May 24, 2017 16:57 UTC

Sura ya As-Sajdah, aya ya 15-19 (Darsa ya 741)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’an, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’an. Hii ni darsa ya 741 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni aya ya 32 ya As-Sajdah. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 15 ambayo inasema:

إِنَّمَا يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا الَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِهَا خَرُّوا سُجَّدًا وَسَبَّحُوا بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ

Hakika wanao ziamini aya zetu ni wale tu ambao wanapokumbushwa hizo, huanguka kusujudu, na humsabihi Mola wao Mlezi kwa kumhimidi, nao hawatakabari.

Si ajabu kukuta watu ambao wanajinasibu kuwa waumini kwa ndimi zao, lakini matendo yao ni tofauti na kauli zao. Watu hao wanadai kuwa wameamini lakini amali na vitendo vyao haviendani kabisa na Qur’ani. Wanasema wameamini, lakini hawako tayari kumsujudia Mwenyezi Mungu wala hawana upole na unyenyekevu katika kuamiliana na watu. Wanamuasi Mola wao na pia wanajivuna na kujitukuza mbele ya wanadamu wenzao. Aya hii tuliyosoma imeanza na neno “innamaa” lenye kubainisha ujumuishi wa hali moja tu na kukana nyengine zote; kwa maana kwamba, ni watu wenye sifa hizi zilizotajwa tu ndio waumini halisi na wa kweli; wengineo wasiokuwa hivyo ni warongo katika kudai kwao kama wameamini. Miongoni mwa sifa za waumini wa kweli ni kusalimu amri mbele ya maneno ya Mola wao ya Qur’ani kwa namna ambayo, kila wanaposikia wito wa Kitabu hicho husalimu amri na wakaporomoka kusujudu, wakamhimidi na kumsabihi Mola wao. Au kila pale wanapokumbushwa na kuaidhiwa kwa aya za Qur’ani wanakubali ukumbusho wanaopewa bila ya kuhoji; na wala hawajivuni na kutakabari. Kwa upande mmoja wanamshukuru Allah kwa neema alizowajaalia na kwa upande mwengine wafikwapo na matatizo na masaibu ya maisha hawambebeshi lawama Mola wao, bali wanamtakasa na kila ila na kasoro katika tadbiri na uendeshaji wake wa masuala ya walimwengu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kumsujudia Mwenyezi Mungu pamoja na kumhimidi na kumsabihi ni miongoni mwa alama za muumini wa kweli. Muislamu yeyote asiyesali, kwa kweli hajafikia daraja ya kuitwa mtu mwenye imani ya kweli. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa dhikri na utajo bora wa kusoma katika hali ya kusujudu ni kumsabihi Allah pamoja na kumhimidi; yaani kusema Subhaana Rabbiyal-A'alaa Wabihamdih. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, kusujudu huwa na thamani na utukufu ikiwa kutamsafisha na kumtakasa mtu na ghururi, kiburi na majivuno.

Tunaiendeleza darsa yetu ya leo kwa aya ya 16 na 17 ambazo zinasema:

تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

Mbavu zao zinaachana na vitanda kumwomba Mola wao Mlezi kwa khofu na tumaini, na hutoa katika yale tuliyo waruzuku.

فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

Nafsi yoyote haijui waliyo fichiwa katika hayo yanayo furahisha macho- ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda.

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kuhusu kunyenyekea mbele ya Allah na maneno yake Mola na kuashiria sifa nyengine za waumini wa kweli kwa kueleza kwamba, watu hao hawaishii kutekeleza Sala za faradhi na wajibu tu lakini katika usiku wa manane, wakati watu wote wamelala na kujipumzikia, wao huinuka vitandani mwao wakasimama kusali, kufanya munajati na kunong’ona na Mola wao. Usiku wa manane ndio wakati bora kwa mja kutaradhia, kuomba na kunong'ona na Allah SW. Kwa sababu katika wakati huo, mtu huwa amejivua na pirika za kutwa za mashughuliko ya kazi  na mazonge ya mawazo na fikra, hivyo huwa na umakini na utulivu wa moyo kwa ajili ya kuzungumza na kunong’ona na Mola wake Mlezi. Faragha ya usiku wa manane ni fursa mwafaka kwa mja kuomba maghufira kwa makosa aliyofanya, kwa hali ya kutarajia kupata msamaha na rehma za Allah na wakati huohuo kuililia nafsi yake kwa hofu ya kuchelea kufikwa na adhabu ya Moto. Hakuna shaka yoyote kwamba, kuwa na mawasiliano ya namna hiyo na Allah humwongoza mtu katika kujenga mawasiliano pia na waja wake Mola. Huwashughulikia wanyonge na wahitaji kwa kuwatatulia shida na haja zao kadiri ya uwezo wake, na kutoa kuwasaidia waja wa Mwenyezi Mungu, mali ambayo ameruzukiwa na Yeye Mola. Kisha aya zinaendelea kwa kuzungumzia malipo ya watu hao kwa kusema: Wale ambao wanamwabudu Mola wao kwa shauku na  mapenzi, bila ya kufanya ria na kujionesha kwa watu na wanashughulikia shida na matatizo ya waja wa Mwenyezi Mungu wana ujira na malipo yasiyotasawarika. Kwa hakika hakuna yoyote ghairi ya Mola ajuaye ni ujira na malipo yenye thamani kubwa iliyoje waliyoandaliwa waja hao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, muumini wa kweli ni yule ambaye hajihisi yuko kwenye amani ya kunusurika na adhabu na ghadhabu za Allah, wala havunjiki moyo na kukata tamaa na rehma zake Mola. Yeye huwa muda wote anaishi katika hali ya hofu na matumaini, pasi na kuingiwa na ghururi wala kukata tamaa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kukesha kwa ibada na kuusamehe usingizi kwa kusoma Qur’an, kusali na kunong’ona na Muumba wa ulimwengu ni miongoni mwa alama za waumini wa kweli. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba inastahiki kuukabili ugumu na uzito wa kuamka na kukesha usiku kwa ibada ili kupata malipo ya thawabu zisizohesabika.

Darsa yetu ya 741 inahatimishwa na aya ya 18 na 19 ambazo zinasema:

أَفَمَن كَانَ مُؤْمِنًا كَمَن كَانَ فَاسِقًا لَّا يَسْتَوُونَ

Ati aliye Muumini atakuwa sawa na aliye fasiki? Hawawi sawa.

أَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَلَهُمْ جَنَّاتُ الْمَأْوَىٰ نُزُلًا بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

Ama walio amini na wakatenda mema, watakuwa na Bustani za makaazi mazuri. Ndipo pa kufikia kwa waliyo kuwa wakiyatenda.

Aya hizi zinaendeleza maudhi ya aya zilizotangulia kwa kulinganisha waumini wa kweli na wale wanaojigamba tu kuwa wameamini na kueleza kwamba: Tazama hatima ya makundi yote mawili ili ujue yule anayetii na kutekeleza kweli maamrisho ya Mwenyezi Mungu anaishi wapi na yule anayedai kwa ulimi wake tu kuwa ni muumini lakini katika matendo anamwasi Mola wake anakuwa na mwisho upi. Tambua kwamba wawili hao katu hawawi sawa mbele ya Allah SW. Kisha aya zinaendelea kwa kueleza kuwa peponi ni pahala ambapo Allah amewaandalia waja wake wema na waumini wa kweli na kila mmoja wao atakuwa na daraja kulingana na amali zake njema alizofanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika  kuwalingania wati imani ya dini tulinganishe maisha ya waumini wa kweli na wale mafasiki na wafanya madhambi ili waweze kubainikiwa kwa uwazi kabisa na nukta chanya na hasi za makundi yote mawili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa imani na amali havitenganiki; na Pepo ni malipo ya amali njema za watu si kudai kwao tu wameamini. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 741 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah radhi zake na Pepo na tunajilinda kwake na ghadhabu zake na adhabu ya Moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags