Jun 24, 2017 04:10 UTC
  • Jumamosi, 24 Juni, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 29 Ramadhani 1438 Hijria sawa na tarehe 24 Juni mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 790 iliyopita alizaliwa katika mji wa Hillah Iraq, Ayatullah Jamaldeen Hassan bin Yusuf mwenye lakabu ya Allamah Hilli mwanazuoni mahiri wa Kiislamu. Awali alisoma kwa baba yake na mjombake na akiwa katika rika la ujana alikuwa tayari amefanikiwa kufikia daraja za juu za elimu katika taaluma kama fikihi, Usul Fikih, hadithi na kadhalika.  Mwanazuoni huyo alikuwa mahiri pia katika uga wa uandishi. Miongoni mwa vitabu vya Ayatullah Jamaldeen Hassan bin Yusuf ni Tadhkiratul al-Fuqahaaa, Irshadul adh'han, na Kashful Murad. Alimu huyo aliaga dunia mwaka 726 Hijria.***

Allamah Hilli

Katika siku kma ya leo miaka 631 iliyopita aliaga dunia mjini Cairo Misri, Nasserdeen Muhammad al-Maarufu kwa jina la Ibnu Furaat. Alikuwa fakihi mahiri, mwanahistoria, hatibu na mhubiri stadi wa Misri. Alizaliwa mwaka 735 Hijria huko Cairo na alianza kujifunza elimu tangu akiwa kijana mdogo. Ibnu Furaat alikuwa na mapenzi makubwa na histotia na kitabu chake mashuhuri katika uwanja huo ni kile kiitwacho "Tarikh al-Daulah Wal-Muluk". Aidha Ibn Furat ana vitabu vibngine mashuhuri kama "Asmaau al-Sahabah".***

Ibn Furaat

Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, Napoleone Bonaparte mtawala wa Ufaransa akiwa na kikosi cha askari 350,000 alianza kufanya mashambulio dhidi ya utawala wa Russia wa Tsar. Miaka mitano kabla ya tukio hilo, nchi mbili hizo zilikuwa zimetiliana saini mkataba wa kutoshambuliana kijeshi. Hata hivyo taratibu uhusiano baina ya tawala mbili hizo ulianza kuharibika, na hivyo kumfanya Bonaparte afikie hatua ya kuandaa jeshi kubwa na kuishambulia Russia na kisha kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Moscow. Hata hivyo hali mbaya ya hewa yaani baridi kali na kutowafikia wanajeshi wa Kifaransa vifaa muhimu na suhula za kivita, kuliwafanya askari hao wakabaliwe na hali ngumu katika medani ya vita. Hali hiyo ilimlazimisha Bonaparte atoe amri ya kurejea nyuma vikosi vyake. Wakati wa kujiri zoezi hilo, askari jeshi wapatao 30,000 wa Kirusi walivishambulia vikosi vya Bonaparte na kuwaua wengi miongoni mwao. Akiwa amebakiwa na askari 30,000 tu, Bonaparte aliikimbia Russia na kufanikiwa kuwasili Paris Ufaransa Desemba mwaka 1812.

Napoleone Bonaparte

Katika siku kama ya leo miaka 174 iliyopita, tanuu za feleji maarufu kwa jina la tanuu za Bessemer zilivumbuliwa. Mvumbuzi wa tanuu hizo alikuwa Mwingereza Henry Bessemer. Tanuu hizo zilitumika huko Uingereza kwa mara ya kwanza na leo hii zinatumika katika masuala mbalimbali viwandani. ***

Henry Bessemer

Na miaka 22 iliyopita Ustadh Sayyid Muslihdeen Mahdavi Isfahani mwandishi wa Kiirani aliaga dunia. Alizaliwa mjini Isfahan moja ya miji ya Iran alianza kujihusisha kwa bidii kubwa na elimu tangu wakati wa kuinukia kwake. Alihudhuria darsa za Maustadhi mirza Muhammad Ali Habib Abadi na Sayyid Muhammad Kadhim Isar. Msomi huyo ameandika vitabu pia katika Nyanja mbalimbali.

 

Sayyid Muslihdeen Mahdavi Isfahani

 

Tags