufurishaji yanafanya mauaji makubwa na ya kutisha dhidi ya Waislamu wenye kutamka shahada mbili na wasio na hatia yoyote huko Iraq, Syria, Yemen, Afghanistan, Pakistan, Nigeria, Somalia, Libya na maeneo mengine ya dunia. kosa kubwa la Waislamu hao wanaouawa ni kupinga itikadi ghalati za Uwahabi (yaani Uanswari Suna.) Hii ni kusema kuwa, mafundisho yasiyo sahihi ya Uwahabi kuhusiana na Tawhidi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu ndio yamechochea wimbi la kuwaita Waislamu wengine kuwa ni makafiri au washirikina na kisha kuhalalisha damu zao.

Jeshi la Iraq likisonga mbele kuwaangamiza magaidi hao wa Kiwahabi

Hata hivyo isisahaulike kuwa, itikadi ambayo inalinganiwa na makundi hayo ya Kiwahabi na kigaidi, hayana uhusiano wowote na dini tukufu ya Uislamu. Magaidi hao, kwa kwenda kinyume na mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu na kwa kushikamana tu na dhahiri ya aya na hadithi sambamba na kutupilia mbali nafasi ya akili, yanauarifisha Uislamu kwa walimwengu katika sura ya ukatili na iliyo kinyume na misingi ya mantiki. Ni dini ya Uislamu ambayo inaitambua misingi ya ubinadamu na kuishi pamoja kuwa inayoenda sambamba na akili salama. Katika fremu hiyo, itikadi za Kiwahabi hazina misingi ya akili wala mantiki sahihi na kielimu.

**************************************

Wasikilizaji wapenzi, kundi la Daesh (ISIS) na makundi mengine ya ukufurishaji ya Kiwahabi hayawezi kusemwa kuwa yametokana na mahitaji asili ya ulimwengu wa Kiislamu, bali ni wimbi ambalo limetokana na sababu na mabadiliko mengine mbali na ulimwengu huo wa Kiislamu na hatimaye kupanuka zaidi siku hadi siku. Kama inavyobainishwa na nyaraka na ushahidi mbalimbali wa kuaminika kwamba, makundi hayo kama lilivyo kundi la Uwahabi, yameanzishwa kama sehemu ya stratijia za Wamagharibi kwa ajili ya kuzusha farqa na mpasuko katika ulimwengu wa Kiislamu na hatimaye kuwapa Wamagharibi fursa ya kupenya na kuingia kirahisi katika nchi za Kiislamu na Kiarabu. Miongoni mwa malengo ya siasa hizo ni kudhoofisha muhimili wa muqawama, kubadili mipaka ya kijografia sambamba na kuzidhoofisha zaidi nchi za Waislamu kupitia fremu ya kulinda maslahi yao haramu na kuunga mkono utawala haramu wa Israel.

Vinara wa Daesh na Boko Haram, ambayo yote ni makundi ya Kiwahabi

Utawala wa Kizayuni wa Israel ndio unaonufaika zaidi na mapigano na mauaji yanayoshuhudiwa baina ya Waislamu. Aidha kuendelea mauaji na ukatili wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh kuliandaa fursa adhimu kwa vyombo vya habari vya Wamagharibi kwa ajili ya kushambulia Uislamu duniani. Kwa kuonyesha picha na video za jinai za kutisha kama vile kuwakata shingo watu wasio na hatia kwa kutumia jina la Uislamu, vyombo hivyo hujaribu kuonyesha sura ya ukatili na mauaji kuhusu dini ya Uislamu na kupitia njia hiyo, viweze kukamilisha mradi kabambe wa Wamagharibi dhidi ya dini hii. Katika hatua nyingine ni kwamba, kuenezwa picha za kuudhi za mauaji na ukatili katika vyombo vya habari na mitandano ya kijamii ni sehemu ya stratijia ya upashaji habari ya makundi hayo ya kigaidi hususan Daesh, ambapo hushirikiana kwa karibu na lobi ya vyombo vya habari vya Wamagharibi katika uwanja huo. Utumiaji mkubwa wa vyombo vya mawasiliano kama televisheni, redio na mitandao ya kijamii unaofanywa na kundi la Daesh unadhihirisha wazi ushirikiano wa hali ya juu wa makundi hayo na vyombo vya habari vya madola ya Magharibi.

Rais Bashar al-Assad ambaye nchi yake inakabiliwa na njama nyingi za Mawahabi na Magharibi

Ni vyema kuelewa kuwa, vyombo vya habari ni moja ya mihimili muhimu katika kufanikisha harakati za makundi hayo ya ukufurishaji. Licha ya makundi hayo kuwa na fikra zilizopitwa na wakati kwa kuamini kwamba kila kitu cha zama hizi lazima kiwe kilikuwepo zama za kwanza za kudhihiri dini ya Kiislamu, lakini wanachama wake wanapendelea sana kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ambavyo havikuwepo enzi hizo. Kupitia mitandao hiyo, vyombo hivyo huweza kuwahadaa vijana wengi kwa kueneza mafundisho ya kufurutu mipaka na ugaidi. Kwa mfano tu, katika mitandao ya kijamii ya makundi hayo ya Twitter, Facebook na Instagram, kumejaa filamu, picha na video za jinai za kutisha ambazo wanachama wake wamefanya dhidi ya Waislamu.

********************************************

Ndugu wasikilizaji kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh linaeneza propaganda zake kupitia lugha tofauti ambazo huenezwa katika maeneo yanayodhibitiwa na genge hilo. Kama ambavyo katika utekelezaji wa mradi huo, kundi hilo huwatumia wataalamu wenye uzoefu wa hali ya juu ambapo hata filamu, video na picha zinazotengezwa na watu hao huwa za kuvutia sana. Kuhusiana na suala hilo, jarida la kila wiki la Der Spiegel la  Ujerumani limefichua kuwa, mashirika ya Ulaya yanalidhaminia mahitaji ya intaneti kundi la Daesh kupitia mfumo wa satalaiti huko Iraq, Syria na kwengineko.

Wanamapambano wa Harakati ya Hizbullah wanaopambana na magaidi wa Kiwahabi

Ripoti hiyo inasema: “Katika maeneo yanayodhibitiwa na Daesh nchini Iraq na Syria, kundi hilo linatumia intaneti ya satalaiti ya nchi za Ulaya. Katika maeneo hayo huwekwa mamia ya vifaa vya kisasa vya intaneti kwa ajili ya kundi hilo ambapo hupatikana intaneti ya kasi ya juu kwa ajili ya kusahilisha uenezaji wa propaganda zake.” Mwisho wa kunukuu. Kadhalika jarida la Der Spiegel linayataja mashirika hayo yanayolidhaminia intaneti kundi la kigaidi la Daesh kuwa ni shirika la Uingereza la ‘Avanti Communications’ na shirika la Ufaransa la ‘Eutelsat.’Pia katika stratijia za kutumia vyombo vya habari za kundi la ukufurishaji la Daesh, genge hilo linafuatilia malengo mengine yaliyo nyuma ya pazia. Moja ya malengo hayo ni kujaribu kuonyesha ushindi wake bandia kwa kujiarifisha kwamba genge hilo halishindwi, suala ambalo lengo lake ni kudhofisha moyo wa kimapambano ya upande wa pili. Makundi ya ukufurishaji yanawatambua Waislamu wa madhehebu nyingine kuwa ni maadui na kwamba kupambana na Waislamu hao ni sawa na kupambana Wamagharibi au utawala haramu wa Israel.

Askari wa serikali halali ya Syria wanaopambana na magaidi

Ukweli ni kwamba, miongoni mwa kazi maalumu za makundi ya ukufurishaji kwa madola ya Magharibi ni kuzusha uadui katika ulimwengu wa Kiislamu, sambamba na kuwasahaulisha Waislamu adui yao asili yaani tawala za Wamagharibi na utawala haramu wa Israel.

****************************************

Wasomi na maulama wa nchi za Waislamu kutoka madhehebu yote, wana jukumu zito la kukabiliana na hatua na vitendo vya ukatili na jinai za makundi ya ukufurishaji na kigaidi ambavyo vinachafua sura halisi ya dini ya Uislamu. Hii ni kusema kuwa, vitendo vya makundi ya ukufurishaji haviishii tu kwenye dhehebu moja, bali vinalenga jamii ya Waislamu wote ambao sio wafuasi wa Uwahabi. Chuki dhidi ya Uislamu inayoshuhudiwa barani Ulaya na Marekani haiwatofautishi Waislamu, bali kinyume chake inawalenga kwa ujumla Waislamu wa kila dhehebu. Katika hali kama hiyo, ilitarajiwa kwamba, makundi mbalimbali ya iislamu yangeweka kando tofauti zilizopo na kuangalia kwanza mambo yanayowajumuisha pamoja Waislamu na kuyatumia mambo hayo kama fursa kwa ajili ya kukabiliana na propaganda za kuchafua sura halisi ya Uislamu. Kinyume chake tunaona kwua makundi ya Kiwahabi ndio kwanza yamejikita katika kuzusha tofauti na kuwakufurisha Waislamu wengine.

Moja ya jinai chungu za kundi la ukufurishaji la Daesh

Aidha miongoni mwa hatua nyingine za makundi ya ukufurishaji katika kuibua tofauti baina ya Waislamu, ni kueneza uongo mkubwa dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Hata hivyo shubuhati hizo zimekuwa zikijadiliwa na kutatuliwa na maulama na wasomi wa Kishia na Kisuni kupitia vikao tofauti vya maelewano na katika ngazi ya vyombo vya habari. Katika fremu hiyo Daesh na makundi mengine ya mfano wake yanawaonyesha walimwengu kwamba dini ya Uislamu ni dini ya mauaji, ukatili na uharibifu. Kama hiyo haitoshi, magaidi hao humuarifisha Mtume wa rehma, Muhammad (saw) katika sura ya kupenda vita, ukatili na umwagaji damu mkubwa. Kupitia propaganda hizo, magaidi hao wanahalalisha jinai zao na kuwahadaa Waislamu kutumia nguvu kwa ajili ya kufikia malengo yao. Hii ni katika hali ambayo kwa kupitia mipango maalumu iliyoratibiwa, vyombo vya Kimagharibi huviakisi vitendo vya makundi hayo ya Kiwahabi na kuvinasibisha kwa Mtume wa Uislamu (saw) kwa lengo la kuchafua kabisa dini ya Uislamu na kuituhumu kuwa ni dini ya kigaidi.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 30 makala haya inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

Tags