Nov 01, 2017 04:32 UTC
  • Jumatano 1 Novemba, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 12 Safar 1439 Hijria sawa na tarehe Mosi Novemba, 2017.

Siku kama ya leo, miaka 103 iliyopita, serikali ya wakati huo ya Iran ilitangaza kutofungamana na upande wowote katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Hata hivyo udhaifu wa kisiasa wa watawala wa wakati huo, matatizo ya ndani, matatizo ya kivita na kupenda kujitanua kwa nchi zilizokuwa zikipigana katika vita hivyo ni mambo yaliyopelekea nchi hii kwenda kinyume na ahadi yake ya kutofungamana na upande wowote katika vita hivyo. Ni kutokana na hali hiyo ndipo Iran ikajikuta katika hujuma na mashambulizi ya majeshi ya Uingereza, Urusi ya zamani na jeshi la Othmania na kuisababishia hasara kubwa.

Vita vya Kwanza vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita utawala wa kifalme nchini Uturuki ulihitimishwa rasmi na Ataturk. Baada ya kumalizika kwa Vita vya Kwanza vya Dunia sanjari na kudhoofika na kupoteza ushawishi wa utawala wa Othmania, Atatürk aliamua kuvunja utawala huo wa kifalme na kutwa uongozi. Hata hivyo haikuwa rahisi kwa Mustafa Kemal Atatürk kumaliza utawala wa kifalme wa Othmania ambao ulikuwa na misingi ya kidini. Hivyo mwanzoni alitenganisha baina ya utawala wa kisultani na cheo cha ukhalifa wa Waislamu na tarehe Mosi mwaka 1922 akavunja rasmi utawala wa kifalme huku cheo cha ukhalifa kikibakia kama cheo cha heshima tu. Suala hilo liliharakisha kuporomoka kwa utawala wa kifalme wa Othmania uliodumu kwa kipindi cha miaka 600. Baada ya kuporomoka utawala huo, uliundwa utawala wa Jamhuri na wa kisekulari hapo tarehe 29 Oktoba mwaka 1923.

Mustafa Kemal Atatürk

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, vilianza vita vya ukombozi wa Algeria baada ya kuundwa Harakati ya Ukombozi wa Algeria chini ya uongozi wa Ahmed ben Bella. Baada ya kupita miaka 132 ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria, hatimaye mwaka 1962 mapambano ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Algeria yalizaa matunda na nchi hiyo kujipatia uhuru wake. Baada ya kutangazwa uhuru wa Algeria, Ahmed ben Bella alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Utawala wa Ahmed ben Bella ulidumu kwa miaka mitatu tu, kwani ulipofika 1965 alipinduliwa na Kanali Houari Boumediene aliyekuwa waziri wake wa ulinzi.

Ahmed ben Bella

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Aban 1359 Hijria Shamsia, alikamatwa mateka Mhandisi Muhammad Jawad Tondguyan Waziri wa Mafuta wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na maafisa kadhaa wa wizara hiyo. Operesheni hiyo ilifanywa na majeshi ya Iraq mwezi mmoja tu baada ya majeshi ya Iraq kushambulia ardhi ya Iran. Mhandisi Tondguyan alikwenda kusini mwa Iran kwa shabaha ya kukagua visima na viwanda vya mafuta katika eneo hilo.

Mhandisi Muhammad Jawad Tondguyan

 

Tags