Oct 20, 2017 08:44 UTC
  • Ijumaa 20 Oktoba 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 29 Muharram mwaka 1439 Hijria sawa na tarehe 20 Oktoba 2017.

Siku kama ya leo miaka 536 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria wa Kiislamu Muhammad Heravi katika mji wa Herat nchini Afghanistan. Heravi alizaliwa katika familia mashuhuri kwenye mji wa Balkh huko kaskazini mwa Afghanistan ingawa aliishi kipindi kirefu katika mji wa Herat. Muhammad Haravi aliheshimiwa mno na waziri msomi wa utawala wa kizazi cha Gurkanian, Amir Alishah Navai, ambaye alikuwa akiwaenzi na kuwaheshimu mno wasomi na wanazuoni. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwanahistoria huyo wa Kiislamu ni kile cha "Tarikh Raudhatu Safa" ambacho kinazungumzia historia ya dunia nzima tangu kuumbwa kwake hadi kipindi cha msomi huyo. 

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, inayosadifiana na 20 Oktoba 1827 kulitokea vita vya majini katika ghuba ndogo ya Navarone iliyoko kaskazini mwa bahari ya Mediteranean. Kwenye vita hivyo, majeshi ya Uingereza, Russia na Ufaransa ambayo yalikuwa yakiiunga mkono Ugiriki, yakitumia meli za kivita yalishambulia meli za dola ya Othmania. Nchi hizo tatu za Ulaya zilifanikiwa kuziangamiza kabisa meli 60 za kivita za dola la Othmania na kuwateka nyara wanajeshi elfu sita.

Vita vya baharini vya Navarone

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, alizaliwa John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na alijifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Columbia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How We Think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture" John Dewey alifariki dunia mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 92.

John Dewey

Siku kama ya leo miaka 6 iliyopita, dikteta wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alikamatwa na wanamapinduzi karibu na mji wa bandari wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa. Gaddafi aliuawa baada ya miezi kadhaa ya mapigano na wanamapinduzi ambapo jeshi lake liliwaua maelfu ya wananchi hususan katika miji ya Benghazi na Tripoli. Gaddafi ambaye aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 42 alizaliwa mwaka 1942. Aliingia madarakani mwaka 1969 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani mfalme Mohammad Idris al-Sanusi.

Muammar Gaddafi