Oct 25, 2017 02:23 UTC
  • Jumatano tarehe 25 Oktoba, 2017

Jumatano tarehe 5 Safar 1439 Hijria inayosadifiana na 25 Oktoba, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1376 iliyopita, Ruqayyah binti mchanga wa Imam Hussein bin Ali (as) alikufa shahidi akiwa huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyya. Ruqayyah ambaye pia anajulikana kwa jina la Fatima binti Hussein (as), alikuwa binti wa mwisho wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kutoka kwa mkewe, Ummu Is’haq binti Twalha. Wanahistoria wanasema mtoto huyo alikuwa na umri wa miaka 3, 4 au 7. Mtoto huyo alikuwa akimpenda sana Imam Hussein na aliandamana naye pamoja na familia yake katika medani ya Karbala. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, ndugu na masahaba wa Imam, Ruqayya alikamatwa mateka na askari wa Yazid akiwa pamoja na watu wengine wa Nyumba ya Mtume na kupelekwa Sham. Huko alikuwa akilia mchana usiku. Wahistoria wanasema mtawala Yazidi aliamuru kichwa cha Imam Hussein kipelekwe na kutupwa mbele ya binti huyo mchanga ambaye alilia na kuzimia kisha akakata roho.

Siku kama ya leo, miaka 206 iliyopita, alizaliwa Évariste Galois, mtaalamu wa hesabati wa nchini Ufaransa, karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris. Kufikia umri wa miaka 12, Galois hakufunzwa na mtu yeyote isipokuwa mama yake na alianza kusoma vitabu vya jiometri na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa.  Galois aliuawa  akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832 baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani.

Évariste Galois

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, alizaliwa Pablo Picasso mchoraji mashuhuri wa Kihispania. Picasso alikuwa mwasisi wa harakati ya Cubist ambayo ilienea kwa kasi kubwa miongoni mwa wachoraji wa Ufaransa. Pablo Picasso alichora picha nyingi na daima alikuwa akifanya juhudi za kuendeleza harakati hiyo. Mchoro wa 'The Girls of Avignon' wa mchoraji huyo ndio uliokuwa mwanzo wa mtindo wa Cubism na kazi kubwa zaidi ya Picasso katika mtindo huo ni 'Guernica'. Katika mchoro huo Pablo Picasso anaonesha hofu iliyompata kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za Ujerumani na Italia dhidi ya mji wa Guernica. Picasso alifariki dunia Aprili mwaka 1973.

Pablo Picasso

Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Halat, malenga, mchekeshaji na mtaalamu wa fani ya tarjama nchini Iran. Akiwa na umri wa miaka 16 Halat alianza kusoma mashairi na kuwa hodari mkubwa katika uwanja huo. Tarjama ya maneno ya Mtukufu Mtume Muhammad (swa) na Imam Ali (as) ni miongoni mwa athari zenye thamani kubwa za Abul-Qasim Halat. Mbali na vitabu hivyo, Halat aliandika majmui ya mashairi katika fani mbalimbali, baadhi zikihusu masuala ya akhlaqi na Irfani. Aidha Abul-Qasim Halat alikuwa mtaalamu pia katika lugha nne za Kifarsi, Kingereza, Kifaransa na Kiarabu. 

Abul-Qasim Halat