Feb 10, 2017 02:43 UTC
  • Ijumaa, Februari 10, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 12 Jamadil Awawal 1438 Hijria sawa na tarehe 10 Februari, 2017

Katika siku kama hii ya leo miaka 38 iliyopita Iran ilikuwa katika siku ya kihistoria itakayokumbukwa siku zote. Siku hiyo wananchi waliokuwa wakipiga takbira na kutoa nara za kimapinduzi chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini walihitimisha kipindi cha giza totoro katika historia ya Iran kwa kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta wa Shah Pahlavi. Wananchi wanamapinduzi wa Iran, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee na watu wa matabaka yote walisimama kidete wakipambana na mizinga na vifaru vya jeshi la Shah na kujisabilia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran yalienea nchini kote huku wafuasi wa Imam Ruhullah Khomeini wakiwa katika juhudi za kumaliza kabisa mabaki ya utawala wa kidhalimu wa kifalme.

Siku kama ya leo miaka  67 iliyopita yaani tarehe 10 Februari mwaka 1950, Joseph Mc Carthy Seneta wa chama cha Republican cha nchini Marekani aliwasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi 205 wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo akiwatuhumu kuunga mkono ukomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Hatua hiyo ilipelekea kuanza kwa kile kilichojulikana kama "McCarthyism" huko nchini Marekani, ambapo kwa mujibu wake wanafikra, wataalamu na viongozi mbalimbali wa Marekani walifuatiliwa nyendo zao na kusakwa baada ya kutuhumiwa kuwa na mitazamo na fikra za Kikomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Kamisheni ya McCarthyism ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa, iliweza kuwafuta kazi karibu watumishi wa serikali wapatao 2000 huku idadi kubwa ya wataalamu na wasomi wakiswekwa jela kwa tuhuma zisizokuwa na msingi.

Joseph McCarthy

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, tawala za waitifaki na zile zilizokuwa zikihasimiana katika Vita vya Pili vya Dunia zilisaini makubaliano ya amani. Katika siku hiyo, Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa zilisaini makubaliano ya amani na nchi zilizoshindwa katika vita hivyo yaani Italia, Finland, Poland, Hungary, Romania na Bulgaria, na kwa utaratibu huo nchi sita hizo kwa mara nyingine tena zikajipatia uhuru wake.

Makubaliano ya amani kati ya tawala za waitifaki na mahasimu wao

Siku kama ya leo miaka 485 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu Ibn Tulun Dimashqi, aliyekuwa faqihi, mwanafasihi na mwanahistoria huko mjini Damascus, Syria. Ibn Tulun alizaliwa mwaka 880 Hijiria mjini Damascus na katika umri wake wote alifanya jitihada kubwa za utafiti, kufundisha na kuandika vitabu vya taaluma mbalimbali. Ibn Tulun Dimashqi ameandika vitabu vingi vya thamani kuhusiana na historia ya Kiislamu na pia katika uwanja wa tafsiri ya Qur'ani Tukufu, hadithi, lugha, tiba na irfani. Kitabu cha 'as-Safiinatu al-Tuluuniyyah' ni miongoni mwa athari za mwanazuoni huyo.

ابن طولون دمشقی

 

Tags