Sep 03, 2017 02:26 UTC
  • Jumapili Septemba Tatu

Leo ni Jumapili tarehe 12 Dhul-Hajj mwaka 1438 Hijiria, sawa na tarehe tatu Septemba 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 965 iliyopita alizaliwa katika mji wa Ghazni, malenga wa Kiirani Hakim Abul-Majd Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi. Akiwa kijana mkufunzi huyo wa mashairi ya Kirafrsi alianza kusoma mashairi ambapo awali alianza kuwasifu shakhsia wakubwa. Hata hivyo alitokewa na mabadiliko ya ghafla katika nafasi yake na kwenda kufanya ibada ya Hijjah katika al-Kaabah ya Mwenyezi Mungu. Akiwa mjini Makkah sambamba na kufanya ibada ya Hijjah, alisoma mashairi ya kusifu nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu. Na baada ya kurejea aliendelea na shughuli hiyo mjini Balkh, moja ya mikoa ya Afghanistan ya sasa. Ameacha athari mbalimbali katika uga wa mashairi ambazo hadi sasa zimehifadhiwa mjini Khurasan na Balkh.

Malenga wa Kiirani Hakim Abul-Majd Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi

Siku kama ya leo miaka 498 iliyopita yaani tarehe 12 Dhul-Hijja mwaka 940 Hijria, alifariki dunia Ali ibn Hussein Karaki Amuli, mmoja wa wataalamu wakubwa wa sheria za Kiislamu. Awali alisoma masomo yake katika eneo alikozaliwa la Jabal Amil nchini Lebanon. Kisha akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu alifanya safari katika nchi za Kiislamu. Mhakiki Karaki kama anavyojulikana zaidi, ameacha vitabu vingi vyenye thamani kubwa. Jamiul Maqaasid na Risatul Adalah ni baadhi ya vitabu vyake mashuhuri.

Ali ibn Hussein Karaki Amuli

Siku kama ya leo miaka 359 iliyopita, alifariki dunia Oliver Cromwell, rais wa kwanza na wa mwisho wa Uingereza. Tangu akiwa kijana Cromwell aliingia katika harakati za kisiasa na kijamii na baadaye kujiunga na bunge la nchi hiyo mwaka 1640. Wakati huo aliyekuwa mfalme wa Uingereza alikuwa ni Charles I. Mwishoni mwa ufalme wa Charles I kulitokea msuguano kati yake na bunge hasa baada ya bunge kutokuwa na imani na mfalme. Suala hilo lilipelekea Oliver Cromwell kuunda kikosi cha jeshi ambalo wakati wa vita vya ndani kikosi hicho kilikuwa upande wa bunge na hatimaye kupelekea mfalme Charles l kushindwa. Baada ya mfalme huyo kushindwa alikimbilia Scotland. Hata hivyo utawala wa Scotland ulimkabidhi Charles l kwa wapinzani wake wa Uingereza na baada ya kupandishwa kizimbani na kuhukumiwa kifo, tarehe 30 Januari 1649 alinyongwa. Baada ya kuuawa Charles, Oliver Cromwell alitangaza serikali mpya huku akiwa rais, ambapo baada ya kutwaa madaraka kikamilifu alianza kukandamiza wapinzani wa Scotland na Ireland. Hata hivyo haukupita muda mrefu mara akataka kujitangaza kuwa mfalme wa Uingereza, lakini jeshi na bunge lilimpinga na kumfanya atangaze kujiuzulu urais.

Oliver Cromwell, rais wa kwanza na wa mwisho wa Uingereza

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, Damascus mji mkongwe na wa kihistoria wa Kiislamu ulikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Uingereza. Moja kati ya malengo makuu ya serikali za Ulaya wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia ilikuwa kuugawa utawala wa Othmania, lengo ambalo baadaye lilifanikiwa. Wakati utawala wa Othmania ulipokuwa ukigawanywa, maeneo yaliyokuwa chini ya utawala huo, nayo moja baada ya jingine yalidhibitiwa na Ufaransa na Uingereza, ambapo mji wa Damascus katika Syria ya leo, pia ulishambuliwa na katika siku kama ya leo ukakaliwa kwa mabavu. Hata hivyo kwa mujibu wa makubaliano ya hapo kabla kati ya London na Paris, Syria ukiwemo mji mkuu wake Damascus ilidhibitiwa na Ufaransa.

Haram ya Bibi Zainab mjini Damascus

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, Ufaransa na Uingereza ziliitangazia vita Ujerumani na kwa utaratibu huo Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikaanza. Baada ya jeshi la Ujerumani kuishambulia Poland, serikali ya Uingereza iliitumia Ujerumani ujumbe ikiitaka iondoke haraka katika maeneo iliyokuwa inayakalia kwa mabavu ya Poland. Hata hivyo Ujerumani ilipuuza takwa hilo la Uingereza. Baadaye Uingereza iliipatia Ujerumani makataa ya kuhitimisha operesheni zake za kijeshi. Hata hivyo Adolph Hitler kiongozi wa wakati huo wa Ujerumani ya Kinazi alikataa kutekeleza takwa hilo. Hatimaye katika siku kama ya leo, Uingereza na Ufaransa zikaitangazia vita Ujerumani. Sio Adolph Hiterl pekee ambaye hakutaraji kama Ufaransa na Uingereza zingeingia vitani kwa ajili ya Poand bali hata Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti pia hakutarajia hilo. 

Wakipanga ramani ya vita hivyo

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, nchi ya Qatar ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Qatar iliwahi kudhibitiwa na Ufalme wa Othmania. Hata hivyo kufuatia kudhoofika utawala huo, Qatar ambayo kuanzia mwaka 1882 na kuendelea kivitendo ilikuwa ikiendeshwa na Uingereza, mwaka 1916 nchi hiyo ya Kiarabu ilitambuliwa rasmi kuwa koloni la Muingereza. Hadi mwaka 1971 Qatar ilikuwa bado inakoloniwa na Uingereza ambapo mwaka huo huo, kwa ushirikiano wa viongozi wa eneo la pambizoni mwa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, likaundwa Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu. Hata hivyo mnamo Septemba mwaka huo huo, yaani 1971, Qatar ilijiondoa katika shirikisho hilo na kujitangazia uhuru.

Bendera ya Qatar