Oct 22, 2017 23:10 UTC
  • Jumatatu tarehe 23 Oktoba, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 3 Safar 1439 Hijria sawa na 23 Oktoba 2017.

Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa.

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilitokea katika mji wenye jina kama hilo la al-Alamein huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani. Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika. Amani kamili ilipatyikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la manazi wa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Vita vya kihistoria vya Alamein

Miaka 40 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Ayatullah Sayyid Mustafa Khomeini mtoto wa Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa shahidi kufuatia njama zilizofanywa na vikosi vya usalama vya utawala wa Shah akiwa nyumbani kwake huko Najaf, moja kati ya miji mitukufu ya Iraq. Al Haj Mustafa Khomeini alizaliwa mwaka 1309 Hijria shamsiya katika mji mtakatifu wa Qum na baadaye akajiunga na chuo cha elimu ya dini cha mji huo kwa jili ya masomo ya juu baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Alikuwa hodari mno na alifikia daraja ya juu ya kielimu ya Ijtihadi akiwa na umri wa miaka 27. Ayatullah Mustafa Khomeini alikuwa pamoja na baba yake Imam Khomeini katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya utawala wa Shah.

Ayatullah Sayyid Mustafa Khomeini

Siku kama hii ya leo miaka 34 iliyopita, wanajeshi 241 wa Marekani na 58 wa Ufaransa waliangamizwa katika mashambulio ya kujitolea mhanga ya Waislamu wa Lebanon dhidi ya makao ya vikosi vamizi vya Marekani na Ufaransa huko Beirut mji mkuu wa Lebanon. Wiki kadhaa kabla ya mashambulizi hayo, wanajeshi wa Marekani, Ufaransa, Uingereza na Italia waliingia Beirut ili kuwaunga mkono Mafalanja katika vita vya ndani vya Lebanon. Kuweko kwa vikosi hivyo vya nchi kadhaa za Magharibi huko Beirut kulikuwa ni sawa na kuunga mkono kwa njia isiyo ya moja kwa moja uchokozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Lebanon. Hata hivyo msimamo wa kishujaa ulioonyeshwa na Waislamu wanamapinduzi wa Lebanon dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani na Ufaransa huko Beirut, uliwalazimisha askari vamizi kuondoka kwa madhila huko Lebanon.

Na miaka 145 iliyopita, aliaga dunia Theophile Gautier, malenga na mwandishi wa Kifaransa. Gautier alizaliwa mwaka 1811 na kuhitimu masomo yake huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa. Theophile Gautier kwa muda fulani alikuwa mwandishi wa gazeti na alikuwa na hamu kubwa ya kuwa mchoraji au mwanamuziki. Lakini hatimaye alijifunza fasihi hususan mashairi na kuacha athari maarufu katika uwanja huo.

Theophile Gautier,