Jumatano tarehe 8 Novemba, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 19 Safar 1439 Hijria, sawa na tarehe 8 Novemba, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1268 iliyopita yaani tarehe 19 Safar mwaka 171 Hijria alizaliwa Abu Ma'ashar Balkhi mmoja kati ya wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya nujumu wa Kiirani. Alielekea Baghdad na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Abu Ma'ashar Balkhi alitumia vyanzo vya lugha za Kiarabu, Kihindi, Kigiriki na Kisiriani kwa ajili ya kupata elimu ya nujumu na kuwa miongoni mwa wanajimu wakubwa katika zama zake. Kazi zake katika taaluma hiyo zilitumiwa kwa karne kadhaa katika ulimwengu wa Kiislamu na Kimagharibi hata baada ya kufariki kwake dunia. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalidul al Saghirah.
Siku kama ya leo miaka 361 iliyopita, alizawa Edmond Halley, mtaalamu wa nyota wa nchini Uingereza. Halley alisoma katika kitengo cha Queen kilicho chini ya chuo kikuu cha Oxford, nchini humo na kuanza kujishughulisha na masuala ya utafiti wa nyota akiwa kijana mdogo, huku akifanya safari kuelekeaa kusini mwa dunia ya Bahari ya Atlantic. Edmond Halley alichukua muda mwingi katika kutalii nyota ambapo alipata kufahamu kwamba, kama ilivyo kwa sayari, nyota nazo zina mzunguko wake maalumu. Mwaka 1704 alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Oxford, huku akiarifishwa kuwa mtaalamu wa masuala ya nyota mwaka 1720. Halley alifariki dunia mwaka 1742 wakati akijishughulisha na masuala ya nyota.
Tarehe 8 Novemba miaka 343 iliyopita, alifariki dunia John Milton, malenga wa Kiingereza. Kazi za kwanza za ushairi za John Milton zilijulikana kwa majina ya Roho na Huzuni na Roho ya Furaha. Kazi nyingine ya uandishi ya John Milton ni ile aliyoipa jina la Paradise Lost. Malenga Milton alikuwa akitetea suala la kutenganishwa serikali na kanisa, kuweko uhuru wa kuabudu na wakati huo huo aliunga mkono uchujaji wa taarifa uliokuwa ukifanywa na serikali.
Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita sawa na tarehe 8 Novemba mwaka 1895, miale ya X iligunduliwa na Wilhem Conrad Rontgen, mwanafizikia na mwanasayansi maarufu wa Ujerumani. Mtaalamu huyo mwaka 1901 alitunukiwa tuzo ya Nobel kwa kufanikiwa kugundua miale hiyo. Kwa kuwa hakutambua miale aliyoigundua, Rontgen aliamua kuipa jina la X. Miale hiyo hupenya kwa urahisi katika mwili wa mwanadamu na kwa ajili hiyo ni njia nzuri zaidi ya kuchukua taswira ya viungo au picha ya X-ray inayotumiwa kujua sehemu za ndani ya mwili zilizodhurika au kuvunjika.
Na siku kama ya leo miaka 117 iliyopita alizaliwa Bi Margaret Mitchell mwandishi wa Kimarekani huko Atlanta katika jimbo la Georgia nchini humo. Baba yake Bi Mitchell alikuwa wakili wa mahakama. Kwa muda fulani alisomea fani ya udaktari, lakini baadaye alilazimika kukatisha masomo hayo kutokana na majonzi aliyokuwa nayo kufuatia kifo cha baba yake. Margaret allianza kazi ya uandishi akiwa na miaka 22. Alizidi kupata umashuhuri baada ya kuchapisha riwaya yake aliyoiita kwa jina la "Gone with The Wind."