Mar 09, 2017 13:46 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika mfululizo wa vipindi hivi vinavyokosoa kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu na suna za Bwana Mtume (saw) makundi ya ukufurishaji yanayotekeleza jinai za kutisha dhidi ya Waislamu wengine hii ikiwa ni sehemu ya 24 ya mfululizo huo.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia baadhi ya hatua za uharibifu za makundi ya ukufurishaji na kigaidi katika kuharibu maeneo ya kidini duniani. Tukasema kuwa maeneo ya kidini hayawasilishi tu thamani za kidini, bali yanabeba utambulisho wa kihistoria wa taifa na wafuasi wote wa dini ya Uislamu kwa ujumla. Makundi ya ukufurishaji sambamba na kuharibu majengo ya kihistoria ya dini ya Kiislamu, yanakusudia kuibua mjadala juu ya utambulisho wa dini ya Kiislamu. Vitendo vya wafuasi wa makundi hayo mbali na kwamba vina lengo la kufuta kila alama ya kihistoria inayohusiana na ulimwengu wa Kiislamu, vinakusudia pia kukinyima kizazi kipya utambulisho wake wa kidini hususan kwa Waislamu na hivyo magaidi hao wawe wametimiza ajenda za maadui wa Uislamu katika uwanja huo. Hii ni katika hali ambayo Qur’ani Tukufu imezungumzia umuhimu wa kuenziwa maeneo ya kidini ambayo makundi ya kigaidi kwa kufuata mafundisho ghalati ya Uwahabi, yamekuwa yakiyaharibu kila siku.

Abubakar al-Baghdadi alipohudhuria kikao cha siri na senata wa Marekani pamoja na wapinzani wa Syria

Kwa hakika uharibifu unaofanywa na magenge hayo ya kigaidi na Kisalafi ni wenye kukinzana kikamilifu na aya za Qur’ani na suna za Bwana Mtume Muhammad (saw). Kwa mfano tu katika aya ya 42 ya Surat Rum, Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake kwamba: “Sema: Safirini duniani muangalie ulikuwaje mwisho wa waliotangulia. Wengi wao walikuwa washirikina.” Mwisho wa kunukuu. Kadhalika aya za 51 na 52 za Surat Naml zinasisitizia umuhimu wa kuenziwa turathi za kihistoria kwa kusema: “Basi angalia ulivyokuwa mwisho wa mipango yao, ya kwamba tuliwaangamiza wao pamoja na watu wao wote. Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyodhulumu. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara kwa watu wanaojua.” Mwisho wa aya. Katika aya hizo Mwezi Mungu anawataka Waislamu kuzuru maeneo ya watu waliopita ili kwa njia hiyo waweze kupata ibra ya watu hao wa kale. Katika aya hizo kumetumiwa lafudhi ya amri inayosema “Safarini duniani” na “Basi angalia ulivyo kuwa mwisho wa mipango yao” suala ambalo linathibitisha umuhimu wa kadhia hiyo, kwani itakuwa si busara kuwaamrisha wanadamu kutembelea maeneo ambayo tayari yameharibiwa na kusambaratishwa, au maeneo ambayo ni haramu kutembelewa lau kama yangeharamishwa. Aidha aya hizo zinatupilia mbali nadharia potofu za wanachama wa kigaidi wanaofuata mienendo ya Uwahabi katika kuharibu turathi za dini ya Kiislamu.

*************************************

Lengo la Qur’ani Tukufu ni kuifanya fikra ya mtu isiishie kwenye vitu vilivyomzunguka maishani mwake tu, bali upeo wa mtazamo wake unatakiwa upanuke na kuangalia hata maisha ya watu wa zamani waliopita ambapo kwa namna hiyo ataweza kujua mambo mengi ambayo alikuwa hayajui. Kwa mtazamo wa Uislamu, historia ni moja ya vyanzo vya maarifa na ufahamu kwa mwanadamu, kwani kwa kushuhudia athari za watu wa zamani na kuchunguza maisha na matukio ya watu hao, anaweza kuainisha mustakbali wake wa baadaye. Hivyo kitendo cha Qur’ani Tukufu kuwataka wanadamu kufanya safari na kuangalia historia za watu wa kale, kina sisitiza ulazima wa kuhifadhiwa maeneo hayo ya kihistoria ili wanadamu waweze kujifunza mengi kutokana na turathi hizo. Na hii haina maana ya kufuatilia historia ya watu hao wa zamani kupitia vitabu vya historia pekee. Kadhalika lengo la Qur’ani katika kuhifadhiwa turathi hizo za kihistoria ni kwa ajili ya maslahi ya vizazi vya sasa na vya baadaye. Kwa msingi huo, kitendo cha kuharibu athari na tamaduni za watu wa zamani kukiwemo kubomoa majengo ya kihistoria kunakofanywa na makundi ya Uwahabi na ukufurishaji, hakina dalili yoyote miongoni mwa mafundisho asili ya dini ya Uislamu. Kwa mfano tu aya za 90 na 92 za Surat Yunus zinaelezea mwisho wa mapambano yaliyojiri baina ya Nabii Mussa (as), Wana wa Israel na Firaun. Katika aya hizo Qur’ani inasimulia kwamba Firaun na jeshi lake aliwafuata Wana wa Israel hadi kwenye bahari ambapo Nabii Mussa kwa amri ya Mwenyezi Mungu aliweza kuwavusha watu wake na kuwaokoa.

Magaidi hao wakufurishaji wakiwaua kwa kuwasulubu Waislamu wa madhehebu ya Kisuni

Hata hivyo Firaun aliwafuata Bani Israel kupitia njia ile waliyoipitia na ghafla mawimbi ya maji ambayo yalikuwa yamesimama pande mbili yakakutana na hivyo ikawa sababu ya Firaun na jeshi lake kuangamia baharini. Qur’ani inasema: “Tukawavusha bahari Wana wa Israili, na Firauni na askari wake wakawafuatia kwa dhulma na uadui. Hata Firauni alipo kuwa anataka kuzama akasema: Naamini kuwa hapana mungu ila yule waliye mwamini Wana wa Israil, na mimi ni miongoni mwa walionyenyekea!. Ala! Sasa? Na hali uliasi kabla yake na ukawa miongoni mwa mafisadi!. Basi leo, tutakuokoa kwa mwili wako, ili uwe Ishara kwa ajili ya (watu) walio nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na Ishara zetu.” Mwisho wa kunukuu. Kutokana na aya hiyo mwili wa Firaun ukaopolewa bila uhai na hadi leo mwili huo umewekwa katika makumbusho nchini Misri ambapo watu mbalimbali hufika nchini humo na kuweza kushuhudia mwili wa taghuti huyo. Kama ambavyo Mwenyezi Mungu alimueleza Firaun kwamba: “Basi leo, tutauokoa mwili wako, ili uwe Ishara kwa ajili ya watu wa baada yako,” yaani kwamba athari ya mwili wake iwe ishara na ibra kwa watu wa baadaye, hivyo mwili huo unatakiwa uendelee kuhifadhiwa ili watu wa vizazi vya baadaye washuhudie hatma ya dhalimu huyo. Kwa imani ya makundi ya kigaidi na Kiwahabi mwili huo wa Firaun unapaswa kuripuliwa kwani ni alama ya ushirikina. Hii ni katika hali ambayo kupitia aya ya 92 ya Surat Yunus Mwenyezi Mungu alikusudia mwili wa taghuti  huyo uopolewe na uwe ibra kwa vizazi vya baadaye na hivyo unatakiwa kutunzwa na kuhifadhiwa kwa gharama yoyote ile.

*******************************************

Kama kwanza ndio unafungua redio yako kipindi kilicho hewani ni makala yanayokosoa kwa mujibu wa aya na hadithi makundi ya kigaidi na ukufurishaji, hii ikiwa ni sehemu ya 24 ya mfululizo huo. Ndugu wasikilizaji katika historia yote ya Mtume Muhammad (saw) hakukuwahi kuripotiwa kujiri uharibifu wowote wa maeneo ya kihistoria yasiyo ya kidini kama vile, kasri, majumba ya zamani, majengo na athari za dini nyingine za mbinguni kama vile makanisa. Mbali na hayo ni kwamba Mtukufu Mtume hakuwahi kutoa amri ya kuharibiwa maeneo kama vile majengo ya kuhifadhia masanamu yaliyokuwepo huko Yemen na maeneo mengine ya Kiarabu kama vile Syria. Kwani maeneo hayo yalikuwa yakihesabiwa na watu wake kuwa yenye utukufu, na hasa kwa kuzingatia kuwa watu hao hawakuwa na mahala pengine ghairi ya maeneo hayo. Kwa msingi huo ni suala la kusikitisha mno kwa makundi ya ukufurishaji na Kiwahabi kuharibu maeneo ya kihistoria yenye umri wa maelfu ya miaka hata kabla ya ujio wa Nabii Muhammad ambapo  Mtume huyo mwenyewe (saw) hakuamuru kubomolewa maeneo hayo ambayo yana mchango mkubwa katika historia ya mwanadamu. Amri ya Mtume katika kuharibu maeneo kama hayo ilikuwa na ukomo maalumu kama ambavyo pia katika maisha yake kulishuhudiwa maeneo yaliyokuwa na utamaduni wa kuabudiwa masanamu. Kubakishwa majengo ya kaumu ya Thamud hata katika kipindi chote cha uhai wa Nabii huyo wa Allah (saw), kunabainisha kwamba mtukufu huyo hakuwa na nia ya kutekeleza uharibifu wa athari na tamaduni za watu wa zamani waliomtangulia ambayo Mwenyezi Mungu amewataka wanadamu kuyatumia maeneo hayo kupata ibra na mazingatio. Kuhusiana na suala hilo imepokewa riwaya kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) inayowataka wafuasi wake kuyatumia maeneo hayo katika kupata ishara na mazingatio. Inaelezwa kuwa: "Wakati Mtume alipokuwa katika njia kuelekea vita vya Tabuk mwaka wa tisa Hijiria, alifika eneo lenye jiwe ambalo lina athari ya watu wa kaumu ya Thamud. Kisha Mtume akatazama jiwe lile na akawambia masahaba zake: “Msiingie nyumba za watu ambao walijidhulumu nafsi zao ispokuwa mlie.” Mwisho wa kunukuu. Katika riwaya hiyo kama mlivyoona Mtume Mtukufu hakuwambia masahaba wabomoe athari zile za kihistoria za watu wa Thamud bali aliwataka walie kwa kupata ibra juu ya watu hao wa kale.

**********************************

Moja ya maeneo ya kihistoria ambayo yamekuwa yakikumbwa sana na uharibifu wa makundi ya kigaidi na Kiwahabi kama vile Daesh ni makaburi ya watu wa zamani. Hii ni katika hali ambayo katika vyanzo na vitabu vya Ahlus-Sunnah kuna hadithi nyingi zinazothibitisha kuwa suna, suala la kuyazuru makaburi hayo. Aidha kufanya ziara na kuwazuru shakhsia wakubwa na wenye historia chanya, kuwakumbuka na kuwaenzi huacha kumbukumbu nzuri katika fikra za mwanadamu na kumuongoza kwenye njia ya kupenda uadilifu na ukamilifu wa kimaanawi. Kwa kushuhudia makaburi hayo mwanadamu hukumbuka mwisho wa uhai wake na hivyo kuikumbuka Akhera. Imepokelewa katika kitabu cha Sunan Ibn Majah hadithi kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) inayosema: “Tembeleeni makaburi kwani yatakukumbusheni Akhera.” Mwisho wa kunukuu. Katika riwaya hiyo Mtukufu Mtume anausia juu ya umuhimu wa kuyazuru makaburi kutokana na taathira yake chanya katika kumkumbusha mtu juu ya hatima ya maisha ya ulimwengu wa Akhera, kinyume kabisa na makundi ya kigaidi ambayo yanayabomoa na kuyaharibu makabiri hayo bila huruma yoyote mioyoni mwao.

Na kufikia hapa ndio tunafikia tamati sehemu ya 24 ya mfululizo wa vipindi hivi. Mimi ni Sudi Jafari kwaherini……./ 

 

 

Tags