Mfululizo wa vipindi vya vinavyokosoa mienendo ya magenge potofu ya kigaidi na ukufurishaji/ sehemu ya 23 pamoja na sauti
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 23 ya makala yanayokosoa kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na suna za Bwana Mtume (sawa) mienendo ya makundi ya ukufurishaji yanayotenda jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu wengine.
Katika kipindi kilichopita tulizungumzia namna ambavyo sira ya Mtume wa Uislamu na Qur'ani Tukufu ilivyojengeka juu ya msingi wa huruma na upole huku ikiwataka wafuasi wa Nabii huyo wa Allah kushikamana na mafundisho hayo adhimu katika maisha yao ya kila siku. Hata hivyo na kwa bahati mbaya, makundi ya kigaidi na ukufurishaji kwa kwenda kinyume na mafundisho ya dini hii, yamekuwa yakitekeleza jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya watu wengine suala ambalo limechafua sura ya Uislamu katika fikra za walimwengu.
Hii ni kwa kuwa fikra, lugha na mienendo ya makundi ya ukufurishaji imejengeka juu ya kuwakufurisha tu watu wengine na kufanya jinai na ukatili dhidi yao. Makundi hayo kwa kufuata mafundisho ghalati yaliyo kinyume na dini ya Uislamu yamegandisha fikra zao kwa kuamini akili na misimamo yao pekee ambapo pia yanawaona watu wenye fikra tofauti na zao kuwa wasiofaa na wanaotakiwa kufutwa haraka kwenye uso wa dunia. Aidha makundi ya ukufurishaji mbali na kuhusika na mauaji ya umati na uporaji mali na vitu vya thamani vya watu wengine kwa kisingizio cha kupambana na ushirikina, yanahusika pia na uharibifu na kuyavunjia heshima makaburi, misikiti na turathi za kihistoria katika nchi mbalimbali za Kiislamu kama vile Iraq, Syria, Tunisia, Libya Yemen na kwengineko duniani. Hata kama kidhahiri uharibifu huo unafanyika kwa kisingizio cha kufuta athari za ushirikina, lakini kiuhalisia, hujuma hizo zinatekelezwa kwa lengo la kupora na kuharibu turathi za kiutamaduni za mataifa ya Kiislamu.
Kama ilivyoshuhudiwa baada ya hatua za uharibifu zilizofanywa na wanachama wa kundi la Daesh (ISIS) za kubomoa athari nyingi za historia huko Iraq na Syria, baadaye magaidi hao wa Kisalafi waliziuza turathi hizo za kihistoria katika nchi za Magharibi na maeneo ya maonyesho ya kihistoria duniani. Matukio hayo yanadhihirisha kwamba makundi hayo ya kigaidi kwa kutumia nara za kidini, yanafuatilia pia malengo mengine yaliyo nyuma ya pazia. Hata hivyo isisahulike kuwa, uharibifu wa makundi hayo ya ukufurishaji katika kubomoa majengo ya kihistoria na kidini, ni wenye hatua nyingi. Hii ni kusema kuwa utambulisho wa tamaduni ni moja ya mambo muhimu sana kwa imani na historia ya kila mtu, ambapo kwa kupitia utamadui huo huweza kuleta mawasiliano baina ya wanadamu. Makundi ya Kisalafi na kigaidi kwa kuzingatia kuwa yanakabiliwa na changamoto nyingi zinazotokana na itikadi na usalama, ndio maana yakachukua hatua ya kubomoa na kuharibu turathi hizo za Kiislamu.
****************************************
Ndugu wasikilizaji kama tulivyosema, maeneo ya kidini na kihistoria ni yenye taathira nyingi katika kuwaunganisha Waislamu wote duniani. Moja ya dhihirisho la mandhari ya Kiislamu ni majengo ya kidini ambayo hata hivyo na kwa bahati mbaya makundi ya kigaidi yanatumia ukatili wa kutisha mbali na mafundisho ya dini katika kuyaharibu na kudai kuwa majengo hayo ni nembo na alama ya ushirikina.
Hii ni kusema kuwa, kwa akali maeneo matakatifu yanayopata 150 yamebomolewa na kuharibiwa kabisa katika nchi nne za Iraq, Syria, Tunisia na Libya. Sehemu ya jinai hizo ni pamoja na kubomoa misikiti, makaburi ya mawalii ya Mwenyezi Mungu, kufukua makaburi ya watu wa mwanzo wa Uislamu na kuharibu maeneo walipozikwa maimamu na shakhsia mbalimbali wa kielimu na kidini. Uharibifu huo nchini Syria, ulijiri baada ya kuibuka wimbi la uasi, huku nchini Tunisia na Libya, ukijiri baada ya kuangushwa tawala za kidikteta za mataifa hayo. Ama huko Iraq, uharibifu huo ulianza tangu mwaka 2004, ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuondolewa na Marekani utawala wa dikteta Saddam Hussein wa nchi hiyo.
Mikoa ya kaskazini mwa nchi hiyo ilishuhudia wimbi kubwa la uharibifu baada ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh kudhibiti maeneo hayo hapo mwaka 2014 ambapo katika kipindi hicho makaburi na athari nyingi za kihistoria ziliporwa na kuharibiwa kabisa. Katika kutekeleza jinai hiyo ya uharibifu wa maeneo ya kidini, kundi hilo liliunda kitengo kilichopewa jina la 'Kikosi cha Kusawazisha Makaburi na Dharih.' Wanachama wa kitengo hicho walikuwa 300 ambapo kwa kutumia magari na vifaa vizito walianza kubomoa na kuharibu maeneo ya kidini ya mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa (Nineveh) Iraq na Syria. Makaburi ya watu wema na Mitume wa Mwenyezi Mungu kama vile, Nabii Yunus, Jarjis na Shith, mtoto wa Nabii Adam (as) yaliharibiwa kabisa. Kaburi la Nabii Yunus (as) lipo umbali wa kilometa 375 kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad, huku historia ya kujengwa kwake ikirudi nyuma hadi mwaka 138 Hijiria.
Pamoja na umuhimu huo wanachama wa kundi hilo la Kiwahabi la Daesh (ISIS) walilivunja na kuliharibu kabisa kaburi hilo. Kadhalika matakfiri hao wanaoungwa mkono na Marekani, Israel na Saudi Arabia kwa kutumia tani 30 za mada za miripuko, walibomoa kwa kuripua jengo la kihistoria ambalo linakadiriwa kuwa na umri wa miaka 2000 la Palmyra huko Syria, ambalo ni moja ya majengo muhimu sana yaliyosajiliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Kitendo ambacho kiligusa nyoyo za walio wengi duniani.
****************************************
Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni Makala yanayokosoa kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na Suna za Mtume Muhammad (saw) makundi ya ukufurishaji hii ikiwa ni sehemu ya 23 ya mfululizo huo.
Aidha magaidi hao wa Kisalafi wasio na utu wowote mioyoni mwao na kwa mujibu wa video waliyoituma katika mitandao ya kijamii, walivamia eneo la kumbukumbu la mji wa Mosul, Iraq na kuharibu athari na masanamu mengi ya kale na ya kihistoria ya mji huo. Kadhalika magaidi hao waliharibu kabisa mji wa kihistoria wa Nimrod ambao unakumbushia historia ya utawala wa Ashuri wa maelfu ya miaka iliyopita. Katika jinai hiyo magaidi hao walitumia mabuldoza na mada kadhaa za miripuko na kuuharibu kabisa mji huo.
Ndugu wasikilizaji, ni vyema mfahamu kwamba, uharibifu wa wanachama wa makundi hayo yanayotekeleza ajenda maalumu za makafiri kwa kutumia nara ya Uislamu, hauishii tu kwenye athari za kihistoria na kidini, bali unalenga moja kwa moja utamaduni na utambulisho wa kihistoria wa dini ya Kiislamu kwa ujumla. Hii ni kusema kuwa, vitendo hivyo vya makundi ya ukufurishaji moja kwa moja vinatekelezwa kupitia ajenda maalumu za maadui wa Uislamu wa Magharibi katika kuangamiza utambulisho wa kale na wa kihistoria wa dini tukufu ya Kiislamu. Ndugu wasikilizaji mtakubaliana nami kwamba, moja ya vyanzo vyenye taathira juu ya utamaduni wa mwanadamu na ambavyo vinadumisha kumbukumbu ya vizazi na vizazi, ni maeneo na majengo ya kihistoria ambayo yanawasilisha utambulisho wa jamii ya watu hao. Kwa kuzingatia kuwa maeneo hayo yanabeba utambulisho wa zamani wa mataifa na tamaduni tofauti, ndio maana yakawa na umuhimu mkubwa kwa kila kaumu na taifa husika. Mbali na hayo ni kwamba maeneo hayo yana hadhi maalumu na ya kipekee kiasi kwamba kila mtu anayefika mahala hapo huweza kushuhudia mambo ya thamani ya watu wa zamani na hivyo kuvuta hisia za watu hao waliotangulia kutokana na yale anayoyaona wakati huo.
Anapokuwa maeneo hayo yanayobeba kumbukumbu na utambulisho wa dini ya Kiislamu, umuhimimu wake huzidi mara dufu kutokana na nafasi yake chanya ya kuwaunganisha Waislamu. Hasa kwa kuwa maeneo hayo yanawakumbusha Waislamu shakhsia wakubwa wa zamani kama vile Mitume, Ahlu Bayti wa Mtume (as) na wafuasi wao ambao kimsingi ndio chimbuko, asili na utambulisho wa dini hii ya mbinguni.
***************************************
Katika hilo tunaweza kuashiria maeneo yenye Baraka ya Saudia ambayo huweza kuwakusanya Waislamu wa maeneo mbalimbali ya dunia katika msimu wa ibada ya Hijjah kwenda kuyazuru maeneo hayo. Utukufu wa maeneo hayo ya kihistoria, huweza kumsukuma mtu kushiriki ibada ya Hijjah kwa lengo la kushuhudia vyanzo vya dini ya Uislamu, kama ambavyo pia yanaweza kumfanya kufahamu chanzo cha historia ya dini yake. Ni kwa msingi huo ndio maana maeneo hayo ya kihistoria yakawa na umuhimu wa kipekee katika dini ya Kiislamu. Kupitia maeneo hayo mtu huweza kuwatambua viongozi wa dini kwa namna bora zaidi kuliko mtu ambaye yupo mbali na sehemu hizo. Ushahidi unaonyesha namna ambavyo maeneo hayo yalivyo na nafasi muhimu katika dini kiasi ambacho hata kufanyia ibada mahala hapo huwa na ubora zaidi. Kuhusiana na hilo Imam Sajjad (as) mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume (saw) alimwambia Shabali mmoja wa wafuasi wake kwa kusema kama ninavyomnukuu: "Ewe Shabali! Wakati ulipokuwa nyuma ya kisimamo cha Nabii Ibrahim, ukasali na kutufu, je, ulinuia kama unataka kusali sala ya Ibrahim?." mwisho wa kunukuu.
Riwaya hiyo pamoja na mambo mengine inaonyesha namna ambavyo Imam Sajjad alimuelekeza Shabali juu ya utamaduni wa kumpwekesha Mungu, ambapo anakumbushia juu ya eneo la kisimamo cha Nabii Ibrahim na ulazima wa kuzingatia matukufu ya kuwepo eneo hilo lililoasisiwa na Nabii huyo wa Allah yaani Nabii Ibrahim (as). Hata hivyo, wakati mjukuu huyo wa Mtume akisisitizia umuhimu wa kuenziwa maeneo hayo ya kihistoria, kwa upande wake makundi ya Kiwahabi na kitakfiri sanjari na kutekeleza uharibifu dhidi ya majengo ya kihistoria ya dini ya Kiislamu, yanayatambua maeneo hayo kuwa ya ushirikina ambayo hayafai kuachwa kwenye uso wa dunia. Kwa hakika vitendo hivyo vinaadaa mazingira ya kuwatenganisha Waislamu na vyanzo vyao vya kihistoria, ambavyo vinawaunganisha pamoja Waislamu wote wa dunia.
Hata hivyo wakati makundi hayo ya Kisalafi na Kiwahabi yakiyataja maeneo hayo kuwa nembo ya ushirikina, tunaona Qur'ani Tukufu ikiyaashiria na kuyataja kwa wema kwa majina. Kwa mfano maneno ya al-Kaabah na 'Maqamu Ismail' Kisimamo cha Islamail ni sehemu ya majina yaliyotajwa na kitabu hicho cha Allah. Hata hivyo suala la msingi ni kwamba, uharibifu mkubwa wa maeneo ya kidini na kihistoria, umetekelezwa katika ardhi za Saudia ambazo ndipo iliyoko hiyo al-Kaaba. Mawahabi na wakuhurishaji hao wanatekeleza uharibifu dhidi ya maeneo hayo ya kidini ya karne nyingi kwa kisingizio cha kupambana na ushirikina. Moja ya maeneo hayo yaliyoharibiwa ni makaburi ya eneo la Baqii mjini Madina. Eneo ambalo walizikwa ndani yake watoto, wajukuu na masahaba wa Mtukufu Mtume Muhammad (saw).
Ndugu wasikilizaji sehemu ya 23 ya makala haya inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./