Jumamosi, Novemba 4, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe 15 Mfunguo Tano Safar 1439 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe 4 Novemba mwaka 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 455 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Shahtahmasebi wa Kwanza aliyekuwa mmoja wa wafalme wa ukoo wa Safavi aliaga dunia na Shah Ismail wa Pili akakalia kiti cha uongozi. Shahtahmasebi Safavi alishika hatamu za uongozi na kuwa mfalme wa Iran akiwa na umri wa miakka 11. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 65 baada ya kuugua. Shatahmasebi aliongoza Iran akiwa mfalme kwa muda wa miaka 54.
Miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufalme wa Austria-Hungary ulisalimu amri kwa waitifaki ikiwa ni wiki moja tu kabla ya kufikia tamati Vita vya Kwanza vya Dunia. Utawala huo ambao ndio uliokuwa umeanzisha vita, ulikuwa ukihesabiwa kuwa muitifaki muhimu wa Ujerumani. Hata hivyo kutokana na kushindwa mara nyingi katika vita, ulikubaliana na masharti ya kuacha vita. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Austria-Hungary uligawanywa kwa nchi kadhaa na ukoo wa Habsburg uliokuwa ukitawala ukasambaratika.
Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, kufuatia kuongezeka upinzani dhidi ya utawala wa kikomonisti huko Hungary, Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti liliikalia kwa mabavu nchi hiyo. Baada ya kifo cha Joseph Stalin, kiongozi dikteta wa Umoja wa Kisovieti 1953 na kupatikana anga ya wazi kwa kiwango fulani kupitia kwa mrithi wake Nikita Khrushchev, baadhi ya nchi za Kikoministi za Ulaya zilitaka kuweko anga ya wazi zaidi. Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Magharibi vilikuwa vikiwashajiisha wananchi na kuwataka waanzishe harakati na mapambano. Hapo ndio wananchi wa Hungary walipoanzisha harakati dhidi ya utawala wa nchi yao na kuwauwa Wakoministi kadhaa.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, askari vibaraka wa utawala wa Shah uliokuwa ukitawala Iran waliivamia nyumba ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini mjini Qum na kumtia mbaroni. Baada ya kumhamishia mjini Tehran, utawala wa Shah ulimbaidishia Imam Khomeini nchini Uturuki. Utawala wa Shah uliamua kufanya hivyo kutokana na uungaji mkono wa Imam Khomeini kwa harakati za mapambano za wananchi Waislamu wa Iran za kutaka kujitawala, uhuru na kutetea thamani za kidini. Lengo la kumpeleka uhamishoni Imam Khomeini lilikuwa kusimamisha mapambano yake na wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala huo, kwani utawala wa Shah ulitambua kwamba kuwepo Imam nchini kunawaamsha wananchi dhidi ya utawala huo wa kidikteta.
Miaka 39 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 13 Aban mwaka 1357 Hijria Shamsia, kulifanyika maandamano makubwa ya wanafunzi na wanachuo mjini Tehran. Maandamano hayo ya yalikandamizwa vibaya na askari wa utawala wa Shah na kusababisha umwagaji damu mkubwa. Katika siku kama hii ambayo ilisadifiana na kumbukumbu ya kubaidishwa Imam Khomeini huko Uturuki, kundi kubwa la wanafunzi na wanachuo, wakiwa na lengo la kulaani kitendo hicho cha mfalme Shah walikusanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran. Askari wa utawala wa Shah walishambulia kundi hilo la wanachuo na wanafunzi na kuwauwa shahidi wanafunzi na wanachuo wengi. Tarehe 13 Aban ina umuhimu mkubwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, na ndio maana imepewa jina la "Siku ya Mwanafunzi."
Siku kama ya leo 38 iliyopita, wanafunzi na wanachuo wa Tehran walifanya maandamano makubwa katika mji huo kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kubaidishiwa nchini Uturuki Imam Khomeini MA na kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu kuuawa wanafunzi na wanachuo wa Iran. Mauaji hayo yalifanywa na vikosi vya usalama vya utawala wa Shah. Wanafunzi na wanachuo kadhaa wa Kiislamu walioshiriki kwenye maandamano hayo ambao walikuwa wakijulikana kama Wafuasi wa Sera za Imam, waliuvamia ubalozi wa Marekani mjini Tehran, ambao ulikuwa pango la ujasusi dhidi ya wananchi wa Iran. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 22 Waziri Mkuu wa wakati huo wa utawala ghasibu wa Israel Yitzhak Rabin aliuawa kwa kupigwa risasi na Mzayuni mwenye misimamo mikali. Rabin alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel kwa tiketi ya chama cha Leba katika mwaka 1974 na kuongoza hadi 1977. ambapo alilazimika kujiuzulu kutokana na ubadhirifu wa mali ya umma. Alichaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Israel mwaka 1992 na kudumisha mazungumzo eti ya amani ya Mashariki ya Kati. Mauaji ya Yitzhak Rabin yaliyofanywa na Myahudi mwenzake Yigal Amir ni mfano wa wazi wa hitilafu kubwa zilizoko kati ya viongozi wa utawala unaoikalia Palestina kwa mabavu wa Israel. Ni muhimu kukumbusha kuwa, Yitzhak Rabin alikuwa miongoni mwa makamanda wa makundi ya kigaidi ya Kizayuni.***