Jumatatu tarehe 6 Novemba, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 17 Safar 1439 Hijria sawa na 6 Novemba, 2017.
Siku kama ya leo miaka 543 iliyopita, alizaliwa Muhammad Mustafa Imad, maarufu kwa jina la Abus-Su’ud, faqihi na mfasiri wa Kiislamu katika kijiji cha Mudares karibu na mji wa Istanbul huko Uturuki. Baada ya kuhitimu masomo yake, Abus-Su’ud alijishughulisha na ufundishaji na kufanya kazi ya ukadhi mjini Istanbul, kazi aliyoendelea nayo hadi mwisho wa uhai wake. Abus-Su’ud alikuwa hodari katika masuala mbalimbali ya kijamii na aliweza kuandaa sheria za kiidara kwa mujibu wa dini ya Kiislamu katika utawala wa Othmania. Mbali na kuzungumza lugha ya Kituruki, alizungumza pia lugha za Kifarsi na Kiarabu. Msomi huyo wa Kiislamu ametunga mashairi kadhaa kwa lugha hizo. Miongoni mwa vitabu vya Abus-Su’ud ni pamoja na ‘Irshadul-Aqlis-Saliim’ ‘Dua Nameh’ ‘Qanun Nameh’ na ‘Mafrudhaat'.

Miaka 385 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Gustav wa Pili, mfalme wa Sweden. Alizaliwa mwaka 1594 na alikalia kiti cha ufalme alipokuwa na umri wa miaka 17. Umaarufu wake ulitokana na kushinda kwake katika vita vya kidini vya miaka 30 kati ya Waprotestant na Wakatoliki vya mwaka 1618 hadi 1648.
Siku kama ya leo miaka 204 vita vya kwanza vya Simon Bolivar, shujaa wa uhuru wa mataifa ya Amerika ya Latini vya kukomboa nchi ya Venezuela kutoka kwa wakoloni wa Kihispania vilimalizika kwa ushindi. Katika vita hivyo askari 6500 wa Simon Bolivar waliwashinda askari elfu 13 wa Uhispania. Hatimaye shujaa huyo wa Amerika ya Latini aliikomboa Venezuela kutoka utawala wa kikoloni wa Uhispania na kisha akashiriki katika mapambano ya kupigania uhuru ya nchi nyingine kadhaa za kusini mwa Amerika.
Siku kama ya leo miaka 184 iliyopita, alizaliwa Sheikh Abdul Rahim Sultanul-Qurrai Tabrizi, qaari mkubwa wa Qur’ani Tukufu na mmoja wa walimu mashuhuri wa fani ya qiraa, huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kujifunza fani hiyo kutoka kwa baba yake, Sultanul-Qurrai Tabrizi alifahamiana na Sheikh Shamil Daghestani na kushirikiana naye. Wakati Sheikh Shamil Daghestani alipoandaa jeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi, Sultanul-Qurrai alifanya safari kuelekea Daghestani ili kushiriki katika harakati hiyo. Baadaye alirejea Tabriz na kuanzisha hawza ya kisomo cha Qur’ani na ni wakati huo ndipo akapewa lakabu ya Sultanul-Qurrai. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na ‘Risala katika elimu ya Tajwidi’ Sultanul-Qurrai alifariki dunia mwaka 1336 Hijiria mjini Tabriz.
Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Novemba 1860 Abraham Lincoln aliyekuwa mpinzani wa utumwa nchini Marekani, alichukua madaraka na kuwa rais wa nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wake vita kadhaa vilitokea nchini humo na kupelekea waliokuwa wakiunga mkono utumwa kushindwa. Abraham Lincoln aliuawa mwaka 1865 na mmoja wa wapinzani wa harakati za kupinga utumwa nchini Marekani.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita wafanyakazi wa redio na televisheni ya Iran walianza mgomo wakipinga utawala wa Shah. Mgomo huo ulifanyika kwa shabaha ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya utawala wa Shah na kuharakisha mwenendo wa kuipindua serikali yake. Siku hiyo hiyo maafisa wa jeshi la Shah walishambulia taasisi za magazeti na vyombo vya habari na kuwatia nguvuni waandishi kadhaa. Hatua hiyo ilipelekea kusitishwa uchapishaji wa magazeti yaliyokuwa yakichapishwa kwa wingi nchini.