Oct 03, 2017 03:59 UTC
  • Jumanne tarehe 3 Oktoba, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 12 Muharram 1439 Hijria sawa na 3 Oktoba 2017.

Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Muharram mwaka 61 Hijria msafara wa mateka wa familia ya Mtume Muhammad (saw) uliokuwa na wanawake na watoto wa mashahidi wa Karbala, uliwasili katika mji wa Kufa, nchini Iraq. Kiongozi wa msafara huo alikuwa Bibi Zainab (as) dada wa Imam Hussein bin Ali (as) pamoja na Imam Ali bin Hussein Sajjad (as), mtoto wa Imam Hussein (as). Imam Sajjad na Bibi Zaynab (as) walitekeleza majukumu yao kwa kufikisha ujumbe wa Imam Hussein kwa jamii ya Waislamu. Siku hiyo pia miili ya mashahidi wa Karbala ukiwemo mwili mtukufu wa mjukuu wa Mtume (saw) Imam Hussein ilizikwa siku mbili baada ya kuuawa na kuachwa jangwani. Mashahidi wa Karbala walizikwa na watu wa kabila la Banii Asad. Mwili wa Imam Hussein na mashahidi wote wa Karbala ilibakia kwa siku mbili bila ya kuzikwa kwani hakuna mtu aliyekuwa na ujasiri wa kuzika miili hiyo kutokana na hofu ya utawala dhalimu wa Banii Umayyah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo wanawake wa kabila la Banii Asad waliwahamasisha wanaume wao kuzika miili hiyo mitakatifu ya wajukuu wa Mtume na masahaba wa Imam Hussein (as).

Siku kama ya leo miaka 1344 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Imam Ali Zainul Abidin maarufu kwa lakabu ya Sajjad mwana wa Imam Hussein (as) na mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu S.A.W, aliuawa shahidi. Imam Zainul Abidin alizaliwa mwaka 38 Hijria huko katika mji wa Madina. Mtukufu huyo aliishi katika zama ambapo watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu walikuwa wakikabiliwa na masaibu mengi. Imam Sajjad A.S ambaye alikuwa mgonjwa wakati wa tukio la Karbala, baada ya harakati adhimu ya Imam Hussein, alibeba jukumu kubwa la kueneza ujumbe wa mapambano hayo na kuendeleza njia ya baba yake.

Miaka 85 iliyopita katika siku kama ya leo Iraq ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Iran iliiweka Iraq chini ya mamlaka yake mwaka 539 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (A.S). Iraq ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Iran hadi ardhi hiyo ilipokombolewa na Waislamu mwaka 642 Miladia. Iraq iliendelea kudhibitiwa na utawala huo wa kifalme hadi mwishoni mwa utawala wa Bani Ummayya na mji wa Baghdad ukachaguliwa kuwa makao makuu sambamba na kuingia madarakani utawala wa Bani Abbas.

Bendera ya Iraq

Tarehe 3 Oktoba miaka 75 iliyopita kombora la kwanza lililotengenezwa na mwanadamu lilirushwa angani. Werner von Braun alikuwa miongoni mwa wataalamu wa makombora wa Ujerumani ambao baada ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia jeshi la nchi hiyo lilimpa jukumu la kutengeneza kombora la kwanza. Tarehe 3 Oktoba mwaka 1942 kundi la wataalamu wa Ujerumani lilifanikiwa kurusha angani kombora hilo lililokuwa na urefu wa mita 14 na uzito wa karibu tani 13. Kombora hilo lilirushwa angani katika Bahari ya Baltic.

Werner von Braun

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, baada ya Imam Khomeini MA kuzuiwa kuendesha shughuli za kisiasa na kidini huko Iraq na kwa kuzingatia kuwa utawala wa zamani wa wakati huo wa Iraq ulikuwa ukikabiliana na juhudi na mapambano ya Imam Khomeini na kuweka vizuizi vikubwa, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliamua kuondoka Iraq na kuelekea Kuwait. Hata hivyo serikali ya Kuwait ilimzuia Imam kuingia nchini humo ili kulinda uhusiano wake na utawala wa Shah. Kufuatia hatua hiyo, siku kadhaa baadaye Imam Khomeini MA akaelekea uhamishoni nchini Ufaransa. Itakumbukwa kuwa, miamala na vitendo visivyo vya kibinadamu vya utawala wa Baath wa Iraq vilizusha hasira za wananchi wa Iran ambao walikuwa katika siku muhimu za kupambana na utawala dhalimu wa Shah hapa nchini.

Imam Khomeini akipelekwa uhamishoni