Jumapili Julai 16, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 21 Shawwal 1438 Hijria, sawa na Julai 16, 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1346 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya mapambano ya Waislamu, akiwa na jeshi kubwa la Kiislamu Twariq bin Ziyad aliweza kuingia Uhispania. Ushindi huo ulikuwa mwanzo wa maendeleo ya Waislamu barani Ulaya ambapo umeenea hadi leo kufikia Ufaransa. Twariq bin Ziyad aliwasili Uhispania baada ya kuvuka lango bahari kati ya Morocco na Uhispania linalojulikana kwa jina lake mwenyewe yaani "Jabal Tariq." Mlango bahari huo unatumika kama njia ya mawasiliano kati ya Bahari za Atlantic na Mediterranean. Waislamu walitawala kwa karne nane huko Uhispania na kueneza mafunzo na utamaduni wa Kiislamu barani Ulaya baada ya kutekwa Andalusia, Uhispania ya leo.

Siku kama ya leo miaka 1084 iliyopita, alifariki dunia Ibn Habban, mtaalamu wa hadithi, elimu ya fiq'hi na mwanahistoria mashuhuri wa karne ya 14 Hijiria. Alipata elimu ya msingi kwa walimu mashuhuri wa zama zake na kisha akaelekea Neishabur kaskazini mashariki mwa Iran, mji ambao katika kipindi hicho ulikuwa ni moja ya vituo muhimu vya kielimu. Ibn Habban anahesabika kuwa mtu mwenye nadharia muhimu katika elimu ya hadithi. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha"At-Thuqat" na Rawdhatul-Uqalaa wa Nazahatul-fudhalaa."

Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita James Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea. Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina lake. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili. Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita bomu la kwanza la nyuklia la Marekani liliripuliwa wakati wa majaribio. Marekani ilifanya jaribio hilo la bomu la nyuklia ili kujiandaa kuishambulia Japan kwa kutumia mabomu hayo. Wakati huo Japan ilikuwa ikipigana na madola makubwa na majeshi ya nchi waitifaki, ikiwemo Marekani.

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita nchi ya Nepal iliyoko katika bara la Asia ilipata uhuru. Ushawishi na uingiliaji wa Uingereza huko Nepal mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, ulisababisha vita kati ya nchi mbili hizo ambapo mwishoni mwa kumalizika vita mwaka 1816, Uingereza ikalikoloni eneo kubwa la ardhi ya Nepal na kuiunganisha ardhi ya India pia na nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena ilifanikiwa kupokea mateka watano na miili ya karibu mashahidi 200 wa Kilebanoni kutoka kwa utawala wa Kizayuni. Ubadilishanaji huo wa miili na mateka hao ulifanyika kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande mbili hizo kwa usimamizi wa serikali ya Ujerumani. Nukta ya kushangaza katika oparesheni hiyo ni hii kwamba vyombo vya usalama na ujasusi vya utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho havikuwa na habari kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa mwanzoni mwa mapigano kati ya jeshi la utawala wa Kizayuni na wapiganaji wa Huzbullah. Shakhsia wengine kutoka makundi ya mapambano ya Lebanon pia walikuwa miongoni mwa mateka walioachiwa huru na utawala wa Kizayuni. Shakhsia muhimu zaidi kuliko wote alikuwa Samir Qantar ambaye alipoteza karibu miaka 30 ya umri wake akiwa katika jela za utawala wa Kizayuni.
