Jumatatu, 13 Novemba, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 24 Safar 1439 Hijria sawa na 13 Novemba, 2017.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita hayati Hafidh Assad alichukua hatamu za uongozi wa Syria baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1970 na baadaye akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Hafidh Assad alizaliwa mwaka 1930 na mwaka 1964 alichaguliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha jeshi la Syria. Miaka mitatu baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Hafidh Assad alifariki dunia mwezi Juni mwaka 2000 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 13 Novemba 1970, tufani kubwa na kimbunga cha kutisha kiliikumba nchi ya Bangladesh. Janga hilo lilitokea wakati mapambano ya Wabangali kwa ajili ya kujitenga na Pakistan na kupata uhuru yalipokuwa kileleni. Tufani hiyo kubwa ilisababisha vifo vya watu laki mbili na kujeruhi wengine laki nane. Kimbunga na tufani hiyo pia iliwalazimisha mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao na kusababisha hasara kubwa katika mashamba, viwanda, makazi ya raia na miundombinu ya nchi hiyo. Bangladesh ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na majanga ya kimaumbile kama vimbunga, tufani na mafuriko ya mara kwa mara.
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita mwafaka na tarehe 22 Aban mwaka 1344 Hijria Shamsia, alifariki dunia mwandishi na mhakiki mkubwa wa Kiirani, Said Nafisi akiwa na umri wa miaka 71. Baada ya kupata elimu ya upili, Nafisi alielekea Ufaransa kwa ajili ya elimu ya juu. Baada ya kumaliza masomo yake huko Ufaransa alirejea Iran na kufunza katika vyuo vikuu hapa nchini. Said Nafisi ameandika na kutarjumu vitabu zaidi ya 180 ikiwemo kamusi ya lugha ya Kifaransa na Kifarsi.
Siku kama ya leo miaka 1054 iliyopita Sahib bin Ubbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami alifariki dunia. Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mashuhuri sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake. Sahib bin Ubbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al Muhiit" chenye juzuu saba.