Mar 27, 2017 04:43 UTC
  • Jumatatu 27 Machi, 2017

Lei ni Jumatatu tarehe 28 Jamadithani 1438 Hijria sawa na 27 Machi, 2017.

Miaka 848 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia katika mji mkuu wa Misri, Cairo Abul Qassim Shatibi, alimu na qarii mashuhuri wa Qur'ani ambaye ni mashuhuri kwa lakabu ya Imam al-Qurra. Alizaliwa mwaka 538 Hijria ambapo mbali na elimu ya usomaji Qur'ani, alikuwa amebobea pia katika elimu ya tajwidi, Tafsiri ya Qur'ani, hadithi, nahau, lugha na elimu  nyingine. Abul Qassim Shatibi ameacha athari nyingine katika nyuga mbalimbali ambapo Qasidat al-Shatibiyah ni moja tu ya vitabu vyake mashuhuri, kitabu ambacho kinazungumzia masuala jumla yanayohusiana na elimu ya tajwidi na kitabu hiki kimechapishwa mara chungu nzima katika nchi mbalimbali. 

ابوالقاسم شاطبی

Siku kama ya leo miaka 520 iliyopita, alizaliwa Hans Holbein the Younger, mchoraji wa Ujerumani katika familia ya kisanii. Younger alijifundisha sanaa ya uchoraji kutoka kwa baba yake aliyekuwa mashuhuri katika uwanja huo. Baada ya hapo alielekea nchini Uswisi na kuvisaidia vyombo vya usalama katika shughuli ya kuonyesha taswira za watu hususan wahalifu. Baada ya muda, alielekea Uingereza na kuendelea na kazi yake hiyo na kupata umaarufu mkubwa. Hans Holbein the Younger alifariki dunia mwaka 1543.

Hans Holbein the Younger

Siku kama ya leo miaka 172 iliyopita alizaliwa Wilhem Conrad Rontgen, mwanafizikia na mwanasayansi maarufu wa Ujerumani. Mwaka 1845 aligundua miale ya X na mwaka 1901 akatunukiwa tuzo ya Nobel kwa kufanikiwa kugundua miale hiyo. Kwa kuwa hakutambua miale aliyoigundua, Rontgen aliamua kuipa jina la X. Miale hiyo hupenya kwa urahisi katika mwili wa mwanadamu na kwa sababu hiyo ni njia nzuri zaidi ya kuchukua taswira ya viungo au picha ya X-ray inayotumiwa kujua sehemu za ndani ya mwili zilizodhurika au kuvunjika.

Wilhem Conrad Rontgen

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita inayosadifiana na 27 Machi 1948, serikali ya Ufaransa iliasisi jumuiya iliyozishirikisha Ufaransa na nchi waitifaki pamoja na nchi ambazo zilikuwa makoloni ya nchi hiyo. Muungano wa nchi hizo unafanana na ule wa Jumuiya ya Madola, ambao unazijumuisha nchi zilizowahi kutawaliwa na Uingereza. Kuundwa kwa muungano huo ulikuwa mwanzo wa kuandaliwa mazingira ya kuundwa Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa 'Francophone' ambayo iliasisiwa mwaka 1970. Wanachama wengi wa jumuiya hiyo wanatoka barani Afrika.

Wawakilishi wa nchi za jumuiya ya Francophone

Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Javier Perez de Cuellar alitoa taarifa akilaani hatua ya utawala wa Iraq kutumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Baada ya kupita muda Iraq ikitumia silaha hizo dhidi ya Iran na kimya cha Baraza la Usalama, Javier Perez de Cuellar aliamua kutoa taarifa na kulaani kitendo hicho cha Iraq. Katika mojawapo ya taarifa zake iliyotolewa tarehe 28 Machi mwaka 1988 de Cuéllar ilisema ana ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa serikali ya Saddam Hussein inatumia silaha za kemikali dhidi ya watu wa Iran na Iraq, suala ambalo limesababisha maafa makubwa.

avier Perez de Cuellar

 

Tags