Jumapili 21 Mei, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 24 Shaaban 1438 Hijria Qamaria sawa 21 Mei 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 2233 iliyopita, yaani sawa na tarehe 21 Mei mwaka 216 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as), jeshi la mtawala wa Carthage chini ya uongozi wa Hannibal, lilishindwa vibaya huko kaskazini mwa Italia. Hivyo vilikuwa vita vya pili baina ya utawala wa Carthage na Roma kwa anwani ya vita vya 'Punic.' Kwa kutumia tembo na wapandaji tembo mahiri Hannibal alishiriki vita hivyo kabla ya kushindwa vibaya.

Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita alifariki dunia Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wasomi wa sheria za Kiislamu na marjaa mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1230 Hijiria mjini Shirazi ambao ni kati ya miji ya kusini mwa Iran ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kujiunga na masomo ya Hawza na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo. Baada ya muda mfupi, Muhammad Hassan Shirazi alitokea kuwa msomi mkubwa wa Kiislamu huku akishika pia uongozi wa kidini mjini hapo. Aidha msomi huyo anafahamika kwa kutoa fatwa iliyopiga marufuku tumbaku, iliyotoa pigo kwa mkoloni Mwingereza.

Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, Andrei Sakharov, mwanafizikia mashuhuri wa Russia alizaliwa. Alihitimu taaluma ya fizikia katika chuo kikuu cha Moscow mwaka 1941 na kisha akaanza kufanya utafiti wa kina kuhusiana na nishati ya nyuklia. Alikuwa na nafsi muhimu katika utengenezaji wa bomu la hydrogen nchini Russia. Sakharov pia alikuwa muungaji mkono mkubwa wa harakati za kutokomezwa silaha za nyuklia na ndio maana akatunukiwa zawadi ya amani ya Nobel hapo mwaka 1975. Miaka mitano baadaye Sakharov alibaidishiwa katika mji wa Gorky, mashariki mwa Moscow kutokana na upinzani wake dhidi ya siasa za utawala wa kikomonisti wa Russia. Hata hivyo ubaidishaji huo ulifikia kikomo mwaka 1986 baada ya Mikhail Sergeyevich Gorbachev kutwaa madaraka. Mwanzoni mwa mwaka 1989 Sakharov alichaguliwa kuwa mbunge katika bunge la Russia lakini akaaga dunia baadaye mwezi Disemba mwaka huohuo.

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Rajiv Gandhi, Waziri Mkuu wa zamani wa India aliuawa kigaidi. Rajiv Gandhi alikuwa mwanawe Indira Gandhi Waziri Mkuu wa zamani pia wa nchi hiyo. Alizaliwa tarehe 20 Agosti 1944 mjini Bombay na kulelewa katika nyumba ya babu yake Jawaharlal Nehru, Waziri Mkuu wa kwanza wa India. Rajiv Gandhi aliingia katika ulingo wa siasa baada ya kuaga dunia mdogo wake ambaye alikuwa akitayarishwa kumrithi kisiasa mama yake Indira Gandhi. Alichukua hatamu za kuiongoza India baada ya kuuliwa kigaidi mama yake hapo tarehe 31 Oktoba 1989. Rajiv Gandhi alikuwa na nia ya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa bunge lakini aliuawa na magaidi tarehe 21 Mei 1991 akiwa na umri wa miaka 47 alipokuwa akifanya kampeni za uchaguzi huo huko kusini mwa India.

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, Jenerali Suharto wa Indonesia alilazimika kujiuzulu baada ya kuitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa miaka 33. Aliingia madarakani mwaka 1965 baada ya kumpindua Ahmad Sukarno, mwanzilishi wa Indonesia huru ambaye alikuwa amechaguliwa na wananchi wa nchi hiyo. Uhuru wa kisiasa ulibanwa sana katika kipindi cha utawala wa Suharto. Hata hivyo nchi hiyo ilishuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi katika utawala wake katika miongo ya 80 na 90. Pamoja na hayo lakini mgogoro wa kiuchumi uliozikumba nchi za Asia Mashariki katika mwaka wa 1997 ulianzisha malalamiko na maandamano makubwa ya wanafunzi wa Indonesia na taratibu yakachukua mkondo wa kisiasa uliopelekea Suharto kuondolewa madarakani. Ufisadi wa kiuchumi uliofanywa na Suharto pamoja na familia yake ulichochea zaidi kuanguka kwa utawala wake, ambako kulitanguliwa na kujiuzulu kwake madarakani.

Na siku kama ya leo miaka 11 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Mei 2006, nchi ya Montenegro ilijipatia uhuru wake kutoka Jamhuri ya Serbia baada ya kufanyika kura ya maoni. Kuanzia karne ya 16 hadi 19, Montenegro ilikuwa chini ya himaya ya utawala wa Othmaniya. Amma baada ya kusambaratika utawala wa Yugoslavia ya zamani, nchi hiyo ikaanza harakati za kujipatia uhuru wake, na ulipoanza mgogoro wa Kosovo mwishoni mwa muongo wa 1990, Montenegro ilikata uhusiano wake wa kisiasa na kiuchumi na Serbia na mgogoro wa pande hizo mbili ukazidi kupamba moto.
