Jumatano tarehe 18 Oktoba, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 27 Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria sawa na Oktoba 18, 2017
Miaka 150 iliyopita, ardhi ya Alaska ilidhibitiwa na Marekani. Alaska ni ardhi yenye upana wa karibu kilometa mraba milioni moja na laki tano, huko Amerika ya kaskazini magharibi, ambapo hii leo ni moja ya majimbo ya nchi hiyo. Hadi mwaka 1867 Miladia, Alaska ilikuwa ikidhibitiwa na Russia, hata hivyo katika kipindi hicho mfalme wa wakati huo wa Urusi ya zamani hakutilia maanani umuhimu wa ardhi hiyo na hivyo mwezi Oktoba mwaka 1867 Miladia akaamua kuiuza kwa Marekani. Ni vyema ifahamike kuwa, hii leo Alaska inahesabika kuwa moja ya majimbo tajiri sana ya Marekani ambapo mwaka 1960 kulivumbuliwa mafuta na kuanza kuchimbwa eneo hilo hadi leo.

Siku kama ya leo miaka 146 iliyopita alifariki dunia msomi wa Uingereza na mvumbuzi wa mashine ya kikokoteo (Calculator) kwa jina la Charles Babbage. Mwaka 1812 Miladia, Babbage aliasisi taasisi ya uchunguzi kwa ajili ya kuendeleza elimu ya hisabati na akiwa na miaka 24 akateuliwa kujiunga na taasisi ya ufalme ya Uingereza. Ni baada ya hapo ndipo akaanzisha harakati ndefu za utafiti wa kuunda mashine hiyo ya hesabu ambapo hadi kufikia mwaka 1833 Miladia akafanikiwa kuvumbua chombo hicho ambacho kilikuja kuwa mashuhuri kwa jina la Babbage. Baada ya hapo karne moja baadaye wasomi mbalimbali waliifanyia marekebisho muhimu mashine hiyo sanjari na kuifanya itumie nishati ya umeme. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Charles Babbage akatambuliwa kwa jina la baba wa kikokoteo (Calculator).

Miaka 95 iliyopita katika siku kama ya leo, redio ya BBC ilasisiwa huko Uingereza. Redio ya BBC awali ilikuwa ya mtu binafasi, lakini ilipofika mwaka 1927, redio hiyo ikawa chini ya usimamizi wa serikali na hivyo kuwa katika kalibu ya redio za serikali ya Uingereza. Bajeti ya redio za BBC ambazo zinatangaza kwa lugha mbalimbali za dunia inadhaminiwa na serikali ya Uingereza. Pamoja na kuwa BBC inadai kwamba haipendelei upande wowote katika matangazo yake, lakini katika kipindi cha nusu karne ya hivi karibuni, chombo hicho cha kupasha habari kimegeuka na kuwa wenzo wa propaganda wa serikali ya Uingereza na hivyo kuiandalia London uwanja wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, msomi aliyegundua umeme kwa jina la Thomas Edison alifariki dunia. Edison alizaliwa mwaka 1847 huko Marekani. Thomas Edison hakuwa na taalumu yoyote kutoka chuo kikuu bali ni tafiti na majaribio yake mengi ndiyo yaliyopandisha juu kiwango chake cha elimu na maarifa. Akiwa kijana, Edison aliasisi maabara moja ya masuala ya kemia na kufanya majaribio makubwa katika maabara hiyo. Bidii ya msomi huyo ilimuwezesha kuvumbua mambo mengi ambapo muhimu kati ya hayo ni hatua yake ya kuvumbua umeme, kutengeneza lampu na gramafoni au santuri.
