Alkhamisi tarehe 9 Oktoba, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Safar 1439 Hijria sawa na Oktoba 9, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume na masahaba zake watiifu ambao walijisabilia roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika ardhi ya Karbala.

Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, alizaliwa Ivan Turgenev mwandishi mashuhuri wa riwaya wa Russia. Turgenev alisomea fasihi ambapo vitabu vyake vingi vilitetea sana uhuru na haki za wanavijiji.
Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita, alizaliwa nchini Pakistan Allama Muhammad Iqbal Lahori mwandishi, mwanafikra na malenga mzungumza lugha ya Kifarsi. Baada ya kumaliza masomo yake ya juu, Iqbal Lahori alielekea katika nchi za Ujerumani na Uingereza kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu zaidi katika taaluma ya falsafa. Alianza kusoma mashairi akiwa kijana na shairi lake la kwanza alilipa jina la 'Naleh Yatiim' kwa maana ya kilio cha yatima. Allama Iqbal Lahori alikuwa mwanaharakati pia aliyepambana kwa minajili ya kuikomboa Pakistan kutoka mikononi mwa India. Allamah Muhammad Iqbal alifariki dunia mwaka 1938.
Miaka 99 iliyopita sawa na tarehe Tisa mwezi Novemba mwaka 1918, mfumo wa jamhuri ulitangazwa huko Ujerumani kufuatia kushindwa mara kadhaa jeshi la Unchi hiyo na vikosi vya waitifaki katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kuzuka uasi nchini humo. Matukio hayo yalipelekea kujiuzulu Wilhelm wa Pili mtawala wa mwisho wa kifalme wa nchi hiyo. Siku mbili baadaye mfalme huyo alikimbilia Uholanzi na hivyo utawala wa Kifalme ukawa umehitimishwa nchini Ujerumani. Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kufutwa utawala wa kifalme, Friedrich Ebert alishika madaraka ya nchi kama rais wa kwanza wa nchi hiyo.
Katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, ukuta wa Berlin ambao ulikuwa ukiugawa mji huo katika sehemu mbili za mashariki na magharibi kwa kipindi cha miaka 28 hatimaye ulivunjwa. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa mji huo lilikuwa likidhibitiwa na Urusi ya zamani, huku eneo la magharibi likidhibitiwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Machafuko yaliyotokea mjini Berlin hapo mwaka 1961 na wakazi wa mashariki kukimbilia upande wa magharibi, kulizitia wasiwasi serikali za Urusi ya zamani na Ujerumani mashariki, suala lililozipelekea nchi hizo kujenga ukuta huo ambao baadaye uliokana kuwa nembo ya kuwaganywa Ujerumani. Hata hivyo kuporomoka kwa Urusi ya zamani ambako kuliacha taathira kubwa pia katika tawala za kikomunisti za Ulaya mashariki kulipelekea kuvunjwa ukuta huo wa Berlin hapo mwaka 1989.