Jun 12, 2017 01:34 UTC
  • Jumatatu 12 Juni, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 17 Ramadhani 1438 Hijria sawa na Juni 12, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia Mtume Mtukufu Muhammad SAW alisafiri kutoka Makka hadi Baitul Muqaddas na kupaa mbinguni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Aya ya kwanza ya Sura ya al Isra inatoa maelezo kuhusu muujiza huo mkubwa ikisema. "Ametakasika aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara zetu. Hakika yeye ni mwenye kusikia na mwenye kuona." Kwa kuzingatia aya hiyo na hadithi za Mtume Muhammad SAW, wakati mtukufu huyo alipokuwa katika safari ya Miiraji alionyeshwa siri nyingi za Mwenyezi Mungu SW, viumbe vyake Jalali na hatima ya wanadamu katika ulimwengu wa Akhera.

Tukio hilo ni miongoni mwa miujiza mikubwa ya Mtume Muhammad SAW na linadhihirisha nafasi ya juu ya mtukufu huyo.

Tarehe 17 Ramadhani miaka 1436 iliyopita, vita vya Badr, moja kati ya vita maarufu vya Mtume Muhammad SAW, vilitokea katika eneo lililoko kati ya Makka na Madina. Badr ni jina la kisima kilichoko umbali wa kilomita 120 kusini magharibi mwa mji wa Madina, ambako kulipiganwa vita vya kwanza kati ya Waislamu na washirikina. Vita vya Badr vilitokea huku washirikina wakiwa na wapiganaji wengi waliokaribia 920 na jeshi la Kiislamu likiwa na wapiganaji 313 na silaha chache. Hata hivyo imani thabiti ya Waislamu iliwafanya washinde vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 477 iliyopita nchi ya Chile iliyoko magharibi mwa Amerika ya Kusini ilitekwa na wakoloni wa Hispania. Kabla ya hapo Wahindi Wekundu wa Chile walikuwa wamevunja hujuma na mashambulio kadhaa ya Wahispania waliokusudia kuteka na kukalia kwa mabavu ardhi yao. Hata hivyo, hata baada ya kutekwa nchi yao, Wahindi Wekundu hao waliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni hadi pale José Francisco de San Martín jenerali wa Argentina alipowasili mwaka 1817 na kuanzisha mashambulio ya kuzikomboa nchi zote zilizokuwa chini ya ukoloni wa Hispania Kusini mwa Amerika, ikiwemo Chile. Kwa msingi huo, Chile akakombolewa na kutangaza uhuru wake mwaka 1818.

Bendera ya Chile

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1914, kwa mara ya kwanza kabisa yalifanyika majaribio ya kutumia nishati ya joto la jua pambizoni mwa Cairo mji mkuu wa Misri. Mbunifu na mtekelezaji wa mpango huo, alikuwa mwanafizikia wa Kijerumani, ambaye aliweza kukusanya miale ya jua, na kufanikiwa kuwasha mashine ya mvuke yenye kutumia 'horse power' 50.

Nishati ya jua

 

Tags