Jumapili, 15 Oktoba, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 24 Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria, mwafaka na tarehe 15 Oktoba 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 475 iliyopita alizaliwa Abolfath Jalal al-Din Muhammad Akbar, mfalme mwenye nguvu wa silsila ya Teimurian nchini India. Mfalme huyo alikuwa maarufu kwa jina la Akbar Shah ambaye baada ya kufariki dunia baba yake Homayun, alichukua madaraka akiwa na umri wa miaka 13. Kwa kipindi cha miaka mitano aliongoza akiwa chini ya usimamizi wa Bairam Khan aliyekuwa na cheo cha naibu mtawala. Baada ya kushika madaraka kikamilifu alianza kupanua wigo wa utawala wake katika maeneo ya Bengal, Kashmir, Sindh, Punjab, Ahmednagar na Kandahar. Mfalme Abolfath Jalal al-Din Muhammad Akbar alikomboa kisiwa cha Dakan, kilicho kusini mwa India kutoka mikononi mwa Wareno huku akifanikiwa pia kuleta nidhamu nchini India. Akbar Shah alifariki dunia mwaka 1605 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 173 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Wilhelm Nietzsche. Baada ya kuhitimu masomo, Nietzsche alianza kufunza katika Chuo Kikuu cha Basel. Mwanafalsafa huyo alikuwa akipinga dini na misingi ya kimaadili na katika falsafa na mitazamo yake alikuwa akiamini nadharia ya "Superman", kwa maana ya mtu mwenye uwezo kupita kiasi. Nietzsche alikuwa akiamini kwamba, mtu mwenye uwezo kupita kiasi au Superman ni matokeo ya irada na matashi ya mwanadamu na huwa juu ya mema na mabaya yote. Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Beyond Good and Evil, The Birth of Tragedy na Thus Spoke Zarathustra. Katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wake Friedrich Wilhelm Nietzsche alipoteza mlingano wa kifikra na kufariki dunia mwaka 1900.
Siku kama ya leo miaka 167 iliyopita, alifariki dunia Hajj Mulla Muhammad Taqi Astarabadi, msomi mkubwa wa Kishia. Mulla Muhammad Ismail, alikuwa mmoja wa wasomi mashuhuri wa Kishia wa zama hizo. Alipata idhini ya kuwa mujtahid kutoka kwa Muhammad Taqi Bin Muhammad Rahim Tehran Isfahani maarufu kwa jina la 'Swahibul-Hidayatul-Mustarshidin' ambapo alichukua miaka 14 akisoma kwa maulama wakubwa wa miji ya Najaf na Karbala, Iraq. Hajj Mulla Muhammad Taqi Astarabadi alifariki dunia mwaka 1271 mjini Tehran baada ya kuibuka harakati za uasi mjini Gorgan.
Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita alifariki dunia Agha Muhammad Shah maarufu kwa jina la 'Agha Hashar Kashmiri' malenga na mwandishi mkubwa wa lugha ya Kiurdu. Alikuwa miongoni mwa Waislamu wa India ambaye alizaliwa mwaka 1296 Hijiria. Alianza masomo yake kwa kujifunza kusoma na kuhifadhi Qur'ani na kisha akajifunza lugha za Kiarabu na Kifarsi kutoka kwa walimu mashuhuri wa mji wa Varanasi nchini India. Baada ya muda, alianza kusoma mashairi na maonyesho ya uandishi ambapo maonyesho yake ya kwanza yaliitwa kwa jina la 'Aftab Mahabbat'. Katika uhai wake Agha Hashar Kashmiri aliendesha maonyesho 36, muhimu zaidi yakiwa yale yaliyopewa jina la 'Tab'iid Sina be Jangal' na ambayo yaliandikwa kwa lugha ya Kihindi.
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, mwakilishi wa Imam Khomeini (MA) na Imam wa Swala ya Ijumaa ya mji wa Kermanshah huko magharibi mwa Iran Ayatullah Ashrafi Isfahani, aliuawa shahidi na vibaraka wa kundi la MKO akiwa katika mihrabu ya ibada. Ayatullah Ashrafi Isfahani aliongoza wananchi wa Kermanshah katika harakati na mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Shah. Aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Imam wa Sala ya Ijumaa ya Kermanshah baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na aliuawa shahidi katika mihrabu akisalisha Swala ya Ijumaa.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Mustafa Swafai Khonsari, muhadhiri mkubwa wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha mjini Qum. Sayyid Mustafa Swafai Konsari alizaliwa mwaka 1321 Hijiria mjini Khonsar huku masomo yake ya msingi na elimu ya kati akisoma kwa baba yake. Kisha alisoma kwa Ayatullah Hairi Yazdi mjini Qum na kupata kutoka kwake cheo cha ijtihadi. Kadhalika Ayatullah Sayyid Mustafa Swafai Konsari alibahatika kuchukua ijaza ya ijtihadi kutoka kwa maraajii 19 wakubwa wa zama zake akiwemo Sayyid Abul-Hassan Isfahani, Ayatullah Sayyid Hussein Borujerdi, Agha Dhiyaa Iraqi, Sayyid Muhammad Hujjat, Sayyid Muhammad Taqi Khonsari, Muhammad Faidh na Mar'ashi Najafi. Ameacha vitabu vingi katika taaluma ya sheria za Kiislamu na nyanja nyingine nyingi.