Jumapili 12 Novemba, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 23 Mfunguo Tano Safar 1439 Hijria, sawa na tarehe 12 Novemba, 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 177 iliyopita alizaliwa mjini Paris, Ufaransa Auguste Rodin, mtengeneza masanamu mashuhuru wa karne ya 19 Miladia. Uvutiwaji wake wa sanaa hiyo ulidhihiri tangu akiwa na umri mdogo. Miaka kadhaa baadaye alianza kuunda athari nzuri na za kuvutia na hivyo kupata umashuhuri kama mtengenezaji mashurhuri wa masanamu katika zama zake. Auguste Rodin alifariki dunia mwaka 1917 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita, alifariki dunia msomi mkubwa na mtaalamu wa fiq'hi ya Kiislamu Sheikh Muhammad Baqir Agha Najafi Isfahani. Sheikh Agha Najafi alizaliwa mnamo mwaka 1234 Hijiria nchini Iran na baada ya kusoma elimu mbalimbali za kidini mjini Isfahan, alielekea Najaf huko Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake. Baada ya kurejea kutoka Najaf msomi huyo aliweka makazi yake mjini Isfahan na kujikita katika kufundisha na kuwalea wanafunzi sambamba na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na "Lubbul-Fiq'h" na "Lubbul-Usuul."
Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita alizaliwa Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita maraajii na maulama wakubwa wa nchini Iraq, walitoa fatwa kwa ajili ya kukabiliana na uvamizi wa Uingereza dhidi ya nchi yao katika kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia. Katika kipindi hicho ardhi ya Iraq, ilikuwa ni sehemu ya utawala wa Othmania ambao askari wake walikuwa hawana uwezo wa kupambana na Uingereza. Baada ya fatwa hiyo Waislamu wa Kishia ambao walikuwa wakikandamizwa sana na utawala wa Othamania, waliamua kupambana na mvamizi huyo Mwingereza na kuitetea nchi yao ya Iraq bila kuzingatia ukandamizaji waliokuwa wakiupitia kutoka kwa watawala wao. Ushiriki wa baadhi ya maulama wakubwa katika harakati ya mapambano dhidi ya mkoloni huyo, ulizivutia hisia za wananchi na kuwafanya washiriki kwa wingi kupambana na mvamizi huyo. Hata hivyo kwa bahati mbaya, badala ya utawala wa Othmania kuziunga mkono harakati hizo na kushirikiana nazo, iliziona kama tishio dhidi yake na hivyo kuanza kuzikandamiza kwa lengo la kuzifuta kabisa, suala ambalo lilitoa mwanya kwa London kuidhibiti kikamilifu nchi hiyo. Hata hivyo baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia Waislamu wa Shia kwa mara nyingine walianzisha upya harakati ya kupambana na mvamizi Mwingereza.
Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita yaani Novemba 12 mwaka 1918, utawala wa kifalme ulifikia tamati nchini Austria na kuanza kipindi cha utawala wa Jamhuri baada ya kushindwa utawala wa Austria na Hungary katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutengana nchi hizo mbili. Mfalme wa mwisho wa Austria, Charles wa Kwanza ambaye alitawazwa kuwa mfalme wa nchi hiyo tarehe 21 Novemba mwaka 1916, alijiuzulu uongozi siku moja tu baada ya kutiwa saini makubaliano ya kusimamisha Vita vya Kwanza vya Dunia hapo tarehe 11 Novemba mwaka 1918 na kuomba hifadhi nchini Uswisi.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, askari wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji mengine ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika kambi kubwa ya Wapalestina mjini Rafah huko katika Ukanda wa Gaza. Jinai hiyo ilifanyika siku chache tu baada ya kutangazwa usitishaji vita baina ya Israel, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Misri. Hujuma hiyo ya kinyama ilisababisha mauaji ya Wapalestina 110, wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi wengine wapatao 1,000.
Na siku kama ya leo miaka 109 iliyopita yaani tarehe 12 Novemba mwaka 1908, Bulgaria ilijitangazia rasmi uhuru wake. Mwaka 1393 ardhi ya nchi hiyo ilivamiwa na utawala wa Othmania. Baada ya karne tano mnamo mwaka 1878, Bulgaria ilipata uhuru wa kiwango fulani. Bulgaria ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwa mfumo wa utawala wa kifalme, katika Vita Vikuu vya Kwanza na vya Pili vya Dunia ilipigana bega kwa bega na Ujerumani. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, kufuatia kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na Umoja wa Sovieti, mfumo wa Kisoshalisti ulianzishwa nchini humo.