Jun 15, 2025 02:16 UTC
  • Jumapili, 15 Juni, 2025

Leo ni Jumapili 19 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1446 Hijria sawa na 15 Juni 2025 Miladia.

Tarehe 15 Juni miaka 317 iliyopita katika siku kama ya leo harakati ya wapigania uhuru wa Scotland ilikandamizwa vikali na Uingereza. Uingereza daima imekuwa ikifanya jitihada za kuiunganisha Scotland na ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Hata hivyo harakati za mapambano za Wascotland zilipinga vikali suala hilo. Hata hivyo mwaka 1707 mabunge ya nchi hizo mbili yaliunganishwa. Suala hilo liliwakasirisha sana Wascotland walioanzisha harakati nyingine ya mapambano mbayo ilikandamizwa vikali katika siku kama ya leo hapo mwaka 1708. ***

 

Siku kama ya leo miaka 177 iliyopita sawa na tarehe 15 Juni 1848, Otto von Bismarck Kansela wa Ujerumani aliuchagua mji wa kihistoria na maarufu wa Berlin, kuwa mji mkuu wa nchi hiyo. Kuteuliwa mji wa Berlin kuwa mji mkuu wa Ujerumani, kulitokana na utekelezaji wa mpango wa kuziunganisha Ujerumani mbili, uliobuniwa na Kansela Bismarck. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Ujerumani iligawanyika katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Mwezi Septemba 1990 baada ya kuvunjwa ukuta wa Berlin, kuliandaliwa mazingira ya kuunganishwa pande hizo mbili, na hatimaye Berlin kurejea tena na kuwa mji mkuu wa Ujerumani.  ***

Otto von Bismarck Kansela

 

Miaka 107 iliyopita katika siku kama ya leo, Ayatullah Seyyed Mustafa Mojtahidi Kashani, mwanachuoni mashuhuri na Mujahidi mahiri alifariki dunia. Alizaliwa Kashan, mojawapo ya miji ya katikati ya Iran katika familia ya wanazuoni, na alikamilisha masomo ya elimu ya msingi kwa baba yake. Kisha akaenda Isfahan na kisha Najaf huko Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kimasomo ambapo akiwa huko alifaidika na elimu ya walimu wengi zaidi na hatimaye akaifikia daraja ya Ijtihad.Ayatullah Mustafa Kashani pia alikuwa na kipaji kikubwa cha ushairi na aliandika mashairi kwa Kiajemi na Kiarabu. Lakini sifa yake muhimu ilikuwa ni kupinga dhulma na haki. Mwanazuoni huyu alikuwa mmoja wa wapinzani wa dhulma na waungaji mkono wa mapinduzi ya kikatiba nchini Iran, na alipigana dhidi ya uingiliaji kati wa wakoloni wa Uingereza na Kirusi katika Iran na Iraq. Kwa mfano, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na kukaliwa kwa mabavu Iraq na Waingereza, Ayatullah Seyyed Mustafa Kashani sio tu alitoa fatwa ya Jihad pamoja na wanazuoni wengine, bali pia alishiriki katika mapambano dhidi ya wakoloni. 

Ayatullah Seyyed Mustafa Mojtahidi Kashani

 

Katika siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, Fazliddin Mohammadiev, mwandishi wa vitabu na mwandishi wa habari maarufu wa Tajikistan, alizaliwa huko Samarkand. Alianza kazi yake kama mwandishi wa gazeti la "Red Tajikistan" na baada ya kusoma katika Shule ya Kati ya Komsomol huko Moscow, alifikia nyadhifa muhimu katika magazeti ya Tajikistan na Kamati ya Sinema ya Tajikistan. Mohammadiev alikuwa mwandishi ambaye alionyesha maendeleo ya kijamii ya Tajikistan kwa kuzingatia. Kazi zake ni pamoja na hadithi fupi, riwaya fupi na riwaya ambazo mara nyingi huandikwa kwa nathari rahisi na safi na michezo ya kuchekesha.

 

Miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai" ilianzishwa baada ya kusainiwa makubaliano kati ya nchi za Urusi, Uchina, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Uzbekistan, " Lengo la kuanzishwa jumuiya hiyo lilikuwa ni kuongeza ushirikiano wa kiuchumi, kiutamaduni na usalama. Historia ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai inaanzia 1996, wakati nchi hizi, isipokuwa Uzbekistan, zilipoanzisha kile kinachoitwa mkataba wa "Shanghai 5" ili kuimarisha uaminifu na kuongeza usalama katika mipaka yao mirefu. Kwa kujiunga Uzibekistan na Shanghai 5, kundi hilo lliligeuka na Jumuiya ya  Ushirikiano ya Shanghai. Hii leo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, India, Pakistan, Afghanistan na Mongolia pia ni wanachama wa jumuiya hiyo.