Apr 10, 2017 11:46 UTC

Sura ya Luqman, aya ya 20-24 (Darsa ya 735)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 735 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 31 ya Luqman. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 20 ambayo inasema:

أَلَمْ تَرَوْا أَنَّ اللَّهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ وَأَسْبَغَ عَلَيْكُمْ نِعَمَهُ ظَاهِرَةً وَبَاطِنَةً وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَلا هُدًى وَلا كِتَابٍ مُّنِيرٍ

Je hamwoni kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na akakukamilishieni neema zake, za dhahiri na za siri? Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.

Katika darsa iliyopita tulihatimisha kuzungumzia aya zinazodondoa nasaha na mawaidha ya Luqman kwa mwanawe kuhusu masuala ya kiitikadi, kiakhlaqi na kijamii. Aya hii tuliyosoma inarejea tena kwenye maudhui iliyotajwa katika aya tulizosoma kabla ya mawaidha ya Luqman, ambayo ni kuhusu elimu ya kumtambua Mwenyezi Mungu na kuwahutubu wanadamu wote kwamba: Mwenyezi Mungu ameziumba na kuziweka mbingu na ardhi kwa namna ambayo daima ziwe zinakuhudumieni na kukutumikieni nyinyi. Maumbo ya kimaumbile kama jua na mwezi angani, na mzunguko wa sayari ya dunia kulizunguka jua na kujizunguka yenyewe, vimewezesha na kuwepesisha mazingira kwa ajili ya uhai na maisha yenu nyinyi wanadamu. Bahari, maziwa na mito, anuai za madini ya chini na ya juu ya ardhi, aina mbalimbali za wanyama wa majini na wa nchi kavu, anuai za miti na mimea na mazao ya kilimo, vyote hivyo viko kwa ajili ya kukuhudumieni nyinyi wanadamu. Baadhi yao mumetiishiwa nyinyi moja kwa moja na baadhi ya vyengine vinafanya kazi kwa kukunufaisheni kulingana na tadbiri aliyoiweka Allah SW. Mbali na neema hizo za kimaada zinazokidhi mahitaji ya kimwili ya mwanadamu, Mwenyezi Mungu amezingatia pia mahitaji ya kiroho na kifikra ya kiumbe huyo kwa kutuma Mitume na vitabu vya mbinguni na hivyo kumwandalia mazingira ya ujengekaji na utukukaji kiroho na kufikia ukamilifu wa kiutu. Lakini pamoja na hayo, kwa masikitiko ni kwamba katika zama zote za historia wamekuwepo watu ambao badala ya kushukuru neema zote hizo zilizowazunguka na zisizo na idadi wanaamua badala yake kufanya mijadala na mabishano kuhusu Mwenyezi Mungu bila ya kuwa na hoja za wazi za kielimu na kimantiki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mwanadamu ni waridi la bustani ya ulimwengu. Mbingu na ardhi na vilivyomo baina ya viwili hivyo vimeumbwa kwa ajili ya kumhudumia na kumnufaisha yeye. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa neema za Mola kwa mwanadamu ni nyingi na pia ni za aina kwa aina; kuanzia za kimaada mpaka za kimaanawi, za dhahiri zinazoonekana na pia za batini zilizofichikana. Kama ni hivyo, kwa nini mwanadamu ni mtovu wa shukurani? Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, mijadala na midahalo huwa na faida pale inapofanywa kwa msingi wa elimu na akili ya mwanadamu au kwa mwongozo wa kitabu cha mbinguni.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 21 ambayo inasema:

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اتَّبِعُوا مَا أَنزَلَ اللَّهُ قَالُوا بَلْ نَتَّبِعُ مَا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا أَوَلَوْ كَانَ الشَّيْطَانُ يَدْعُوهُمْ إِلَى عَذَابِ السَّعِيرِ

Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, husema: Bali tunafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je! Ijapo kuwa Shet'ani anawaita kwenye adhabu ya Moto uwakao?

Baada ya aya iliyotangulia kueleza kuwa wale wanaojenga shaka na kuzusha mijadala kuhusu Mwenyezi Mungu hawana hoja na mantiki wadhiha, aya hii ya 20 inasema: Hoja inayotolewa na wengi miongoni mwao kama sababu ya kufanya hivyo ni eti kuchunga mila na desturi zao za kale na kufuata waliyoyarithi kwa wazee wao waliotangulia. Wao hawako tayari kuacha imani potofu na itikadi batili za wazee wao waliopita; na badala ya kufuata mwongozo wa uongofu utokao kwa Allah wanaamua kufuata imani na mienendo hiyo potofu na batili waliyoirithi kwa mababa na mababu zao. Hali ya kuwa mantiki hiyo si sahihi na ni ya kishetani na itawafanya watu hao pia kama wazee wao waishie kwenye moto wa Jahanam. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba taasubu na imani potofu za kurithi, na kufuata kiupofu na kibubusa vitu hivyo ni miongoni mwa mambo yanayomzuia mtu kuikubali haki na kudumaza fikra na akili ya mwanadamu ishindwe kuutambua uongofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kutunza na kuhifadhi turathi za kiutamaduni pamoja na desturi na mila za kitaifa huwa na thamani pale turathi hizo zinapowiana na akili na dini; vinginevyo zinaweza kuwa sababu ya kupotoka na kuporomoka taifa na kaumu ya watu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba shetani huwa muda wote anamshawishi na kujaribu kumvuta na kumuelekeza mtu kwenye njia batili na ya upotofu.

Aya ya 22 hadi 24 ya sura yetu ya Luqman ndizo zinazotuhatimishia darsa yetu ya leo. Aya hizo zinasema:

وَمَن يُسْلِمْ وَجْهَهُ إِلَى اللَّهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَى وَإِلَى اللَّهِ عَاقِبَةُ الأُمُورِ

Na mwenye kuuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa anafanya wema, basi huyo hakika amekwisha kamata kishikilio madhubuti. Na mwisho wa mambo yote ni kwa Mwenyezi Mungu.

وَمَن كَفَرَ فَلا يَحْزُنكَ كُفْرُهُ إِلَيْنَا مَرْجِعُهُمْ فَنُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ

Na anaye kufuru, isikuhuzunishe kufuru yake. Kwetu ndio marudio yao, na hapo tutawaambia waliyo yafanya. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

نُمَتِّعُهُمْ قَلِيلا ثُمَّ نَضْطَرُّهُمْ إِلَى عَذَابٍ غَلِيظٍ

Tunawastarehesha kwa uchache, kisha tutawasukuma kwenye adhabu ngumu.

Aya hizi zinawagawa watu makundi mawili kwa kuzingatia msimamo wao kuhusiana na wito wa Mwenyezi Mungu. Kundi moja ni la watu ambao wanauendea wito wa Mola wao kwa ujudi wao wote na kusalimu amri mbele yake; na kundi jengine ni la watu waliohitari kukaidi na kuasi na hivyo kuukufuru wito waliofikishiwa na Mola Muumba. Kundi la kwanza limeishika kamba imara ya uongofu utokao kwa Allah ya njia sahihi iliyonyooka na kuwa watu wafanyao amali za kheri na kuwafanyia wema na ihsani wanadamu wenzao. Mwisho mwema ndio unaowasubiri watu hao. Ama watu wa kundi la pili, hata kama watanufaika na baadhi ya mambo ya kidunia na kujistarehesha nayo lakini mwishowe watakuwa na hatima mbaya na watafikwa na tabu na adhabu duniani na akhera. Duniani kwa namna moja na akhera kwa namna nyengine. Pamoja na hayo kwa kuwa Bwana Mtume Muhammad SAW ni nabii wa rehma, hakuwa akifurahi kwamba makafiri waliokuwa wakimuudhi na kumfanyia uadui watafikwa na adhabu kwa sababu ya ukafiri wao. Bali daima alikuwa akiwahurumia; na moyo wake ulikuwa ukiungulika kwa kuwaona wamepotoka. Hata hivyo watu hao walishajiamulia kufuata njia ya ukafiri; na yeye Bwana Mtume hangeweza kuwafanya wamwamini Allah kwa kuwalazimisha wafuate njia ya haki kwa nguvu.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ikiwa mfumo mzima wa ulimwengu wa maumbile na vyote vilivyomo ndani yake vinasalimu amri na kumtii Mwenyezi Mungu; na Yeye Mola ameviweka vyote hivyo kwa ajili ya kutuhudumia na kututumikia sisi wanadamu, kwa nini sisi tusimtii Mola wetu?

Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mwanadamu hapa duniani huchagua na kuyakimbilia maegemeo kadha wa kadha ya watu au vitu kwa ajili ya kulinda nafasi yake; lakini kwa watu waumini, egemeo na kimbilio lao ni Allah SW tu. Wanaupigania uwokovu kwa kushikamana barabara na Kamba ya Mola na kwa kufanya amali njema. Kwa mujibu wa hadithi, Mitume na Maimamu nao pia ni Kamba imara ya Mwenyezi Mungu. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba katika maisha ya dunia tujichagulie njia ya kufuata kwa kuangalia na kutafakari mustakabali wa dunia ili tusije tukawa na hatima mbaya mwisho wa uhai wetu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 735 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuwa washukurivu wa neema zake, kubwa na ndogo, za dhahiri na za batini, tunazozijua na tusizozijua. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags