Nov 02, 2017 04:03 UTC
  • Alkhamisi tarehe Pili Novemba

Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Safar 1439 Hijria sawa na Novemba Pili, 2017

Siku kama ya leo miaka 1138 iliyopita alifariki dunia mtaalamu mashuhuri wa hadithi wa Kiislamu Abu Abdulrahman Ahmad bin Shuaib Nasaii maarufu kwa jina la Sheikhul Islam. Nasaii alizaliwa mwaka 220 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Khorasan huko kaskazini mwa Iran na akaelea nchini Misri akiwa kijana. Huko alipata elimu ya fiqhi na hadithi na akaanza kufunza taaluma hizo. Baadaye Sheikhul Islam Nasaii aliekele Damascus, Syria ambako alibainisha sifa na maadili ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake) na kupigwa mara kadhaa na wapinzani wa Ahlul Bait. Hatimaye alielekea Hijaz na kuishi mjini Makka. Nasaii ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Khasaisu Amirul Muuminina Ali" na kile cha "Sunanun Nasai" ambacho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya hadithi vya Kiislamu. 

 

Siku kama ya leo miaka 1069 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa fasihi, fiqhi na tafsiri ya Qurani Muhammad Azhari Harawi. Alizaliwa mwaka 282 Hijria katika eneo la Harat nchini Afghanistan. Harawi alitekwa nyara na Waarabu wa jangwani akiwa safarini kuelekea Makka kwa ajili ya ibada ya hija na huko alijifunza lahaja asilia ya lugha ya Kiarabu ambayo aliitumia katika vitabu vyake. Mtaalamu huyo wa lugha ameandika vitabu vingi vya tafsiri na hadithi. Kitabu chake muhimu zaidi ni kile cha "Tahdhibul Lugha."

Miaka 101 iliyopita katika siku kama hii ya leo Sharif Hussein mtawala wa Makka na Madina alijitangaza kuwa sultani wa nchi zote za Kiarabu. Sharif Hussein alianzisha mapambano dhidi ya serikali ya Othmania tarehe 5 mwezi Juni mwaka huo baada ya kuchochewa na Uingereza. Utawala wa Othmania wakati huo ulikuwa ukipigana katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Uingereza ilimuahidi Sharif Hussein kuwa baada ya kumalizika vita hivyo itamtambua moja kwa moja kama mfalme wa Saudi Arabia. Hata hivyo Uingereza haikutekeleza ahadi hiyo kwa Sharif kwa sababu London ilikuwa ikiuunga mkono ukoo wa Aal Saud.  

Shariff Hussein

Miaka 100 iliyopita mwafaka na tarehe Pili Novemba mwaka 1917 azimio la Balfor lilitangazwa. Azimio hilo ambalo liliwasilishwa na Arthur Balfor, Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Uingereza liliandaa uwanja wa kuasisiwa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hii ni kwa sababu Palestina wakati huo ilikuwa chini ya himaya ya serikali ya kikoloni ya Uingereza. Azimio la Balfor lilibainisha kuwa serikali ya Uingereza imeafiki kuasisiwa serikali ya Kiyahudi huko Palestina na kwamba itafanya juhudi zote kuhakikisha kuwa serikali ya aina hiyo inaundwa. Hatimaye utawala wa Kizayuni wa Israel ulitangazwa rasmi huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu miaka 31 baada ya kutangazwa azimio hilo la kikoloni mwaka 1948 chini ya uungaji mkono wa Uingereza na Marekani.

Arthur Balfour

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita Indonesia ilipata uhuru baada ya kukoloniwa kwa karne tatu na nusu na Uholanzi. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa siku hiyo kati ya Uholanzi na wapigania uhuru wa Indonesia chini ya uongozi wa Dakta Ahmad Sukarno na Ahmad Hatta, ilisisitizwa kuwa wanajeshi wa Uholanzi waondoke huko Indonesia nchi ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Nedherlands-Indie.  

Indonesia iko kusini mashariki mwa bara Asia huku ikiwa na ukubwa wa kilomita mraba karibu milioni mbili. Indonesia ina watu karibu milioni 250 ambapo asilimia 88 ya jamii hiyo ni Waislamu na kwa msingi huo nchi hiyo inahesabiwa kuwa nchi ya Kiislamu yenye idadi kubwa zaidi ya watu.

Saudi bin Abdulaziz

Na siku kama ya leo miaka 53 iliyopita Saud bin Abdul Aziz, mfalme wa pili wa Saudi Arabia aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyofanywa na ndugu yake, Faisal bin Abdul Aziz. Faisal alikuwa waziri mkuu wa Saud bin Abdul Aziz na alitumia ujanja kwa ajili ya kupata uungaji mkono wa idadi kadhaa ya wanafamilia wa kizazi cha Aal Saud na maulama wa Kiwahabi. Wakati Mfalme Saud alipokwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, Faisal aliwapa wafuasi wake ndani ya kizazi cha Aal Saud nyadhifa muhimu kama uongozi wa Gadi ya Taifa na kwa njia hiyo akawa amedhibiti nchi. Mapinduzi hayo yaliungwa mkono na wanasiasa na viongozi wa kidini wa Saudi Arabia na Faisal akawa mfalme mpya wa nchi hiyo. Miaka 11 baadaye Mfalme Faisal bin Abdul Aziz mwenyewe pia aliuawa na ndugu yake. Vita vya kuwania madaraka vimekuwepo siku zote ndani ya kizazi cha watawala wa Aal Saud huko Saudi Arabia.