Jumatano, Agosti 23, 2017
Leo ni Jumatano tarehe Mosi Mfunguo Tatu Dhulhija 1438 Hijria sawa na 23 Agosti 2017 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita, Bibi Fatima Zahra binti ya Mtume SAW alianza maisha mapya baada ya kufunga ndoa na Imam Ali bin Abi Talib AS. Bibi Fatima alikuwa mwanamke mwema, mtukufu na kigezo bora cha Waislamu. Masahaba mashuhuri walijitokeza kumposa binti huyo wa Mtume. Hata hivyo, Mtume alikuwa akimjibu kila aliyekwenda kumposa binti yake huyo kwamba, suala la ndoa yake liko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Baada ya kufunga ndoa, watukufu hao walianza maisha yao ya kawaida kabisa yaliyojaa huruma, upendo na masuala ya kiroho na kimaanawi. Familia hiyo imeitunuku dunia shakhsia adhimu na wa kupigiwa mfano kama Imam Hassan, Imam Hussein na Bibi Zainab (as).
Miaka 852 iliyopita katika siku kama ya leo yaani mwaka 586 Hijiria, alizaliwa Ibn Abil Hadid mwanazuoni na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu. Athari muhimu zaidi ya Ibn Abil Hadid ni shere ya Nahjul Balaghah ambacho ni kitabu kilichokusanya, semi za hekima, barua na hotuba za Imam Ali bin Abi Twalib (AS). Katika kitabu hicho Ibn Abil Hadid amefanya jitihada kubwa kuonyesha adhama ya Nahjul Balagha kwa kuzingatia fasihi, historia na ufasaha wa lugha. Kitabu kingine cha mwandishi huyo wa Kiislamu ni Al 'Abqariyul Hisaan na al Qasaaidus Sab'i fii Mad'hi Sayyidina Ali (as).
Siku kama ya leo miaka 73 iliyopia mji wa Paris ulikombolewa kutoka kwenye uvamizi wa Ujerumani. Miezi 15 baada ya kushtadi moto wa Vita vya Pili vya Dunia dikteta Adolph Hitler aliyaamuru majeshi ya nchi hiyo kuushambulia mji wa Paris kwa lengo la kutaka kuudhibiti. Tarehe tano Juni mwaka 1940, Hitler alitoa amri ya kuharibiwa kikamilifu muundo wa majeshi ya Ufaransa ambapo siku tatu baadaye yaani tarehe nane Juni mwaka 1940, vikosi vya majeshi ya Wanazi vilikishinda kikosi cha ulinzi cha Ufaransa katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na jeshi la Ujerumani likaingia nchini Ufaransa bila ya upinzani wowote. Mji wa Paris ulikaliwa kwa mabavu na Ujerumani kwa kipindi cha miaka 4 na ulikombolewa katika siku kama hii ya leo baada ya Wajerumani kushindwa mtawalia katika medani mbalimbali za vita. Mji huo ulikombolewa na majeshi ya waitifaki.
Tarehe Mosi Shahrivar katika kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi Hassan bin Abdullah maarufu kwa jina la Abu Ali Sinan na siku ya daktari. Abu Ali Sina alizaliwa tarehe 3 Safar mwaka 370 Hijria katika eneo la Balkh na kujifunza elimu za zama hizo akiwa bado kijana hadi alipopata umashuhuri mkubwa katika taaluma mbalimbali na kutambuliwa kuwa gwiji wa zama hizo. Alikuwa miongoni mwa wanafalsafa, maurafa na matabibu wakubwa. Ibn Sina alihifadhi Qur'ani yote alipokuwa na umri wa miaka 10. Alijifunza utabibu baada ya kupata elimu za mantiki, hisabati, nujumu, falsafa pamoja na elimu nyinginezo. Alianza kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 21 na miongoni mwa vitabu vyake maarufu ni Qanun, Shifaa na Isharaat.