Apr 08, 2017 13:49 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika mfululizo wa vipindi hivi vinavyokosoa kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu na suna za Bwana Mtume (saw) makundi ya ukufurishaji yanayotekeleza jinai za kutisha dhidi ya Waislamu wengine hii ikiwa ni sehemu ya 28 ya mfululizo huo.

Katika vipindi viwili vivyopita tulizungumzia mwenendo wa makundi ya Kiwahabi yanayowakufurisha Waislamu wengine, yanavyowadhalilisha wanawake na kuwaona kama viumbe wasio na thamani yoyote.
Aidha tulikunukulieni fatwa za kustaajabisha na zisizokuwa na msingi wowote katika mafundisho ya dini ya Kiislamu za mamufti wa Kiwahabi katika kuhalalisha ufuska na uzinzi kwa kile mamufti hao walichokiita kuwa ni Jihadun-Nikaah. Kupitia fatwa hizo, makundi ya kigaidi na ukufurishaji hususan Daesh (ISIS) na Jab’hatu Nusra yaliingia katika vitendo vya kishetani kwa kuwachezea wanawake ambapo mbali na kukiuka misingi ya dini ya Uislamu, yalikiuka pia misingi ya ubinaadamu. Hata hivyo sambamba na madola ya Magharibi kuendelea kufumbia macho jinai hizo za makundi ya Daesh, Jab’hatu Nusra na mfano wa hayo, ndivyo ambavyo kunadhihiri malengo machafu yaliyo nyuma ya pazia ya kuanzishwa magenge hayo katika nchi za Waislamu. Lengo hilo si jingine ila ni kuchafua sura ya dini ya Uislamu inayolingania upendo na huruma kwa wanadamu wote.

Kinara wa Daesh

Itafahamika kuwa, kwa miaka kadhaa sasa Wamagharibi wamekuwa wakifanya njama za kila aina katika kujaribu kuchafua sura ya dini hii ya mbinguni bila mafanikio. Katika fremu hiyo ndipo madola hayo yakaanzisha mradi mpya wa makundi hayo ya kigaidi yenye fikra mgando na yanayotenda jinai za kutisha dhidi ya binaadamu na kisha kuvihusisha vitendo hivyo na dini ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla ili kwa njia hiyo yaweze kutoa pigo kwa dini hiyo.
Ndugu wasikilizaji mnafaa kufahamu kwamba, kudhihiri makundi ya kigaidi na ukufurishaji, kuliandaa fursa kubwa kwa Wamagharibi kwa ajili ya kuuangamiza Uislamu. Magaidi wa Kiwahabi kwa kutumia nara kama vile kuwaua maadui wa Mungu, yalianzisha mauaji makali dhidi ya watu wasio na hatia sambamba na kuwakata shingo watu hao. Wakati magaidi hao wakifanya jinai hizo za umati, kama kawaida hutoa takbira na hivyo kuzioanisha jinai hizo na dini ya Uislamu. Wakati mwingine huenezwa  katika mitandao ya kijamii mikanda ya video na picha za zinazoonyesha mandhari ya kutisha ya kuwakata watu vichwa huku nyuma yao kukiwa kumewekwa vitambaa vyenye aya na hadithi. Hakuna shaka kwamba, vitendo hivyo vinatekelezwa kwa malengo maalumu ya kuichafua dini ya  Uislamu, ambapo matokeo yake ni kuingiza katika fasihi ya kisiasa ya madola ya Magharibi, istilahi ya kuziambatanisha jinai  na ukatili wa magaidi pamoja na Uislamu, jambo ambalo halina ukweli wowote ndani yake. Kwa kuchunguza mienendo ya madola ya Magharibi na vyombo vya habari vya madola hayo katika kuuonyesha Uislamu kuwa hatari ndani ya kipindi cha miaka ya hivi karibuni, inatubainikia ni kwa kiasi gani madola hayo yanavyofanya njama chafu dhidi ya dini hii. Uthibitisho wa hilo ni propaganda zinazofanywa katika kuakisi jinai za makundi ya al-Qaidah, Taleban, Daesh, Jab’hatu Nusra, Boko Haram, ash-Shabab na mfano wa hayo.

Jinai za magaidi wa Kiwahabi (ISIS)

Kwa mfano tu wakati Wamagharibi na vyombo vyao wanapolitaja genge la kigaidi la Daesh, yanatumia istilahi ya ‘Dola la Kiislamu’ kama ambavyo pia huwataja wapiganaji wa kundi la ash-Shabab nk kwa jina la ‘wapiganaji wa Kiislamu wa ash-Shabab, Boko Haram nk’ suala ambalo linakusudia kuyaonyesha makundi hayo na wanachama wake kuwa ni wawakilishi wa Uislamu kisiasa na kiutawala. Hiyo ni sehemu ndogo ya propaganda chafu za kuuonyesha Uislamu kuwa wa hatari na wa kutisha.


**************************************


Ndugu wasikilizaji mnafaa kufahamu kwamba, madola ya Magharibi na vyombo vyao yanaeneza mawimbi mapana ya kipropaganda dhidi ya Uislamu kwa kuuarifisha kuwa ni iliyopitwa na wakati na hatari, katika hali ambayo kiuhalisia, Waislamu ndio wahanga wakubwa wa mashambulizi na ukatili wa makundi hayo kote duniani. Hii ni kusema kuwa, hadi leo kiwango na ukubwa wa vitendo vya kigaidi ambavyo vimewahi kutekelezwa na vinavyoendelea kushuhudiwa katika maeneo ya Waislamu, haviwezi kulinganishwa na matukio ya kigaidi yaliyotekelezwa katika nchi za Maghribi.

Wapiganaji wa Daesh

Ukweli ni kwamba walengwa nambari moja wa makundi ya Kiwahabi na ukufurishaji kama vile Daesh (ISIS) na mfano wake ni Waislamu wa Suni na Shia ambao wanapinga dhehebu la Uwahabi na kuiona mienendo yake kuwa inayokinzana na mafundisho ya Uislamu asili unaolingania uadilifu, amani, upendo na umoja duniani. Aidha mbali na makundi hayo kuchafua sura ya Uislamu, yanafuatilia malengo mengine, nayo ni kuibua fitina na tofauti baina ya madhehebu ya Kiislamu hususan kati ya Suni na Shia, lengo ambalo limekuwa likifiuatiliwa kwa muda mrefu katika siasa za madola yanayopenda kujitanua kama vile Marekani na waitifaki wake. Katika fremu hiyo, makundi hayo yanafanya njama kubwa katika kujaribu kuionyesha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ina asilimilia kubwa ya wafuasi wa madhehebu ya Shia kuwa ndio adui mkuu dhidi ya Waislamu.

Abu Musab al-Zarqawi, mwasisi wa kundi la Daesh (ISIS)

Kuhusiana na hilo Abu Musab al-Zarqawi, mwasisi wa kundi la Daesh (ISIS) anaizungumzia Iran kwa kusema: "Ushia si tu kwamba umetoka nje ya umma wa Kiislamu, bali ni dini ya kujiundia ambayo lengo lake la mwisho ni hatimaye Iran iweze kuwadhibiti Masuni na kuchukua uongozi wa Umma wa Kiislamu." Mwisho wa kunukuu. Katika propaganda hizo, kinara huyo wa zamani wa ugaidi na mfuasi wa Uwahabi, anajaribu kujinasibisha na Usuni ili kuwavutia Waislamu wa Kisuni duniani kumfuata, katika hali ambayo yeye mwenyewe hakuwa mfuasi wa dhehebu hilo. Lakini kama hiyo haitoshi, gaidi huyo mkufurishaji alidai kuwa, eti Iraq imetoka katika Uislamu asili na kuangukia mikononi mwa makafiri wa Shia. Hii ni katika hali ambayo kwa muda wote Iran ya Kiislamu imekuwa ikilingania umoja baina ya madhehebu na nchi tofauti za Waislamu. Mbali na hayo ni kwamba hadi sasa Iran, ni nchi muhimu sana duniani katika kupambana na makundi ya kigaidi yanayowakufurisha Waislamu wengine. Katika fremu hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ina mashahidi elfu 17 wa vitendo vya kigaidi na hivyo kuwa miongoni mwa nchi ambazo zina kiwango cha juu cha wahanga wa wimbi hilo hatari la ugaidi. Hata hivyo isisahulike kuwa, mchezo huo mchafu dhidi ya dini ya Kiislamu, unasimamiwa na madola ya Magharibi na ya kikoloni kupitia baadhi ya tawala za eneo la Mashariki ya Kati na kadhalika makundi ya Kiwahabi na ukufurishaji. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, kila upande unatekeleza nafasi yake ili kukamilisha njama hizo.


**********************************
Ndugu wasikilizaji radiamali na athari ya jinai za makundi ya kigaidi na ukufurishaji, inaonyesha kwamba makundi hayo kiuhalisia yanatekeleza siasa za nchi za Magharibi na madola mengine waitifaki wao katika eneo hili kutokana na uepo wa baadhi ya nyufa zilizojitokeza. Mikakati ya madola yaliyo nje ya eneo la Mashariki ya Kati ni kuibua machafuko na mapigano baina ya Waislamu na Waarabu kwa madhumuni ya kudhoofisha nguvu yao na hatimaye kuweza kuingilia kijeshi na kisiasa katika eneo la magharibi mwa Asia. Hii ni kwa kuwa madola hayo yanakusudia kuzigawa nchi za ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu na hivyo kuweza kuimarisha nafasi zao katika eneo kwa lengo la kuulinda utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Katika fremu madola ya ukoloni sambamba na kuanzisha tofauti kati ya Waislamu, au kueneza khofu na wasi wasi baina yao, yanajaribu pia kuzitenganisha nchi za Kiislamu na kuzifanya zisiwe na umoja baina yao.

Edward Snowden, Afisa wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA)

Nyaraka zilizofichuliwa na Edward Snowden, Afisa wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA)  zinaonyesha wazi kwamba, nchi za Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Uingereza ndizo zilizohusika katika kuanzishwa kwa kundi la kigaidi la Daesh. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, baada ya kundi hilo kuasisiwa, jukumu la kutoa uangalizi, mwongozo na kuwatibu wanachama wake wanaojeruhiwa na askari wa Iraq na Syria, likikabidhwa kwa utawala bandia wa Kizayuni wa Israel. Kuhusiana na suala hilo, Michel Chossudovsky, mtaalamu wa uchumi wa nchini Canada na mwasisi wa kituo cha uchunguzi wa masuala ya dunia, anazungumzia genge la Daesh katika Makala aliyoyaita 'Injinia wa uharibifu na mpasuko wa kisiasa nchini Iraq' kwa kusema: "Daesh ni nyenzo na njia kwa ajili ya umoja wa kijeshi wa Magharibi. Kwa ajili hiyo, wanachama wake wanajionyesha kama maadui wa Marekani na Wamagharibi, katika hali ambayo kwa mujibu wa nyaraka na shahidi zilizopo, kundi hilo limeanzishwa na Shirika la Ujasusi la Marekani CIA na Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni MOSSAD." Aidha Michel Chossudovsky anaendelea kwa kusema: "Hata mauaji yaliyofanywa na wanachama wa Daesh dhidi ya askari wa Marekani, yalitekelezwa kupitia lengo maalumu nalo ni kuipatia kisingizio Marekani na nchi nyingine za Kimagharibi, kuweza kuingilia kijeshi katika nchi za Kiislamu." Mwisho wa kunukuu. Kwa upande wake, Kevin Barrett, mtaalamu wa masuala ya dini ya Kiislamu na mchambuzi wa kisiasa wa nchini Marekani anaandika katika Makala aliyoyapa jina la 'Dola lisilo la Kiislamu, Ukhalifa wa Shetani' kwamba: "Jukumu la Daesh ni kueneza machafuko, vita na ukosefu wa usalama katika eneo la Mashariki ya Kati ili kuifungulia mlango Marekani kufanya uingiliaji kijeshi usio na mwisho katika eneo hilo." Mwisho wa kunukuu.
********************************
Katika hali hiyo Uwahabi nao kama msingi na chanzo cha fikra za makundi ya kigaidi na ukufurishaji, umekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha mpango huo kabambe. Kuhusiana na hilo maulama wa Kiwahabi sambamba na kutoa fatwa za ukufurishaji, wamekuwa pia wakiibua fitina za kimadhehebu baina ya Waislamu na hivyo kupandikiza mbegu ya farqa na chuki katika ulimwengu wa Kiislamu. Kupitia fatwa hizo, maulama hao wa Kiwahabi huwa wanawachochea watu wenye upeo mdogo wa kielimu kwa ajili ya kujiunga na makundi ya kigaidi katika kuwaua Waislamu wa Kisuni na Kishia.

Magaidi wa Kiwahabi wa Jab'hatu Nusra

Makundi ya ukufurishaji hususan Daesh (ISIS), Jab'hatu Nusra, Boko Haram, ash-Shabab na mfano wake, yanatekeleza jinai na mauaji kwa kufuata fatwa hizo bandia. Kwa kushirikiana na madola waungaji mkono wao katika eno, magaidi hao wanakusudia kuenea fikra za mauaji baina ya Waislamu na kuugawa umma wa Kiislamu. Hii ni katika hali ambayo Qur'an Tukufu na viongozi wa awali wa Uislamu, wamewalingania Waislamu kwenye udugu, urafiki na kuoneana huruma baina yao. Aidha kitabu hicho cha Allah kinawataka Waislamu kujiepusha na kila aina ya tofauti baina yake. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mwenyezi Mungu akawataja Waislamu kama ndugu kwa kusema: " Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe." Surat Hujaraat aya ya 10.
Ndugu wasikilizaji sehemu ya 28 ya makala haya inafikia tamati hapa kwa juma hili. Msikose kutegea sikio sehemu ya 23 wiki ijayo. Mimi ni Sudi Jafar na hadi wakati huo, kwaherini.

 

 

 

Tags