Nov 06, 2025 03:21 UTC
  • Alkhamisi, Novemba 6, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 15 Mfunguo Nane Jamad al-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 16 Novemba 2025.

Siku kama ya leo miaka 1409 iliyopita, Muhammad Abu Bakr mmoja wa masahaba watiifu wa Imamu Ali (as) na kamanda mashuhuri wa Kiislamu aliuawa shahidi katika vita na wanajeshi wa Amr bin al-As.

Muhammad Abu Bakr ambaye alikuwa ameteuliwa na Imamu Ali kuwa mtawala wa Misri alikabiliwa na uasi wa aina mbalimbali. Muawiya mtawala wa Bani Umayyah akitumia vibaya mazingira hayo, alimtuma Amr bin As huko Misri akiwa pamoja na wanajeshi 6,000. Muhammad bin Abu Bakr akiwa na wanajeshi 2000 alishindwa katika vita hivyo. Baada ya kutiwa mbaroni  aliunguzwa katika moto na kufa shahidi. 

Miaka 393 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Gustav wa Pili, mfalme wa Sweden.

Alizaliwa mwaka 1594 na alikalia kiti cha ufalme alipokuwa na umri wa miaka 17.

Umaarufu wake ulitokana na kushinda kwake katika vita vya kidini vya miaka 30 kati ya Waprotestant na Wakatoliki vya mwaka 1618 hadi 1648.

Gustav wa Pili

Siku kama ya leo miaka 212 iliyopita vita vya kwanza vya Simon Bolivar, shujaa wa uhuru wa mataifa ya Amerika ya Latini vya kukomboa nchi ya Venezuela kutoka kwa wakoloni wa Kihispania vilimalizika kwa ushindi.

Katika vita hivyo askari 6500 wa Simon Bolivar waliwashinda askari elfu 13 wa Uhispania. Hatimaye shujaa huyo wa Amerika ya Latini aliikomboa Venezuela kutoka utawala wa kikoloni wa Uhispania na kisha akashiriki katika mapambano ya kupigania uhuru ya nchi nyingine kadhaa za kusini mwa Amerika.

Simon Bolivar

Miaka 164 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Novemba 1860 Abraham Lincoln aliyekuwa mpinzani wa utumwa nchini Marekani, alishika madaraka na kuwa rais wa nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wake vita kadhaa vilitokea nchini Marekani na kupelekea kushindwa waliokuwa wakiunga mkono utumwa.

Abraham Lincoln aliuawa mwaka 1865 na mmoja wa wapinzani wa harakati za kupinga utumwa nchini Marekani.

Abraham Lincoln