Jumapili, Oktoba 8, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 17 Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria, mwafaka na tarehe 8 Oktoba 2017 Miladia.
Siku kama ya leo, miaka 541 iliyopita, alifariki dunia Nurud Din Abdur-Rahman Jami, mtaalamu wa elimu ya irfani, malenga na fasihi maarufu wa Iran huko katika mji wa Herat, ambao wakati huo ulikuwa ni sehemu ya ardhi ya Iran huku leo ikiwa ni sehemu ya Afghanistan. Akiwa kijana mdogo alipata kusoma elimu ya msingi na ya juu mjini Herat na Samarkand huku akiwa hodari pia katika kusoma mashairi. Akiwa kijana alihesabika kuwa mmoja wa wataalamu wa elimu ya irfan na kwa ajili hiyo akaamua kushikamana na njia ya elimu hiyo na kuibukia kuwa mwanairfani mkubwa wa zama hizo. Alifanya safari kwenda Hijaz, Baghdad na maeneo mengine katika nchi za Kiarabu. Aidha msomi huyo alijulikana kuwa mpenzi mkubwa wa watu wa familia ya Mtume Muhammad (saw) na kutokana na kubobea sana katika elimu ya irfani, kamwe hakuwahi kuwasifu watawala, na badala yake alimsifu Mtume na watu wa familia yake. Vitabu vya ‘Baharestan’ ‘Nafahaatul-Ins’ ‘Shawaahidun-Nubuwwah’ na ‘Haft Orang’ ni miongoni mwa athari za Nurud Din Abdur-Rahman Jami.
Siku kama ya leo miaka 486 iliyopita alizaliwa Bahauddin al Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, faqihi na aalim mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Baalbek nchini Lebaon. Baba yake Sheikh Bahai alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa Lebanon ambaye alisafiri naye nchini Iran akiwa mtoto. Sheikh Bahai alitumia kipaji chake kikubwa kuweza kufikia daraja ya uanazuoni katika kipindi kifupi. Aalim huyo alipewa jina la Sheikhul-Islam kutokana na kipawa chake cha kielimu cha hali ya juu. Sheikh Bahai ameacha zaidi ya vitabu 88 alivyoviandika kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Baadhi ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyo wa Kiislamu ni kama vile Jame Abbasi, Kashkool kilichojumuisha riwaya na hadithi, Tashrih al Aflaq na vingine vingi alivyoviandika kuhusu masuala ya hisabati na kemia. Sheikh Bahai alifariki dunia mwaka 1030 Hijria huko Isfahan Iran.
Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, kimbunga kikali kiliikumba nchi ya Vietnam. Kimbunga hicho ambacho kililiathiri zaidi eneo la kusini mwa nchi hiyo, kiliharibu nyumba, miundombinu na mashamba. Kimbunga hicho kikubwa kilisababisha karibu watu laki tatu kufariki dunia.
Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, vilianza vita vya Balkan kwa ushiriki wa Bulgaria, Serbia na Ugiriki dhidi ya dola la Othmania. Mtawala wa Othmania kwa kipindi cha miaka kadhaa mtawalia alikuwa akipanua satwa yake katika maeneo ya magharibi mwa Asia, kaskazini mwa Afrika na mashariki mwa Ulaya. Katika kipindi hicho wimbi la kutaka kujitawala katika nchi zilizokuwa chini ya utawala huo wa Othmani, lilisababisha kuibuka vita vingi ambapo vita vya Balkan vilikuwa mojawapo. Sababu ya kuibuka vita hivyo vya Balkan ambavyo vilianza Oktoba 1911 ilitokana na hatua ya utawala wa Othmania kukataa kuzipatia uhuru nchi zilizokuwa chini yake kama vile, Serbia, Bulgaria, Ugiriki na Montenegro.
Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha rishta uliyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Pakistan. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa katika mji wa Muzaffarabad. Watu karibu elfu 90 walipoteza maisha na wengine 3,300,000 kubaki bila makazi.