Alkhamisi 3 Agosti, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Dhilqaada mwaka 1438 Hijria mwafaka na tarehe Tatu Agosti 2017.
Siku kama ya leo miaka 525 iliyopita baharia wa Kiitalia Christopher Columbus alianza safari kubwa zaidi ya kiuvumbuzi. Christopher Columbus alipewa jukumu la kuvumbua njia mpya inayoelekea India katika makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mfalme na malkia wa Uhispania. Christopher Columbus aliondoka katika bandari ya Paulus huko Uhispania akiwa na meli tatu na mabaharia 120 na hatimaye walifika katika nchi kavu baada ya kuwa baharini kwa siku 33. Baharia huyo wa Kiitalia na wenzake walidhani kuwa wamefika India. Hata hivyo walikuwa wamefika katika kisiwa kilichojulikana kwa jina la Salvador katika bara la Amerika.
Miaka 103 iliyopita katika siku kama hii ya leo Mfereji wa Panama ulifunguliwa baada ya meli ya kwanza kupita katika mfereji huo. Mfereji wa Panama ulianza kujengwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye ujenzi huo ukakamilishwa na Wamarekani. Mfereji wa Panana ulio na urefu wa kilomita 68 unaunganisha bahari mbili za Atlantic na Pacific.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, mwafaka na tarehe 3 Agosti 1960, nchi ya Kiafrika ya Niger ilipata uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Niger ilikuwa chini ya himaya ya Ufaransa tangu karne ya 18 na mwaka 1922 ikawa koloni rasmi la Wafaransa baada ya nchi hiyo kujenga vituo vyake vya kijeshi nchini humo. Hata hivyo taratibu wananchi wa Niger walianzisha uasi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa na hatimaye nchi hiyo ilifanikiwa kupatia uhuru katika siku kama hii ya leo. Niger iko magharibi mwa Afrika na inapakana na Libya, Chad, Mali na Benin.

Na miaka 39 iliyopita sawa na tarehe 3 Agosti 1978 utawala wa Kizayuni ulimuuwa kigaidi Izzudin Qalq, mwakilishi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na naibu wake huko Paris, Ufaransa. Shirika la ujasusi la utawala wa kibaguzi wa Israel Mossad liliwauwa viongozi wengi wa PLO katika miongo miwili ya 1970 na 1980 lengo likiwa ni kudhoofisha mapambano ya ukombozi wa Palestina na kuwalazimisha wapigania uhuru kufikia makubaliano eti ya mapatano na utawala huo haramu.