Aug 06, 2017 18:27 UTC
  • Jumapili Agosti 6, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 13 Dhul-Qaadah mwaka 1438 Hijria, sawa na tarehe 6 Julai, 2017.

Siku kama ya leo miaka 672 iliyopita, alifariki dunia Qutbu Din Muhammad Razi. Razi alizaliwa katika viunga vya mji wa Rey na kwa kuwa alikulia katika mji huo ndipo akapata umashuhuri wa jina la Razi. Qutb ad-Din Muhammad Razi alikuwa mwanafunzi mkubwa wa Allamah Hilli. Kwa kipindi fulani aliwatumikia Sultan Abu Said na waziri wake Khaja Ghiyathuddin Mohammad ambapo pia aliweza kuandika vitabu viwili vya 'Sharhu al-Shamsiyyah' na 'Sharhu Matwaali'.' Baada ya kufariki dunia Sultan Abu Said, Qutbu Din Muhammad Razi alielekea Sham na alifariki dunia mjini Damascus. 

Qutb ad-Din Muhammad Razi

Siku kama ya leo miaka 410 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Mirza Muhammad Isterabadi, mtaalamu wa sheria za Kiislamu na elimu ya theolojia. Ayatullah Mirza Muhammad Bin Ali Bin Ibrahim Isterabadi alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Awali alikuwa akiiishi mjini Najaf, Iraq na baadaye alielekea Makkah na kufanya makazi mjini hapo. Isterabadi ni kati ya watu wanaoelezwa kuwa waliopata sharafu ya kukutana na Imam wa zama (af). Msomi huyo aliandika vitabu juu ya wapokezi wa hadithi kikiwemo kitabu cha 'Tawdhihul-Maqaal' 'Talkhisul-Aqwaal' na 'Manhajul-Maqaal.' Vitabu hivyo vinatambuliwa kuwa vitabu muhimu na chemchemi ya elimu ya wapokezi wa hadithi .

Ayatullah Mirza Muhammad Isterabadi

Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, nchi ya Bolivia ilifanikiwa kupatia uhuru kutoka mikononi mwa mkoloni Muhispania. Ukoloni wa Uhispania dhidi ya Bolivia ulianza katika karne ya 16 kwa kupora utajiri wa madini wa nchi hiyo. Katika kipindi cha utawala wa Wahispania kulishuhudiwa harakati mbalimbali za wananchi waliokuwa wakipambana na wakoloni hao wakidai uhuru chini ya kiongozi wao Simón Bolívar. Mapinduzi hayo yalianza mwaka 1809 na taratibu yakaenea katika nchi yote ya Bolivia na hatimaye yakafanikiwa kuwaondoa wakoloni hao na kupatikana uhuru katika siku kama ya leo mwaka 1825.

Ramani ya nchi ya Bolivia

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, alizaliwa Alexander Fleming tabibu, mwanabiolojia na mtaalamu wa madawa wa Scotland. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, tabibu huyo pamoja na wasomi wenzake wawili Chain na Florey, waligundua dawa ya antibiotic ya Penicillin. Mwaka 1945, wasomi hao watatu kwa pamoja walitunukiwa tuzo ya Nobel katika elimu ya tiba kutokana na ugunduzi wao huo muhimu. Penicillin inatumika sana hivi sasa katika elimu ya tiba.

Alexander Fleming

Siku kama leo miaka 72 iliyopita, kwa mara ya kwanza kabisa duniani Marekani iliushambulia vikali kwa mabomu ya nyuklia mji wa Hiroshima huko Japan mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Mabomu hayo yalikuwa na nguvu kubwa ya uharibifu iliyokuwa sawa na tani elfu 20 ya mada za milipuko za TNT. Katika mashambulizi hayo watu zaidi ya elfu 90 waliuawa na wengine 75 elfu kujeruhiwa. Athari mbaya za mabomu hayo ya nyuklia zingali zinashuhudiwa hadi hii leo huko Hiroshima licha ya kupita miaka mingi sasa tangu kufanyike mashambulizi hayo ya nyuklia ya Marekani. Muda mfupi baada ya kuushambulia mji wa Hiroshima, Marekani iliushambulia pia kwa mabomu ya nyuklia mji wa Nagasaki huko huko Japan na kuilazimisha nchi hiyo kusalimu amri. Maafa hayo ya kutisha na kusikitisha yaliyofanywa na Marekani katika miji miwili ya Japan ambayo yanahesabiwa kuwa jinai kubwa zaidi ya kivita katika historia, yanaonyesha kuwa silaha za nyuklia ni wenzo hatari sana katika mikono ya nchi zinazopenda kujitanua duniani kama Marekani na ndiyo maana kuna udharura wa kusimamiwa na kudhibitiwa silaha hizo na taasisi husika, na hatimaye kutokomezwa kabisa kwa ajili ya usalama wa dunia.

Mji wa Heroshima baada ya kushambuliwa kwa nyuklia

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita nchi ya Jamaica inayopatikana huko Amerika ya Kati ilipata uhuru. Jamaica iligunduliwa mwaka 1494 na mvumbuzi Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania kuanzia karne ya 16 hadi ya 18. Nchi hiyo baadaye ilikoloniwa na Uingereza; na maghasibu wa Ulaya wakawafukuza wenyeji wa kisiwa hicho na badala yake wakawachukua makumi ya maelfu ya watumwa weusi kwa ajili ya kuwalimia mashamba yao.

Ramani ya Jamaica

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein alilazimika kukubali usitishaji vita na Iran. Baada ya Iran kukubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo tarehe 27 Tir mwaka 1367 Hijria Shamsia ambalo lilijumuisha usitishaji vita baina ya pande mbili, ilitarajiwa kuwa mapigano ya kijeshi baina ya nchi hizo mbili pia yangekomeshwa. Hata hivyo siku kadhaa baadaye Saddam Hussein alifanya mashambulizi makubwa dhidi ya ardhi ya Iran ambayo yalifeli kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa Kiirani. Hatimaye Saddam Hussein ambaye aliilazimisha Iran kuingia katika vita vya miaka 8 vilivyosababisha hasara kubwa ya hali na mali na hakuweza kufikia malengo yake, alikubali kusitisha mapigano katika siku kama hii ya leo na kutekeleza makubaliano hayo wiki mbili baadaye.

Azimio nambari 598

Na Miaka 22 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Agosit 6, 1995, Profesa Kighoma Ali Malima aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha NRA katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini Tanzania aliaga dunia. Malima alizaliwa mwaka 1938 katika wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani. Akiwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 19 na mwanafunzi hodari alikatisha masomo yake ya sekondari ili ajiunge na TANU katika harakati za kuikomboa Tanganyika kutoka katika utumwa wa Waingereza. Hayati Profesa Malima, atakumbukwa na wapenda haki wengi nchini Tanzania kutokana na kupinga kwake dhulma. Profesa Kigoma Ali Malima aliaga dunia ghafla katika mazingira ya kutatanisha huko mjini London, Uingereza alikopitia kutoka Makka alikokwenda kufanya Umra, zikiwa zimepita siku chache tu tangu alipotangaza uamuzi wake wa kukihama chama tawala cha CCM kufuatia kujiuzulu wadhifa wa uwaziri katika serikali ya chama hicho. Suala hilo lilimfanya akasirikiwe sana na chama hicho cha CCM.

Profesa Kighoma Ali Malima

 

Tags