Ijumaa, tarehe 7 Novemba, 2025
-
Leo Katika Historia
Leo ni Ijumaa tarehe 16 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Novemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 1166 iliyopita alifariki dunia Abu Hanifa Dinawari, mtaalamu wa fasihi, nujumu na mwanahisabati wa Kiislamu.
Abu Hanifa Dinawari ni mmoja wa wanafalsafa na wataalamu wa theolojia na wanahisabati wa zamani wa ulimwengu wa Kiislamu ambaye alizaliwa mjini Kermanshah yapata mwaka 222 Hijiria. Alikuwa msomi mashuhuri katika kipindi cha utawala wa Samanid huku akitabahari katika elimu za nahw, lugha, mantiki, nyota, elimu ya maumbo, uhandisi na kadhalika.
Mbali na hayo pia Abu Hanifa Dinawari alikuwa mtaalamu wa elimu ya mimea, historia, jografia, nyota, hisabati na kadhalika. Moja ya athari maarufu za mwanazuoni huyo ni pamoja na 'Kitaabun-Nabaat' ambacho kimejikita katika kutambua mimea, 'Al-Akhbaaru al-Twiwaal' 'Al-Faswaaha' 'Al-Shiiru wa Al-Shuaraa Wal-Buldaan.'

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, Madam Escudo Doska ambaye baadaye alikuwa maarufu kwa jina la Marie Curie alizaliwa huko Warsaw mji mkuu wa Poland.
Baba yake alikuwa profesa wa fizikia na baadaye Madam Curie alielekea Paris, Ufaransa kwa ajili ya kuendeleza masomo yake katika taaluma hiyo hiyo ya baba yake. Madam Curie alifunga ndoa na Pierre Curie mwanafikizikia wa Ufaransa wakati alipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Sorbonne.
Hatimaye mwanamama huyo alifanikiwa kuvumbua mada ya radium baada ya utafiti miaka mingi.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa Madam Curie alitunukiwa tuzo ya Nobel mara mbili katika taaluma za fizikia na kemia na aliaga dunia mwaka 1934.
Katika siku kama ya leo miaka 146 iliyopita, Leo Trotsky mmoja kati ya viongozi wakuu wa mapinduzi nchini Russia alizaliwa.
Alibaidishwa Siberia mara mbili katika zama za utawala wa Tsar kutokana na kujihusisha kwake na harakati za mapinduzi. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Russia, Trotsky alirejea nchini Russia. Hiyo ilikuwa mwaka 1917 na akapatiwa wadhifa wa Kamishna wa Masuala ya Kigeni. Mwaka mmoja baadaye akateuliwa kuwa Kamishna wa Vita ambapo baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani na Ujerumani wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, alianzisha mapambano dhidi ya wapinzani wa mapinduzi.
Hata hivyo baada ya kuaga dunia Lenin, mwanamapinduzi huyo alishindwa katika vita vyake na Joseph Stalin na mwaka 1925 alibaidishiwa Siberia na baadaye huko Uturuki. Hatimaye aliuawa mwaka 1940 huko Mexico na makachero wa Lenin.
Miaka 112 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Albert Camus mwandishi mashuhuri wa Ufaransa.
Licha ya kuwa familia yake ilikuwa masikini, lakini kutokana na kipaji, bidii pamoja na irada thabiti aliyokuwa nayo, Camus alifanikiwa kupata umashuhuri mkubwa. Mwandishi huyo wa Kifaransa ana vitabu vingi.
Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Firs Man, The Fall, The Stranger na A Happy Death.
Katika siku kama ya leo miaka 69 iliyopita vita vya Mfereji wa Suez vilimalizika baada ya uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa.
Vita hivyo vilianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia jangwa la Sinai na kufuatia mashambulizi ya askari wa miavuli wa Uingereza na Ufaransa katika eneo la mfereji huo.
Serikali hizo tatu zilizotajwa zilianzisha vita hivyo kufuatia hatua ya rais wa wakati huo wa Misri, Jamal Abdulnassir, kuutaifisha mfereji huo.

Na miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, wananchi kote nchini Iran walifanya maandamano makubwa wakipinga kuingia madarakani serikali ya kijeshi ya Jenerali Gollam Reza Azhari aliyekuwa kibaraka wa utawala fasidi wa Kipahlavi.
Katika maandamano hayo wananchi Waislamu wa Iran walitangaza azimio wakisema kuwa mabadiliko ya kimaonyesho na kubadilisha nafasi za vibaraka wa Marekani hakuwezi kuzuia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Siku hiyo pia Kiongozi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa ujumbe kwa mnasaba wa mauaji yaliyofanywa na utawala wa Shah dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu tarehe 13 Aban mwaka huo huo akiwaambia wananchi kwamba: “Ninyi taifa shujaa, mumethibitisha kwamba vifaru, mitutu ya bunduki na mikuki imepata kutu na kwamba haiwezekani kukabiliana na irada ya chuma ya wananchi.”
